Miezi sita iliyotolewa na Waziri wa Viwanda na Biashara kwa ajili ya kupima utendaji kazi wa Bodi na Manejimenti ya Shirika la Viwango nchini (TBS) imekamilika na hapa Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Joseph Masikitiko anaeleza mafanikio yaliyofikiwa kama alivyohojiwa na Mwandishi Wetu, EDMUND MIHALE.

Swali: Ni mafanikio gani kwa ujumla ambayo yamepatikana ndani ya miezi sita ya uongozi mpya wa Shirika?

 

Jibu: Katika kipindi cha miezi sita Shirika limepata mafanikio katika maeneo  mbalimbali ikiwa ni pamoja na kukuza uelewa wa wazalishaji na walaji  kuhusu masuala ya viwango na udhibiti ubora wa bidhaa  zinazozalishwa hapa nchini na zile zinazotoka nje ya nchi. Hili limewezekana kwa kutumia vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na magazeti, redio na televisheni.

 

Vilevile katika kipindi hicho Shirika limeweza kufunga maduka makubwa mawili yanayouza nondo, viwanda vya nondo vinne vya maji viwili, mikate kumi na sita, sabuni ya unga kimoja, nyanya rojo (Tomato sauce) kimoj na chakula cha mifugo kimoja. Bidhaa hizi hazikuwa zimethibitishwa ubora wake. Kati ya viwanda hivyo, 10 vimeshatuma maombi na kupata leseni ya ubora na 18 viko katika utaratibu wa kupata leseni.

 

Mbali ya viwanda vilivyofungiwa na Shirika, pia viwanda 48 vilitangazwa kufutiwa leseni baada ya kukiuka utaratibu,  ikiwamo kukwepa ukaguzi, kuhamisha maeneo ya uzalishaji, kusitisha uzalishaji na baadhi  kutolipia ada ya kila mwaka. Kati ya viwanda hivi, vitatu vimeshafunguliwa baada ya kufuata taratibu.

 

Viwanda hivyo ni pamoja na kile kinachozalisha sabuni ya Klin, mifuko ya visafeti na Gypsum Board (Tangypsum).

 

Vilevile Shirika limetoa leseni mpya 94 za kutumia alama ya ubora wa TBS kwa wazalishaji mbalimbali nchini. Aidha,  Shirika limepata maombi mapya zaidi ya 200 ya leseni za alama ya ubora katika kipindi cha miezi sita.

 

Idadi hii ni kubwa ikilinganishwa na malengo ya maombi 80 kwa miezi sita. Pia kwa upande wa ukaguzi wa awali kwa walioomba leseni, Shirika limekagua viwanda vipya 89 ikilinganishwa na malengo ya kukagua viwanda 40 katika kipindi cha miezi sita.

 

Idadi hii imekuwa kubwa kutokana na ongezeko la maombi ya leseni.

Kwa upande wa ukaguzi wa bidhaa sokoni, sampuli 74 zilichukuliwa kutoka kwenye maduka na kupimwa maabara.

 

Idadi hii imevuka lengo la kuchukua sampuli 60 kwa miezi sita. Vilevile kwa upande wa bidhaa kutoka nje ya nchi, jumla ya vyeti vya ukaguzi (CoC) 8,106 vilitolewa ingawa malengo ilikuwa ni CoC 6,000 katika kipindi cha miezi sita.

Vilevile jumla vya vyeti 13,496 vya ukaguzi wa magari vilitolewa wakati malengo ilikuwa ni kukagua magari 7,500. Mafanikio hayo yote yanatokana na usimamizi mzuri na uelewa wa wafanyabiashara juu ya umuhimu wa ubora.

 

Katika utayarishaji wa viwango vya kitaifa, Shirika limetayarisha viwango 139 wakati lengo lilikuwa ni kutayarisha viwango 95.

 

Swali: Je, jitihada za Shirika za kuwabana wazalishaji wasiofuata Sheria ya Viwango Na.2 ya 2009 kwa kuzuia uzalishaji kwa muda zinazaa matunda?

 

Jibu: Jitihada za kuwabana wazalishaji wasiofuata sheria ya viwango kwa kuzuia uzalishaji kwa muda zinazaa matunda kwani kumekuwa na mwamko kwa wazalishaji ambao wamejitokeza kwa wingi kuomba leseni za kutumia alama ya ubora ya TBS. Mathalani maombi mapya ya leseni kwa sasa ni zaidi ya 200 ambayo ni idadi kubwa ikilinganishwa na malengo ya maombi ya leseni 80 katika kipindi cha miezi sita.

 

Swali: Kuna kikwazo gani kinachowazuia wazalishaji kutofuata utaratibu? Je, ni uelewa mdogo au ni uzembe tu?

 

Jibu: Baadhi ya wazalishaji hasa wale wanaokiuka utaratibu kwa kutothibitisha ubora wa bidhaa wanazozizalisha, wanapohojiwa hueleza kuwa hawakuwa na uelewa wa masuala ya viwango na wengine wanaelewa masuala ya viwango lakini hawakuona umuhimu.

 

Swali:  Je, ukaguzi wa Shirika wa mara kwa mara na wa kushitukiza viwandani umeleta mafanikio yoyote hasa katika uzalishaji endelevu wa bidhaa zenye ubora?

 

Jibu: Lengo kubwa la kufanya ukaguzi wa mara kwa mara  na wa kushitukiza ni kuhakikisha kuwa wazalishaji wanazalisha bidhaa zenye ubora wakati wote. Kwa kufanya hivyo, inawasaidia wazalishaji kuwa macho katika kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango.

Swali: Una wito gani kwa wazalishaji, waagizaji na walaji juu ya umuhimu wa kufuata Sheria ya Viwango?

 

Jibu: Shirika linatoa wito kwa wazalishaji kuendelea kuzalisha bidhaa bora na ambazo zimethibitishwa na TBS. Waagizaji wahakikishe kuwa bidhaa wanazoingiza nchini zimekaguliwa na wakala  wetu katika nchi  mbalimbali zinakotoka. Endapo bidhaa hizo zitaingizwa bila kukaguliwa,  waagizaji kwa mujibu wa sheria,  wanatozwa faini ya asilimia 45% ya gharama ya mzigo (CIF).  Baada ya kulipa faini hiyo bidhaa hizo hupimwa na kama zitaonekana ni hafifu, mwagizaji anawajibika kuharibu au kurudisha  bidhaa hizo katika nchi zilikotoka.

Wito wetu kwa walaji ni kwamba wao ni wadau muhimu sana katika kupambana na bidhaa hafifu, kwani kama watazikataa bidhaa hizo waagizaji hawawezi kuendelea kuzileta nchini na wazalishaji pia wataacha kuzalisha. Kwa kununua bidhaa zenye ubora walaji hupata thamani ya pesa zao. Kwa upande wa wazalishaji na waagizaji, viwango huwapa  uhakika wa soko  la bidhaa zao ndani na nje ya Tanzania

Swali: Umesema katika kipindi cha miezi sita iliyopita kuna baadhi ya viwanda ambavyo mlivifungia na kuvifungua baadaye. Je, uongozi wa viwanda hivyo umeahidi kufuata utaratibu bila ya  kufuatwa fuatwa?

 

Jibu: Katika kipindi cha miezi sita baadhi ya viwanda  vilifungiwa na baadaye kufunguliwa baada ya kufuata utaratibu wa kuzalisha bidhaa kwa kuzingatia viwango. Wazalishaji hao wameahidi na wanaendelea kuzalisha kwa kufuata matakwa ya viwango. Wakati huo huo, Shirika limekuwa likifanya ukaguzi wa kushitukiza ili kuhakikisha kuwa wazalishaji hao hawakiuki utaratibu.

 

Swali: Je, Serikali ina  msimamo gani kuhusu mitumba ya nguo za ndani inayoagizwa kutoka nje ya nchi?

 

Jibu: Serikali itaendelea na msimamo wake wa kuzuia nguo za ndani za mitumba kwa kuwa ziko katika kiwango cha lazima ambacho ni TZS 758:2003. Kiwango cha nguo za mitumba kimeeleza wazi kuwa nguo za ndani za mitumba hazitakiwi kuingizwa na kuuzwa nchini kutokana na sababu za kiafya na kiusalama. Sababu hizo ni pamoja na maambukizi ya magonjwa ya ngozi.Tunaendelea kutoa wito kwa waagizaji wa nguo za mitumba kuwa  wanapoagiza nguo hizo wahakikishe hawaagizi nguo za ndani.

 

Swali: Je, mmeshatoa elimu kwa waagizaji juu ya madhara ya nguo hizo?

 

Jibu: Elimu imetolewa  kwa waagizaji wa nguo za mitumba kupitia njia mbalimbali ikiwa ni pamoja na mkutano wa pamoja na waagizaji wa mitumba kabla ya kuanza utekelezaji wa kiwango cha mitumba. Elimu pia imetolewa kupitia matangazo ya redio, televisheni, magazeti na matangazo ya barabarani.

Swali: Shirika kwa sasa lina mipango gani ya kuwawezesha kielimu wazalishaji wa kati na wakubwa ili wazalishe bidhaa zenye ubora?

 

Jibu: Moja ya majukumu ya Shirika ni kutoa mafunzo kwa wazalishaji wa bidhaa kuanzia wadogo, wa kati na wakubwa. Jukumu hili ni endelevu na mafunzo haya yamekuwa yakitolewa viwandani, katika maonesho na makongamano mbalimbali. Mathalani hivi karibuni Shirika lilitoa mafunzo kwa wazalishaji wa mikoa ya Singida, Manyara, Dodoma na Kigoma. Vilevile Shirika limeshiriki katika maonesho yaliyofanyika katika mikoa ya Tanga, Manyara, Dodoma Arusha na Dar es Salaam.  Utaratibu huu kwa kiasi kikubwa umekuza uelewa wa wazalishaji kuhusu masuala ya viwango na udhibiti ubora.

 

Swali: Kuna baadhi ya bidhaa kama mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi hivi karibuni mliutangazia umma kwamba hayafai kwa matumizi ya binadamu, je, wananchi wameupokeaje ushauri wenu huo?

 

Jibu: Shirika la Viwango limepewa dhamana ya kuhakikisha  kuwa wananchi wakati wote wanapata bidhaa zenye ubora, hivyo basi endapo bidhaa isiyo na ubora inabainika kuwepo sokoni ni jukumu la Shirika kuhakikisha kuwa bidhaa hiyo inaondolewa mara moja ili isilete madhara kwa watumiaji.

 

Ni katika mtazamo huo, Shirika lilitangaza uwepo wa mafuta ya kupikia hafifu ya Nasma, Oki na Viking yenye ujazo wa lita moja, mbili na tatu, ambayo yaliingia nchini kupitia njia zisizo halali na yalipopimwa ikabainika kuwa hayakukidhi matakwa ya kiwango cha kitaifa. Hivi karibuni Shirika lilifanya utafiti katika maduka mbalimbali Jijini Dar es Salaam na kubaini kuwa wauzaji wameshayaondoa mafuta hayo.

 

Hata hivyo, tutaendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na wa kushitukiza ili kujiridhisha kuwa mafuta katika ujazo huo hayaingii tena sokoni. Wananchi wanapoona kuwa Shirika linasimamia utekelezaji wa viwango na suala la ubora kwa ujumla wanakuwa na imani na kujua kuwa afya   na usalama wao vinalindwa.

 

Swali: Kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto katika udhibiti wa ubora wa mafuta ya kuendeshea magari na mitambo. Shirika limejizatiti vipi kukabiliana na changamoto hii?

 

Jibu: Shirika la Viwango linayo maabara ya Kemia ambayo hupima bidhaa mbalimbali zikiwamo za mafuta ya petrol, dizeli na mafuta mazito. Pia hivi karibuni Waziri wa Viwanda na Biashara, Mh. Dkt. Abdallah Kigoda alizindua mtambo ujulikanao kitaalamu kama Correlative Fuel Research Engine ambao ni maalum kwa kupima kipimo kijulikanacho kitaalamu kama Research Octane Number (RON) katika mafuta ya petroli.

 

Pamoja na mambo mengine, mtambo huu hupima uwezo wa mafuta kuzuia kuharibika kwa injini za magari kunakosababishwa na ubovu wa mafuta (knock intensity engine). Pia hupima uwezo wa uharibifu wa injini za magari unaotokana na kuwahi kulipuka kwa mafuta kabla ya muda unaotakiwa.

 

Shirika la Viwango Tanzania ni shirika pekee nchini na Afrika nzima kwa kuwa na mtambo huu wa kisasa (semi-automatic) wa kupimia ubora wa mafuta aina ya petroli ambao umegharimu shilingi bilioni moja na laki moja. Ununuzi na ufungaji wa mtambo huu muhimu  na vifaa vingine unalipa Shirika uwezo wa kupima mafuta ya kuendeshea magari, ndege na mitambo mbalimbali kabla ya kuingizwa nchini yakiwemo mafuta ya dizeli, petroli, mafuta ya taa na mafuta mazito.

 

Swali: Je, TBS inashirikiana  vipi na Shirika la Viwango la Zanzibar (ZBS) katika kudhibiti uingizwaji wa bidhaa zisizo na ubora kupitia Zanzibar?

 

Jibu: TBS na ZBS zimeshaanza mazungumzo kuhusu namna ya kukabiliana na bidhaa hafifu zinazoingia kupitia Zanzibar. Mazungumzo hayo ni pamoja na kuangalia utaratibu wa kukagua bidhaa zote huko zinakotoka kupitia mfumo wa PVoC kwa kutumia wakala wa kimataifa  wanaotumiwa na TBS ambao ni  SGS ya Uswisi, Bureau Veritas ya Ufaransa na Intetek ya Uingereza.  Mazungumzo haya yanaendele na yatakapokamilika tutakuwa tumepiga hatua kubwa sana katika kudhibiti bidhaa zisizo na ubora kuingia nchi Tanzania.

 

Swali:  Katika harakati zake za kudhibiti ubora, TBS inashirikiana vipi na wadau wengine katika nyanza ya ubora?

 

Jibu:        Shirika lina uhusiano wa karibu na taasisi mbalimbali nchini na hususan zile  zinazohusika na kudhibiti ubora kama vile, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Tume ya Ushindani (FCC), Polisi na  Shirikisho la wenye Viwanda Tanzania (CTI).

 

Lengo la ushirikiano ni kuwa na jitihada za pamoja za  kupunguza au kuondoa bidhaa hafifu sokoni.  Hivi sasa tupo katika hatua za awali za kuzishirikisha Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili ziweze kutunga sharia ndogondogo kwa ajili ya kutekeleza sheria ya viwango Na. 2 ya mwaka 2009.  Hii ni kwa mujibu wa kifungu 36(20 ya sheria hiyo.

 

Swali: Nini tathmini ya mafanikio ya Sheria  mpya ya Viwango ambayo kwa sasa ina meno? Je, inawabana waagizaji bidhaa wajanja wajanja kama ilivyokusudiwa?

 

Jibu: Sheria ya Viwango No.2 ya mwaka 2009 imelipa Shirika nguvu zaidi za kiutendaji kwani imeweza kudhibiti wale wote wanaokiuka taratibu tofauti na ilivyokuwa kwa Sheria ya awali No 3 ya mwaka 1975 ambayo ilikuwa haina nguvu katika utekelezaji. Kwa mujibu wa Sheria ya Viwango ya sasa mzalishaji anayekiuka utaratibu anaweza kutozwa faini ya kuanzia shilingi milioni 50 mpaka milioni 100 au kifungo kisichopungua miaka miwili jela.

 

Kumekuwepo na ongezeko la wafanya biashara kuzingatia viwango, kwa sababu sheria mpya imeongeza   adhabu kwa wakosaji chini ya kifungu cha 27 na 30 cha sheria ya viwango. Utendeja wa kazi za udhibiti ubora, katika Shirika umeongezeka kwani kurugenzi  mahususi inayoshughulikia  suala hilo imeimarishwa.

 

Swali: Hivi karibuni mlikuwa na mkutano wa mashirika ya Viwango ya Jumuiya ya Afrika  Mashariki, ni yapi maazimio ya pamoja katika mkutano huo hasa katika udhibiti wa uingizwaji bidhaa hafifu hapa nchini?

 

Jibu: Mashirika ya viwango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kila mwaka yamekuwa yakikutana na  kujadili masuala mbalimbali kuhusu  udhibiti ubora, viwango, ugezi na upimaji.  Uwianishaji wa Viwango vya Afrika Mashariki ni mojawapo ya masuala muhimu yanayojadiliwa na kupitishwa, vilevile kuwa na viwango vya Afrika Mashariki. Viwango hivi vikiwianishwa vinatumika katika nchi wanachama ili kuondoa vikwazo vya kibiashara.

 

Swali: TBS ina ushauri gani kwa umma kuhusu matumizi ya bidhaa zenye alama ya ubora ya TBS?

 

Jibu: Ushauri wa TBS kwa umma kuhusu matumizi ya bidhaa zenye alama ya ubora ya TBS ni kwamba inapobainika kuwa bidhaa iliyothibitishwa ubora wake na TBS iko chini ya kiwango wasisite kuwasilina nasi kwa namba ya bure ya 0800110827 kwa kutumia mitandao ya Vodacom, TTCL na Sasatel. Shirika litatoa ushirikiano kwani kwa kufanya hivi tutafanikiwa kuondoa bidhaa hafifu katika soko la Tanzania.