Shirika la Viwango Tanzania (TBS) mkoani Kilimanjaro limekifungia kiwanda cha kusindika maziwa cha Kilimanjaro Creameries Ltd (KCL) kilichopo Sanya Juu baada ya kubainika kutumia namba feki za ubora za shirika hilo kinyume cha Sheria ya Viwango ya mwaka 2009.
Uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umebaini kuwa mbali na kukifunga, TBS imekitoza kiwanda hicho faini ya Sh milioni tatu baada ya wamiliki wake kukiri kosa la kutumia namba feki ambazo ziliiaminisha walaji kuwa maziwa hayo ni salama, ilhali ukweli ukiwa kwamba ubora huo haujathibitishwa.
Maziwa hayo yalibainika kuwa na namba TZS-1220 na TZS-251 huku uchunguzi ukibaini kuwa TBS haijawahi kutoa namba hizo; hivyo kukiuka sheria namba 2 ya mwaka 2009.
Mkurugenzi wa TBS kupitia Ofisa Masoko wake, Gladness Kaseka, ameliambia JAMHURI kuwa mbali na kukifungia kiwanda hicho, jalada la uchunguzi limefunguliwa ikiwa ni hatua za kisheria.
TBS imechukua sampuli 10 za bidhaa zinazozalishwa na kiwanda hicho kwa ajili ya vipimo zaidi.
Katika majibu kwa maswali aliyoulizwa juu ya hatua zilizochukuliwa dhidi ya kampuni hiyo, Kaseka alisema kuwa TBS ilitumia kifungu cha 30(1) kuitoza faini ya Sh milioni tatu kampuni hiyo baada ya wamiliki wake kukiri kukiuka matakwa ya sheria.
Kifungu kidogo cha pili kinaipa nguvu TBS kumtoza faini ya Sh milioni 20 endapo itabainika kuwa mkosaji amekiuka sheria hiyo.
Akifafanua zaidi ofisa huyo alisema kuwa kifungu cha 27 (1) cha Sheria ya viwango nambari 2 ya mwaka 2009 kinaeleza bayana kwamba endapo mtenda kosa wa aina hii atahukumiwa ni wazi kuwa atatumikia kifungo jela kwa muda usiopungua miaka miwili au atapigwa faini na Mahakama ya Sh milioni 50 hadi Sh milioni 100; ama adhabu zote kwa pamoja.
Adhabu katika kifungu cha 27(1) cha Sheria ya viwango inatekelezwa endapo mkiukaji hatakubali kuwa amekiuka sheria tajwa na kufikishwa mahakamani. Shirika limekuwa likiwaadhibu wakiukaji wanaokiri kukiuka sheria kwa kutumia kifungu cha 30(1) (2) cha Sheria ya Viwango.
Kaseka amesema zipo kampuni nyingi zinazovunja sheria za TBS, baadhi zikiwa ni Deniz company Ltd, Murzah Soap and Detergents and Water com T (Ltd) na kwamba TBS inaendelea kufanya ukaguzi.
Yafuatayo ni mahojiano ya Mwandishi wa JAMHURI na TBS:
JAMHURI: Je, baada ya kukifungia kiwanda hicho kama hatua za awali ni hatua gani zaidi Shirika lako limechukua dhidi ya kampuni hiyo kwa kukiuka sheria namba 2 ya mwaka 2009 ya viwango kwa kutumia namba bandia bila kupitia mchakato wa uthibitisho?
TBS: Hatua ya kwanza iliyochukuliwa na Shirika ilikuwa ni kukifungia kiwanda cha KCL. Pili, shauri hili liliripotiwa Polisi kwa ajili ya hatua stahiki.
Tatu, kama ilivyoelekezwa na Sheria ya Viwango nambari 2 ya mwaka 2009 katika kifungu cha 30(1) na (2) kwamba Shirika linaweza kumpiga faini mkiukaji wa sheria tajwa ya viwango isiyozidi millioni ishirini endapo itabainika kwamba amekiuka sheria hiyo kwa kutenda kosa na amekiri kukiuka sheria hiyo.
Hivyo baada ya KCL kukiri kukiuka matakwa ya sheria, Shirika liliamua kutumia kifungu kilichotajwa hapo juu yaani kifungu cha 30(1) cha sheria ya viwango kumtoza faini ya shilling millioni tatu kama adhabu ya kutenda kosa hilo.
JAMHURI: Je, sheria zenu zinasemaje kwa mtu au kampuni inayobainika kufanya udanganyifu wa aina hiyo?
TBS: Kifungu cha 27 (1) cha Sheria ya Viwango nambari 2 ya mwaka 2009 inaeleza bayana kwamba endapo mtenda kosa wa aina hii atahukumiwa ni wazi kwamba atatumikia kifungo jela kwa muda usiopungua miaka miwili ama atapigwa faini na Mahakama kati ya Sh milioni 50 na Sh milioni 100, ama adhabu zote kwa pamoja.
Adhabu katika kifungu cha 27(1) cha Sheria ya Viwango inatekelezwa endapo mkiukaji hatakubali kuwa amekiuka sheria tajwa na kufikishwa mahakamani. Shirika limekuwa likiwaadhibu wakiukaji wanaokiri kukiuka sheria kwa kutumia kifungu cha 30(1) (2) cha Sheria ya viwango.
JAMHURI: Je, upi mwito wenu kwa wananchi ambao hawana uelewa juu ya namba zinazotumiwa na kampuni mbalimbali kuonyesha kuwa bidhaa zao zimethibitishwa na TBS wakati si kweli?
TBS: Wananchi wanapopata shaka na alama ya ubora katika bidhaa yoyote wasisite kuwasiliana nasi kwa namba 0800 110 827.
JAMHURI: Upi mwito wenu kwa kampuni ambazo zinatumia udanganyifu wa aina hiyo na kuwalisha wananchi bidhaa zisizokuwa na ubora?
TBS: Waache mara moja kwani wakibainika hatua kali za kisheria zitachukuliwa.