Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Joseph Masikitiko, amesema shirika hilo limeteketeza nondo tani 500 zenye thamani ya Sh bilioni 8, baada ya kubaini hazina ubora unaotakiwa kwa ajili ya matumizi ya ujenzi.
Nondo hizo zilipatikana baada ya kufanya ukaguzi na kuvifungia viwanda vinne vinavyozalisha nondo katika Jiji la Dar es Salaam.
Viwanda vilivyofungiwa ni Metro Steel Mills kilichoko Vingunguti, Dar es Salaam, Quaim Steel Mills kilichopo Chang’ombe wilayani Temeke, Am Steel na Dar Steel vyote vya Mbagala, Zakhem.
Hatua hiyo imekuja baada ya kubainika kwamba vimekuwa vikizalisha na kuuza nondo zisizo na ubora unaotakiwa na vingine vikizalisha nondo bila kuwa na kibali cha TBS.
Masikitiko aliwaambia waandishi wa habari baada ya shirika kutoa semina kwa wazalishaji wa nondo jijini Dar es Salaam wiki iliyopitana kusema kuwa nondo hizo zimebainika kutokuwa na viwango vya ubora unaotakiwa na ni hatari kwa shughuli za ujenzi.
“Licha ya kuteketeza nondo zisizo na viwango, pia tumekusudia kuhakikisha kuwa nondo zote zinakuwa na nembo ya TBS, na zinaonesha madaraja ya viwango vyake, kwa sababu zinatofautiana kwa matumizi,” amesema Masikitiko.
Amesema wakikamilisha kazi hiyo, watafanya kazi nyingine ya kukagua viwanda vya maji ya kunywa na vile vinavyotengeneza mabati. Hatua hiyo inatokana na ukweli kwamba baadhi ya viwanda hivyo, vinazalisha bidhaa zisizokuwa na ubora unaokubalika.
Amedai kuwa TBS sasa itashirikiana na halmashauri zote kuhakikisha wajasiriamali wakubwa na wadogo wanazalisha bidhaa zilizo na viwango vinavyotakiwa, na kuwa kazi ya kukamata na kuteketeza bidhaa zisizo na kiwango ni endelevu na itafanyika nchi nzima.
Masikitiko amesema tayari amewaandikia barua ya kuwataarifu wafanyabiashara na wazalishaji wa bidhaa nchini, kuhakikisha wanaharibu mali zote zisizo na kiwango kabla TBS haijachukua hatua.
“Zoezi hili ni endelevu na la nchi nzima, tutaziharibu mali zote zisizo na ubora wa kiwango… tumewaandikia kuwapa tahadhari wafanyabiashara na wazalishaji wote kuwa tutafanya msako wa nchi nzima ili kubaini bidhaa hizo,” amesema Masikitiko.
Ili kufanikisha hilo, wameendesha semina kwa wakaguzi wote nchini kutoka idara tofauti za serikali. Semina hiyo iliendeshwa mwishoni mwa wiki Jijini Dar es Salaam. Amesema lengo la semina hiyo ni kuhakikisha kuwa wakaguzi hao wanafanya kazi kwa mujibu wa sheria za TBS.
“Unajua kuwa kwa sasa operesheni zote tunazofanya tunaongozana na mwanasheria ili atoe elimu kwa watu wanaovunja sheria za viwango, haiwezekani akatembea nchi nzima.
“Lakini tukiwapa elimu hawa wakaguzi watafanya kazi huku wakijua kuwa wanafanya nini na kwa sheria ipi, baada ya hapo tutamwandikia waziri barua waanze kazi, tumedhamiria kumaliza bidhaa mbovu zisizo na viwango na hili linawezekana,” amesema Masikitiko.
Hata hivyo, Masikitiko amesema pamoja na kuwa shirika hilo lina upungufu wa wafanyakazi, kwa kiasi kikubwa litafanya kazi kwa uadilifu mkubwa.
Amesema kuwa hadi sasa TBS inawafanya kazi 197 nchi nzima.
Akizungumzia sheria ya ubora wa viwango nchini Mwanasheria wa Shirika hilo, Baptister Bitaho, amesema kuwa shirika limepewa jukumu kwa mujibu wa kifungu cha sheria cha 3(2) cha sheria Na. 2 ya mwaka 2009 kuwa mwangalizi na msimamizi wa uzingatiaji wa viwango nchini.
Amesema vile vile chini ya kifungu cha 4 (1)(a) cha sheria hiyo hiyo na mazingira ya aina yoyote ili kujenga uzingatiaji wa viwango kwenye sekta ya viwanda na biashara.
“Hivyo basi wazalishaji na wasambazaji wa bidhaa zote zikiwamo nondo, ni muhimu kuzingatia matarajio ya TBS kuhusu viwango vya bidhaa hizo,” amesema Bitaho.
Amesema kwa mujibu wa sheria ya viwango zipo aina mbili za viwango – nazo ni viwango vya hiari na vya lazima.
“Viwango vya hiari ni vile ambavyo havina athari ya moja kwa moja kwa mtumiaji na kwa mazingira, kwa mfano, kiwango cha karatasi mzalishaji anapozalisha saizi ya karatasi kinyume na kiwango husika, hakuna madhara kwa mtumiaji wa karatasi hiyo.
“Ambapo mzalishaji anapaswa kuzingatia kiwango hicho, vinginevyo anaweza kusababisha madhara makubwa kwa mtumiaji na mazingira yanayomzunguka,” amesema Bitaho.
Amesema viwango vya lazima ni vile ambavyo vina athari ya moja kwa moja kwa mtumiaji kwa mazingira.
Ametoa mfano kuwa vyakula, nondo, mabati na nyaya za umeme n.k. ndivyo vilivyo katika viwango vya lazima.
Mzalishaji anapokiuka matakwa ya viwango hivyo, madhara yake yanakuwa makubwa kwa afya mlaji na mazingira yanayomzunguka.
Amesema kifungu cha 20 cha sheria ya viwango kinampa waziri mamlaka ya kutoa tamko la kiwango kuwa cha lazima. “Tamko hilo huzingatia vigezo vya kiwango cha lazima kama ilivyoelezwa awali. Kwa hiyo, bidhaa kama nondo ni moja ya bidhaa zinazoangukia katika viwango vya lazima (compulsory standards), kwa sababu kujengea nondo isiyo na ubora inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwamo vifo kwa kuporomoka kwa majengo,” amesema.
Amesema kanuni za udhibiti ubora (Tangazo la Serikali namba 406 la mwaka 2009) linamtaka mzalishaji mwenye leseni kuzingatia masharti yaliyomo kwenye leseni
Pia amesema kanuni ya 15 inamtaka mwenye kiwanda kufuata masharti ya mpango wa ukaguzi na utahini ambayo ni pamoja na masharti mengine.
Amesema pia inamtaka mzalishaji kuhakikisha kwamba anazalisha bidhaa inayokidhi kiwango, vinginevyo atafutia leseni ya alama ya bidhaa ya ubora.
Amesema kuwa ni kosa la jinai kukiuka masharti ya leseni yaliyoainishwa katika kanuni zilizotajwa hapo juu, iwapo mwenye leseni kwa makusudi atazalisha bidhaa ambayo haikidhi viwango vya ubora na kuziingiza sikoni.
Amesema kuwa kwa kufanya hivyo atakuwa amekiuka masharti hayo na adhabu yake ni kifungo au faini kuanzia Sh milioni 50 hadi Sh milioni 100 kwa mujibu wa kifungu cha 27 cha Sheria ya Viwango namba 2 ya 2009.
“Lakini iwapo pia mzalishaji atatumia vibaya leseni ya ubora, atakuwa amekiuka taratibu za leseni ya ubora, hivyo adhabu yake haitofautiani na adhabu iliyotajwa hapo juu.
“Tunatoa rai kwa wazalishaji wote wa nondo kuzifuata taratibu zilizoainishwa katika sheria iliyotajwa pamoja na kanuni zake ili kulinda usalama wa wananchi na kukuza uchumi wa taifa,” amesema.