Kuzinduliwa kwa mtambo mpya wa kupima mafuta kunaashiria kwisha kwa tatizo la muda mrefu la kuharibika kwa injini za magari yanayotumia mafuta ya petroli nchini. Mtambo huo wa kisasa uliozindulia wiki iliyopita na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda,  jijini Dar es Salaam, ni miongoni mwa mitambo inayopima mafuta ya magari iliyopo katika maabara ya kemia.

Awali Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lilikuwa linalipa dola  250.00 za Marekani nchini Kenya kama gharama ya kupima sampuli moja ya mafuta ya petroli.

 

Ununuzi na ufungaji wa vifaa hivi muhimu vya maabara vinalipa shirika uwezo wa kupima mafuta ya kuendeshea magari, ndege na mitambo mbalimbali kabla ya kuingizwa nchini yakiwamo mafuta ya dizeli, petroli, mafuta ya taa (dual purpose kerosene) na mafuta mazito (heavy fuel oil).

 

Akizungumuza katika uzinduzi huo, Kaimu Mkurugenzi wa TBS, Joseph Masikitiko, amesema kitaalamu mtambo huo unaitwa Correlative Fuel Research Engine (CFR engine).

Amesema TBS ni shirika pekee Afrika kuwa na mtambo huo wa kisasa (semi-automatic) wa kupimia ubora wa mafuta aina ya petroli.

 

Amesema mtambo huo umeligharimu shirika hilo dola laki saba za Marekani ambazo ni sawa Sh. 1.1 bilioni za Tanzania.

 

“Katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, mtambo kama huu upo Mombasa lakini ni manual si kama huu tulionao,” amesema Masikitiko.

 

Amesema ni mtambo huo maalum na muhimu unaotumika kupima kipimo kinachoitwa kwa kitaalamu Research Octane Number (RON), katika mafuta aina ya petroli.

 

Pamoja na mambo mengine, mtambo huu hupima uwezo wa mafuta kuzuia kuharibika kwa injini za magari kunakosababishwa na ubovu wa mafuta (knock intensity engine).

 

Masikitiko amesema mtambo huo hupima uwezo wa uharibifu wa injini za magari unaotokana na kuwahi kulipuka kwa mafuta kabla ya muda unaotakiwa.

 

“Iwapo mafuta yatashindwa kukidhi matakwa ya kiwango husika, aidha, injini haitawaka kabisa, au itaishiwa nguvu na kusababisha kuzima kwa gari au kung’oka kwa sehemu za injini zinazopishana kama vile pistoni na gia, hivyo kusababisha kuharibika (knock)) kwa injini,” amesema Masikitiko.

 

Amesema kwamba shirika lina imani kubwa kwamba mitambo hiyo ya kisasa itaongeza ufanisi kiutendaji, hasa katika utoaji matokeo ya vipimo  yenye uhakika na ya kuaminika kwa haraka. Kufungwa kwa mtambo huo kumekwenda sanjari na kutoa mafunzo maalumu  ya kutumia mitambo na kupima mafuta ndani na nje ya nchi, wafanyakazi nao kwa sasa wana weledi wa kutosha katika eneo hilo.

 

Masikitiko amesema TBS ina maabara nane zenye vifaa vya kisasa na wataalamu wenye weledi wa kutosha na waliobobea katika kazi za upimaji.

 

Amezitaja maabara hizo kuwa ni maabara ya kemia ambayo pia inahusika na upimaji wa mafuta ya magari kwa kutumia mtambo uhandisi umeme, uhandisi mitambo, uhandisi ujenzi, chakula na mazao ya kilimo, ngozi na nguo, kondomu na maabara ya kupima ubora wa pamba katika kanda za     Afrika Mashariki na Kusini.

 

Amesema shirika lina Kituo cha Teknolojia ya Ufungashaji ambacho kinatoa huduma ya upimaji wa nyenzo za kufungashia na kuratibu maendeleo ya tasnia ya ufungashaji.

 

Amesema kati ya maabara hizo nane tayari maabara nne zimekwisha pata umahiri (Accreditation) katika ugezi (calibration) na upimaji wa sampuli mbalimbali baada kuidhinishwa na Shirika la umahiri wa maabara la Afrika kusini (South Africa Accreditation Systems- SANAS).

 

Amesema maabara hizo ni pamoja na ugezi, kemia, chakula na kondomu. Hata hivyo maabara nyingine zikiwemo za upimaji mafuta ya magari (fuel lab), uhandisi na pamba ziko katika matayarisho ya kupata umahiri katika utendaji wake.

“Ni matarajio ya Shirika kuwa hadi kufikia mwezi Disemba mwaka 2013 maabara zote zitakuwa zimehakikiwa na kutambulika kimataifa.

 

“Shirika la Viwango Tanzania limekuwa likitenga fedha kutokana na mapato yake kidogo  ya ndani, ili kununua vifaa hivi. Hali hii imelifanya Shirika kushindwa kununua vifaa  vya kisasa vya maabara  kutokana na uwezo mdogo wa kifedha.

 

“Licha ya Shirika kugharamia ununuzi wa vifaa vya maabara kwa kutumia vyanzo vya mapato vya ndani, vifaa vingi tumevipata pia kutokana na misaada ya wahisani na wafadhili mbalimbali yakiwemo mashirika ya misaada ya kimataifa kama vile mfuko wa maendeleo wa nchi za Ulaya (EDF), Shirika la Maendeleo la Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO), Shirika la Maendeleo la Denmark (DANIDA) na Shirika la Maendeleo la Uswisi (SECO) amesema Masikitiko.

 

Matatizo yanayolikabili shirika

Masikitiko amesema pamoja na jitihada nyingi zinazofanywa na shirika lake katika kuboresha utendaji, lakini maabara zimeendelea kukabiliwa na matatizo mbalimbali. Ameyataja matatizo hayo kuwa ni ufinyu wa nafasi ya kufanyia kazi za upimaji, kuweka vifaa vya kupimia pamoja na sehemu ya kukaa wafanyakazi wa maabara.

 

Amesema hali hiyo inatokana  na ongezeko la viwanda vidogo na vya kati pamoja na ongezeko la bidhaa kutoka nje, linaloenda sanjari na uhitaji wa upimaji ubora wa bidhaa hizo.

 

Ametaja tatizo jingine kuwa ni uhaba  wa vifaa vya kutosha kuhakiki aina zote za bidhaa zinazoingizwa na kuzalishwa nchini kama vile bidhaa za kielektroniki zikiwamo simu.

 

Ametaja pia wafanyakazi kutotosheleza katika maabara, hasa maabara za uhandisi ili kukidhi matakwa ya kutoa ripoti za upimaji kwa wakati kwa wateja.

 

Amesema kutokana na huduma ya upimaji ubora wa bidhaa kupatikana Dar es Salaam pekee ikilinganshwa na ukubwa wa nchi, maabara zinashindwa kukidhi mahitaji na kuwafikia wateja wake kwa wakati katika mikoa yote.

 

“Kukosekana kwa sera inayoainisha ubora wa maabara za upimaji pamoja na ufahamu mdogo kwa jamii kuhusu tofauti ya maabara zenye umahiri na zisizokuwa na umahiri, hivyo kuleta ushindani usio sawa katika soko bila kujali gharama ya kuidhinishwa (accreditation cost) na ubora wa taarifa/majibu ya sampuli zake.

 

“Mapato madogo ya ndani yasiyoendana na gharama za manunuzi ya vifaa vya kisasa vya maabara kwa wakati, hivyo maabara kuendelea kutumia baadhi ya vifaa vya kizamani vinavyochukua muda mrefu kutoa majibu.

 

“Kuchelewa kuanza kazi kwa maabara ya huduma za vifungashio (operationalization) uliotokana na ukosefu wa vifaa vya upimaji vinavyokidhi matakwa ya soko.

 

“Ugumu wa upatikanaji wa mafundi wa kufanya matengenezo madogo na makubwa (service & maintenance) ya vifaa vilivyonunuliwa. Hii inatokana na uhaba wa wataalamu hao nchini,” amesema Masikitiko.

 

Amesema kwamba pamoja na changamoto alizozitaja, shirika hilo lina mipango mbalimbali ya baadaye kama ujenzi wa maabara za kisasa zitakazoendana na mahitaji pamoja na hali halisi, pia kuingia mikataba na wataalamu kutoka nje ili kufanya matengenezo madogo na makubwa ya vifaa vya maabara.

 

Masikitiko amesema  shirika linatoa mafunzo kwa wafanyakazi wa maabara ya huduma ya vifungashio pamoja na kununua vifaa vya upimaji wa vifungashio vinavyoendana na matakwa ya soko (retail packaging).

 

Amesema shirika lina mpango wa kupanua wigo wa umahiri katika maabara zilizothibitishwa na kuhakikisha maabara zote zinapata vyeti vya umahiri ifikapo Juni 2016.

Naye Waziri Kigoda amelipongeza shirika hilo kwa ununuzi na ufungaji wa vifaa muhimu vya maabara, ambavyo vinalipa shirika uwezo wa kupima mafuta ya kuendeshea magari, ndege na mitambo mbalimbali kabla ya kuingizwa nchini.

 

“Nimeambiwa aina ya mafuta yapimwayo na TBS ni dizeli, petroli, mafuta ya taa na mafuta mazito. Pia nimeelezwa kuwa mtambo ninaouzindua leo wa CFR, una uwezo wa kupima parameta ya Research Octane Number (RON). Mtambo huu ni maalum na muhimu sana katika upimaji wa mafuta aina ya petroli.

 

“Nimeambiwa pamoja na mambo mengine, mtambo huu hupima uwezo wa mafuta kuzuia kuharibika kwa injini za magari kunakosababishwa na ubovu wa mafuta (knock intensity engine). Pia hupima uharibifu wa injini za magari unaotokana na kuwahi kulipuka kwa mafuta kabla ya muda unaotakiwa,” amesema.

 

Hata hivyo, Waziri Kigoda amewataka TBS na wadhibiti wengine kuhamasisha wenye viwanda na wazalishaji wa bidhaa, kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingizwa na zile zinazozalishwa hapa nchini zinakidhi matakwa ya viwango vya ubora.

 

Amesema TBS ina majukumu mengi kwa mujibu wa Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009. Jukumu mojawapo ambalo ni kubwa ni kuhakikisha kuwa Tanzania inaongoza kwa uingizaji na uzalishaji wa bidhaa zenye ubora.

 

Amsema katika kutekeleza hilo TBS kwa kushirikiana na taasisi nyingine  za hapa nchini pamoja na wananchi wote kwa ujumla inatakiwa kuwa macho kuhakikisha sekta ya viwanda inazalisha  bidhaa bora zinazokidhi viwango na hatimaye kukuza masoko ya ndani na nje.

 

Amsema kwa kufanya hivyo biashara na uzalishaji unaozingatia viwango, utasaidia kuhimili ushindani wa soko huria la ndani na la kimataifa.

 

Amesema Watanzania wengi na wadau kwa sasa wanaonesha imani kubwa kwa TBS kwani kazi zake nzuri zinafanywa kwa uwazi.

 

Amesema ushahidi wa hayo ni matukio mbalimbali ambayo TBS inayafanya katika mchakato mzima wa udhibiti bidhaa zisizokidhi matakwa ya viwango kwa ubora unaostahili na uondoaji bidhaa hafifu katika masoko ya Tanzania.

 

“Vile vile Shirika la Viwango (TBS) lina jukumu la kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa Taifa, kwa kuwaelimisha na kuwashirikisha wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo wadogo (SMEs) katika kuwaelekeza na kuwahamasisha kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango na hatimaye kupata leseni ya ubora ya TBS.

 

“Lengo kuu ni kuhakikisha kuwa bidhaa zinazotengenezwa na viwanda vya Tanzania zinakuwa na ubora na zina uwezo wa kuuzwa kokote ndani na nje ya nchi.

 

“Hivyo basi, ninatoa wito kwa wazalishaji wote wa bidhaa kuhakikisha wanakuja TBS ili kupata leseni ya ubora ambayo itawahakikishia walaji ubora na usalama wa bidhaa wanazonunua na pia itawawezesha kupanua wigo wa masoko yao,” amesema.

 

 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa TBS Profesa Cutbert Muhilu amesema mtambo huo ni mwendelezo wa jitihada za shirika hilo katika kuboresha huduma za upimaji wa ubora wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na zile zinazotoka nje ya nchi.

 

Amesema katika jitihada za kukuza matumizi ya viwango, shirika linatambua umuhimu wa kuboresha huduma za maabara kwa kuwa na vifaa vya kisasa na wataalam waliobobea.

 

“Shirikali natarajia ifikapo mwaka 2015, kuwa kituo kikuu na bora katika masuala ya upimaji na udhibiti ubora wa bidhaa.  Kwa hivyo basi mtambo huu wa kisasa ambao utauzindua leo unaendana na mtazamo na malengo ya Shirika amesema Profesa Muhilu.