• Yapania kutowaonea haya wazalishaji na waingizaji wa bidhaa hafifu
Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1975, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limekuwa likiwahudumia wananchi na umma kwa ujumla katika kuhakikisha kwamba ni bidhaa bora tu ndizo zinazoingia sokoni. Hata hivyo, kwa miaka mingi, utendaji wa shirika hilo umekuwa ukikwamishwa kwa kukosekana nguvu za kisheria za kuwachukulia hatua wale wanaokiuka kanuni na taratibu za ubora. Katika makala haya, MWANDISHI WETU anabainisha jinsi shirika hilo lilivyojizatiti kuitekeleza ipasavyo Sheria mpya ya Viwango ili kuhakikisha kuwa soko la Tanzania linatawaliwa na bidhaa bora…
Unapozungumzia suala la ubora wa bidhaa nchini, unalizungumzia Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Ndilo shirika pekee nchini lenye dhamana ya kuweka viwango vya kitaifa na kudhibiti ubora wa bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazoagizwa nje ya nchi, malengo yakiwa ni kuwezesha biashara, kukuza uchumi wa nchi na kuwalinda walaji na mazingira.
Shirika hili lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge – Sheria ya Viwango Na. 3 ya mwaka 1975, iliyofanyiwa marekebisho na Sheria Na. 1 ya mwaka 1977.
Sheria hiyo ilifutwa na nafasi yake kuchukuliwa na Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009 ambayo ililipa Shirika uwezo mkubwa zaidi wa kutekeleza majukumu yake.
Shirika lina majukumu mengi kama yalivyoainishwa katika Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009, lakini majukumu yake makuu ni kuweka viwango vya kitaifa vya bidhaa, huduma na mifumo ya usimamizi wa ubora katika sekta zote na kutekeleza viwango hivyo katika sekta za viwanda, biashara na huduma, kwa kutumia skimu mbalimbali za udhibiti ubora.
Majukumu mengine ni upimaji wa bidhaa kwa lengo la kuhakikisha ubora wake, ugezi wa zana za kupimia viwandani na kutoa mafunzo kwa wazalishaji na wafanyakazi katika taasisi na viwanda kuhusiana uzalishaji wa bidhaa bora, uzalishaji salama na usimamizi wa ubora.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Joseph Masikitiko, anasema katika kutekeleza majukumu yake ya udhibiti ubora, Shirika linazo skimu mbalimbali za udhibiti ubora.
Anasema kwa bidhaa za ndani, skimu kuu inayotumika ni ile ya alama ya ubora ya TBS, ambapo bidhaa hupimwa na zikithibitishwa kukidhi matakwa ya kiwango husika, mzalishaji hupewa leseni ya kutumia alama ya ubora katika bidhaa husika.
• Bidhaa hupimwa nchi zinakotoka
Kuhusu bidhaa zinazoagizwa nje ya nchi, Masikitiko anasema baadhi ya bidhaa hizo hupimwa nchini baada ya kuingizwa, wakati nyingine hupimwa na kuthibitishwa ubora katika nchi zinakotoka.
Amesema Shirika lake lina mawakala ambao hufanya kazi duniani kote, ili kuhakikisha kwamba bidhaa zinathibitishwa ubora kabla hazijasafirishwa kuja nchini.
“Tunao mawakala makini ambao hufanya kazi duniani kote, lengo likiwa ni kuhakikisha kwamba hakuna bidhaa ambazo hazijathibitiswa ubora wake zinazoingizwa nchini,” amesema na kuongeza kuwa mawakala hao wanafanya kazi chini ya mpango ujulikanao kama Pre-shipment Verification of Conformity to Standards (PVoC).
Anabainisha pia kuwa Shirika huendelea kufanya ukaguzi katika masoko na kuchukua sampuli ili kujihakikishia kuwa kweli bidhaa hizo zina ubora unaotakiwa.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu huyo amesema TBS ilianzishwa kwa madhumuni ya kuwezesha biashara na kuhakikisha kwamba Watanzania wanashiriki katika kukuza uchumi kwa kuzalisha bidhaa zinazokidhi matakwa ya ubora.
Amesema bidhaa zinazokidhi matakwa ya viwango huweza kushindana vizuri kwenye soko, na wakati huo huo kumhakikishia mlaji usalama na pia hutunza mazingira.
Anafafanua kuwa ili kuhakikisha yote hayo yanafanyika, sheria na kanuni mbalimbali zimetungwa, lengo likiwa ni kuwabana wazalishaji au wafanyabiashara wasio waaminifu.
Masikitiko amesema TBS imekuwa na mikakati mbalimbali ya kuwabana wafanyabiashara wasio waaminifu, na miongoni mwa mikakati hiyo ni kwa kutumia Sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009, ambayo anasema ina meno ya kuwabana wazalishaji na wafanyabiashara wanaovunja sheria kwa makusudi kwa lengo la kupata faida kubwa, ikilinganishwa na sheria iliyotangulia.
*Viwanda vyafungwa
“Kwa sasa hatuna utani na wavunja sheria, bali tunawachukulia hatua mbalimbali kwa kuzingatia Sheria ya Viwango,” amesema Masikitiko na kuongeza kuwa hii si nguvu ya soda kwani Shirika limedhamiria kuwabana wavunja sheria ili kuhakikisha kuwa linapunguza kwa kiasi kikubwa tatizo la bidhaa hafifu sokoni.
Akitoa mfano wa baadhi ya viwanda vya nondo vilivyosimamishwa kuzalisha bidhaa hiyo kwa muda hivi karibuni na kisha kuruhusiwa kuendelea na uzalishaji baada ya kutimiza matakwa ya ubora, Kaimu Mkurugenzi Mkuu amesema Shirika lake limejizatiti kuwabana wazalishaji wazembe na kwamba ukaguzi utafanyika kwa bidhaa zote.
Viwanda vingine vilivyofungiwa ni Kiwanda cha Maji ya Mawenzi (Great Zone Investment, Dar es Salaam). Wanatumia leseni ya ubora ya TBS wakati walishanyang’anywa na kuamriwa kufunga kiwanda. Kiwanda cha Maji ya Al hayaa (Al hayaa Limited, Tanga), Duka la Chakula cha Mifugo Ng’ombe Mix (Keen Feeders, Arusha) na Kiwanda cha Mikate (Tanga Modern Bakery Limited, Tanga).
“Ukaguzi na ufungaji wa viwanda au maduka haufanyiki kwenye nondo tu, bali utakuwa unafanyika kwa bidhaa zote. Tutahakikisha kwamba tunafanya ukaguzi wa kushitukiza katika kila miezi miwili na si kama utaratibu uliokuwa ukitumika siku za nyuma wa mara nne kwa mwaka,” amesema Masikitiko, akirejea ukaguzi ambao hufanyiwa wazalishaji waliopewa leseni za kutumia alama ya TBS.
“Tutafanya hivyo mpaka hapo tutakapojiridhisha kwa sasa uzalishaji unafuata matakwa ya ubora wakati wote.
Amesema hivi karibuni TBS ilitoa mwezi mmoja kwa wazalishaji wasio na alama ya ubora ya TBS kuhakikisha kwamba wanaanza mchakato wa bidhaa zao kuthibitishwa ubora kisha kuipata alama hiyo ya ubora.
Anabainisha kuwa baada ya muda huo kwisha, TBS itafanya ukaguzi na wale wote watakaobainika kukiuka. Hatua kali zitachukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Ametoa wito kwa wananchi wote kusaidia katika mapambano dhidi ya bidhaa hafifu kwa kutonunua bidhaa zisizothibitishwa na pia anawaomba wananchi kutoa taarifa kwa TBS wanapoona bidhaa inazalishwa au kuuzwa bila kuwa na nembo ya ubora kwa kupiga simu ya bure ya Shirika ambayo ni 0800 110 827. Namba hii hupatikana kwa kutumia mitandao ya Vodacom, TTCL na Sasatel.
Ili kuhakikisha kwamba bidhaa hafifu hazipenyezwi nchini, TBS imekuwa na mazungumzo na wenzao Shirika la Viwango la Zanzibar, ambapo amesema mazungumzo yao yanalenga kuhakikisha kwamba bidhaa hafifu haziingii Zanzibar na kisha Tanzania Bara, na kwamba maeneo ya ushirikiano yameainishwa na kuyataja kuwa ni uandaaji wa viwango, upimaji na ugezi na udhibiti ubora.
“Udhibiti wa bidhaa Zanzibar ni muhimu sana kwa sababu Zanzibar ni sehemu ya nchi yetu, hivyo wao wasipokuwa imara huku tutayumba pia,” amesema Masikitiko na kutoa wito kwa wazalishaji na waagizaji wa bidhaa kufuata sheria na kuacha mazoea kwa kuwa sasa TBS iko makini kusimamia sheria za nchi.
• Wadau wengi wahusishwa kudhibiti ubora
Lakini pia ili kuhakikisha kwamba wananchi hawatumii bidhaa hafifu, TBS inafanya mazungumzo na halmashauri za miji kuhakikisha kwamba sheria ndogondogo zinatungwa ili kudhibiti matumizi ya bidhaa zisizo na ubora.
Masikitiko amesema kwamba kwa kuwa nchi yetu ni kubwa, ushirikiano wa wadau mbalimbali kama vile halmashauri za miji ni muhimu katika kuhakikisha kwamba viwanda vyote ambavyo vipo katika halmashauri zao vinasajiliwa na kupata nembo ya ubora, na kuhakikisha kuwa bidhaa zinazoingizwa nchini kupitia maeneo yao zinadhibitiwa.
Ushirikishwaji wa wadau wengine kama Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI) na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) ni muhimu pia, na hapa Masikitiko anasema: “CTI wanapaswa kuwahimiza wanachama wao kuzalisha bidhaa zenye ubora wakati TIC wanapaswa kuwa na sheria inayowabana wawekezaji wazalishe bidhaa zenye ubora unaokubalika katika nchi yetu.”
Hata hivyo, anasema,“Sheria mpya imelipa Shirika mamlaka ya kuwabana wale wote wanaokiuka taratibu kuhusiana na masuala ya ubora.”
Miongoni mwa wale wanaobanwa na sheria hiyo ni wanaotumia vibaya alama ya ubora ya TBS, mathalani kwa kuiweka katika bidhaa isiyo na ubora. Wengine ambao sheria hiyo itawabana ni wanaoagiza bidhaa hafifu na ambao hawazingatii kanuni na taratibu za udhibiti ubora.
Anabainisha kuwa kabla ya sheria ya sasa, sheria iliyotangulia ilikuwa dhaifu kiasi cha kutoweza kuwabana watu wa namna hiyo, na hivyo wafanyabiashara wasio waaminifu waliutumia udhaifu huo kwa maslahi yao.
“Kabla ya sheria hii mpya kupitishwa, wafanyabiashara wasio waaminifu walikuwa wanatozwa faini ya Sh 1,500 (shilingi elfu moja mia tano), sasa hebu ifikirie faini hiyo kwa kiwango cha maisha ya sasa, nadhani ndiyo maana sheria na kanuni zetu zilikuwa zinakiukwa sana,” anasema.
Anamalizia kwa kubainisha kuwa sheria mpya inatoa adhabu ya kwenda jela miaka miwili au kulipa faini ya kati ya Sh milioni 50 na Sh milioni 100 kwa mtu anayekutwa na hatia katika makosa ya ukiukwaji wa kanuni na taratibu za ubora wa bidhaa.