Kwa muda wa wiki sita tumekuwa tukikuletea mwedelezo wa taarifa jinsi kampuni ya SABmiller inayomiliki Kampuni ya Bia ya Tanzania (TBL) inavyotumia udhaifu wa kisheria kutolipa kodi sahihi. Ifuatayo ni taarifa ya utafiti uliofanywa na Kampuni ya Uingereza iitwayo ActionAid na kubaini mchezo inaofanya SABmillar wa kutolipa kodi kwa kutumia udhaifu wa kisheria. Kampuni ya SABmiller kuwa ina uzoefu mkubwa wa kutumia udhaifu wa sharia hadi nchini Uingereza kutolipa kodi stahiki. Endelea…
Njia mbadala kwa bei linganishi
Sheria zenye nguvu na kuwajengea uwezo maofisa wa kodi wa Mamlaka ya Mapato Ghana (GRA) na kuziba mianya ya ulipaji wa bei ya chini kwa bidhaa wanazouza nje ya nchi kupitia kampuni dada, linaweza kuwa suluhisho la kudhibiti ukwepaji kodi kwa nchi zinazoendelea, unasema utafiti wa ActionAid.
Pia kuna kila sababu ya kutilia shaka mfumo wa tafsiri ya bei linganishi inayozaa upotevu wa mamilioni ya pauni, si katika nchi maskini tu, bali hata nchi zilizoendelea. Mwongozo wa bei linaganishi katika biashara ya kimataifa kwa nchi zinazoendelea ulioandaliwa na Kamati ya Kodi ya Umoja wa Mataifa unafafanua mfumo wa bei linganishi kwa kina.
“Kanuni zinazotokana na bei linganishi zinaendelea kuwa ngumu kuzisimamia. Utii katika bei linganishi kwa kampuni za kimataifa kwa sasa unahusisha uanzishawaji wa kanzidata ambazo ni gharama kubwa na zenye zinahitaji utaalamu wa hali ya juu.
“Ukaguzi wa bei linganishi unapaswa kufanywa kwa mauziano ya bidhaa moja hadi nyingine, na mara nyingi ni ngumu kwani inahusisha gharama kubwa kwa wanaohusika… Mamlaka za kodi za nchi nyingi zinazoendelea hazina rasilimali za kutosha kuchunguza taarifa na mazingira ya kila mauziano yanayofanyika kuweza kubaini kiwango kinachokubalika cha bei linganishi, hasa katika mazingira ambayo hakuna kampuni ya kulinganisha nayo mauzo wanayojiuzia,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.
Kwa mfano, Kampuni ya Bia Tannzania (TBL Group) isingekuwa na mshindani nchini Kenya ambayo ni Kampuni ya Kapari Limited, gazeti hili la JAMHURI lisingeweza kubaini kuwa TBL inajiuzia Konyagi na Bia kwa bei ya chini kupitia Kampuni dada iliyoko nchini Kenya ya Crown Baverage.
Waziri wa zamani wa Fedha wa Afrika Kusini, Trevor Manuel amekuwa mkosoaji mkubwa wa kampuni za kimataifa zinazoepuka kodi. Aliwaambia maafisa wa kodi barani Afrika kwamba nchi ndogo na maskini zenye mamlaka za kusimamia kodi zisizo na uwezo wa kutosha, hatuwezi kuzitegemea kujenga utaalamu unaotakiwa kubaini mfumo mgumu wa kampuni za kimataifa na kampuni nyingien kubwa zinazofanya kila mbinu kupunguza kiwango cha kodi zinacholipa.
Michael Durst, Mkurugenzi wa zamani wa Idara ya Huduma ya Kodi za ndani ya Wamarekani inayofuatilia mkataba wa bei linganishi za kimataifa anasema kwa kuendelea kung’ang’ania ajenda ya bei linganishi ni sawa na maafisa kodi kujipiga risasi.
Moja ya sababu alizozitoa ni upotoshaji katika mifumo yanapofanyika mauziano ya bidhaa zisizoshikika kama nembo za bidhaa (trade mark). Bei linganishi inapaswa kuchukuliwa na kila shirika hata hayo yenye nia ya kuepuka kodi kwa kuangalia bei zinazotozwa bila kuangalia mfumo wenyewe.
“Kampuni za kimataifa kwa ujumla zimekuwa huru katika kuingia kwenye mikataba na kuhamisha kwenda katika nchi ambazo ni pepo ya kodi, “ anasema Durst.
“Ni vigumu kuelewa dhana ya tozo ya usimamizi (Management fee),” alisema Kamishna Mkuu wa Kodi wa Ghana. Kwani ni vigumu kupima viwango vilivyopelekwa, achilia mbali bei. “Ni mbaya zaidi kwa suala la nembo za biashara. Nembo ya biashara ni bidhaa ya kufikirika, makadirio ya thamani wanayoipa watumiaji kwa bidhaa iliyopo hayaelezeki. Unatunzaje thamani ya vitabu vyako, ni suala lisiloelezeka.”
Dhana ya bei linganishi si mchezo pekee unaofanywa na kampuni kubwa. Brazil kwa mfano inatumia mfumo wa OECD kwa kupanga viwango vya bei katika kanuni ya bei linganishi ambayo bado inatoa fursa ya kuchezea bei.
Wanapeleka maombi ya bei wanazouziana kati ya kampuni zilizoko Brazil na zile zilizo na uhusiano nazo nje ya nchi. Na mauziano yote ya kampuni zilizoko kwenye nchi ambazo ni pepo ya kodi. Mfumo huu wa Brazil una changamoto, lakini unaweka viwango na njia rahisi ya kutekeleza kanuni ya bei linganishi kwa nchi zinazoendelea.
Baadhi ya watu wamejenga hoja ya kuachana na suala la bei linganishi duniani wakitaka bei za jumla ndizo zitumike kutoza kodi bidhaa zote zinazouzwa nje ya nchi, mfumo ambao kwa kampuni za kimataifa faida yake yote ingetozwa kodi katika nchi inakofanya biashara kwa mujibu wa kanuni. Nchini Marekani kampuni zimeanza kutumia mfumo wa kugawa faida katika majimbo unaofahamika kama ‘three factor state formula’ inayojumuisha hisa za kampuni na mali zote, malipo kwa afanyakazi na mauzo katika kila jimbo.
Viwango vinavyopendekezwa na jumuiya ya Ulaya katika kodi za kampuni zinaelekea zitachukua mkondo huo. Pia imependekezwa kwamba kwa vyovyote iwavyo, mfumo wa kikanuni ungeweza kutumika katika kupiga hesabu za kodi linganishi.
Malipo
Sampuli ya nchi kadhaa iliyofanywa na kampuni ya ActionAid inaonyesha kwamba upangaji kodi ni dhana ya msingi kwa biashara ya SABmiller kwa bara la Afrika lote na India.
ActionAid imefanya makisio ya uhakika juu ya kiwango cha kodi zinazopoteza serikali. Kuna aina mbili za kodi zinazokwepwa walizobaini, ambazo ni malipo ya mrahaba na kodi ya uendeshaji.
Katika miaka minne ya fedha kuanzia 2007 hadi 2010 Kiwanda cha Bia cha Ghana peke yake kililipa pauni milioni 4.57 (karibu Sh bilioni 15 kama kodi ya uendeshaji na mrahaba-ikiwa ni asilimia 6.7 ya mauzo yote ya kampuni. Kiwango hiki ni mara 10 ya faida ghafi na kiasi hiki kimelipwa kwa kampuni tanzu mbili za Bevman Services AG nchini Uswisi na SABmiller International BV.
Kwa mujibu wa taarifa za hesabu za miaka ya karibuni zilizopo wanakadiria kuwa Afrika yote na India malipo ziliyofanya kwa kampuni hizi mbili za SABmiller zinazodaiwa kutoa huduma ya uendeshaji yanakadiriwa kufikia pauni milioni 90 (Karibu Sh bilioni 300).
Kiasi hiki kingeweza kununua chupa aina ya Grolsch zinazowezwa kutandazwa kutoka Mashariki hadi Magharibi mwa Afrika na Kusini hadi Kaskazini.
Kampuni za SABmiller zilizopo barani Afrika zimelipa dola milioni 16 sawa na asilimia 15 ya faida ghafi pia. Inakadiriwa kuwa mirahaba iliyolipwa kwa kampuni za SAMmiller zilizopo Uholanzi, imezipotezea Serikali za nchi za Afrika kodi ipatayo pauni milioni 10 (karibu Sh bilioni 30) na kwamba kodi za uendeshaji ambazo mara nyingi hulipwa nchi Uswisi zimepunguza mapato ya kodi kwa Afrika na India kwa wastani wa pauni milioni 9.5 (karibu Sh bilioni 29). Ukijumlisha malipo yaliyofanywa kwa Kampuni zilizo Mauritius makisio ya jumka ambayo serikali za Afrika zilipoteza yanafikia pauni milioni 20 (karibu Sh bilioni 60). Inakisiwa kwamba biashara za SABmiller barani Afrika ukiondoa Afrika Kusini ina viwango vya kodi inayofanana, hivyo takwimu za kodi iliyopotea inaweza ikafikia 1/5 ya makisio ya kodi yote linayopaswa kukusanya Bara la Afrika kwa mwaka.
Kiwango kinachopotea Afrika kinatosha kupeleka watoto 1,000,000 shuleni katika nchi ambazo SABmiller inafanya biashara zake. ActionAid imebaini mbinu zinazotumiwa na SABmiller kuhakikisha kwamba kodi inayopelekwa katika nchi za pepo ya kodi hukusanywa na kupelekwa Uingereza kwa ajili ya kuzilipa gawio kampuni zenye hisa kwa SABmiller kupitia mbinu ambayo inakwepa sheria za kodi za Uingereza pia.
Mfano mzuri umebainika katika akaunti ya SABmiller ya Uholanzi iitwayo SABmiller Finance BV. Kampuni hii ilihamisha nembo za biashara kwenda SABmiller International BV mwaka 2005 ikiweka mazingira ya kulipa mirahaba isiyotozwa kodi.
Kampuni ya SABmiller Finance BV ilipata hadhi ya kuwa mkaazi wa Uingereza kikodi (baada ya kusajiliwa Uingereza) hivyo kuiwezesha kulipa faida iliyolimbikizwa ya pauni bilioni mbili kama gawiwo kwa kampuni mama ya SABmiller Holdings Limited PLC mwaka 2009 bila kulipa kodi.
Kwa nchini Uingereza sheria inatoa fursa kwa kampuni inayotoa gawio kiasi inacholipa kutolipiwa kodi, hivyo SABmiller imekuwa ikitumia fursa hii kuhamisha faida kutoka sehemu mbalimbali duniani kwenda Uingereza, kisha inazihamishia kwenye kampuni mama kama gawio na hivyo kukwepa wajibu wa kulipa kodi.
Hii inavyoonyesha SABmiller kwa gawio la pauni bilioni 2 kutoka Kampuni ya SABmiller Finance International BV kwenda SABmiller Holding Limited PLC, haikulipa kodi yoyote kwa Uingereza kwani gawio kutoka kampuni ya Uingereza halitozwi kodi kwenda kwa kampuni nyingine ya Uingereza.
Je unajua wataalamu walivyopendekeza mbinu mbadala kodi ziweze kulipwa kwa ukamilifu? Usikose toleo lijalo la JAMHURI.