Kwanza niipongeze Wizara ya Maliasili na Utalii na hasa Idara ya Wanyamapori, kwa kuanzisha Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania inayojulikana kwa Kiingereza kama Tanzania Wildlife Management Authority (TAWA).

 Kuna sababu kadhaa za kuipongeza Wizara na Idara kwa kuanzisha TAWA, lakini kuu, nionavyo mimi, ni mbili; kwanza ni ugumu uliokuwapo katika mchakato hadi kufikia hatua iliyofikiwa, na pili ni umuhimu wa kuwa na chombo hicho.  Nitafafanua kidogo kuhusu sababu hizi kwa manufaa ya hatua za baadaye katika kukamilisha chombo hiki kiutendaji. Kuanzishwa kwa mamlaka ya kitaifa ya usimamizi wa wanyamapori haikuwa rahisi hata kidogo. Jitihada za kuanzisha chombo hicho zilianza kwenye miaka ya 1980. Kuna mambo kadhaa yaliyokwaza mchakato huo na wakati mwingine kusita kwa muda kabla ya kuanza tena.

Mambo haya ni pamoja na kubadilishabadilisha viongozi muhimu, hasa kwenye nafasi ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Mkurugenzi wa Wanyamapori.

Yamkini mabadiliko ya mara kwa mara kwa nafasi ya Mkurugenzi wa Wanyamapori na kukaimiwa kwa muda mrefu, yakawa ndiyo yaliyoathiri mwenendo wa mchakato wa kuanzisha TAWA kuliko jambo lolote lile.

Jambo jingine lililoleta ugumu katika mchakato na kuchelewesha uamuzi ni kile kilichoonekana kuwa mgongano wa kimaslahi.

Hili lilijitokeza zaidi ilipokuwa imependekezwa TAWA kusimamia masuala yote ya uhifadhi nchini na mbuga zote za kuhifadhi wanyama, ikiwa ni pamoja na hifadhi zilizokuwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa (TANAPA) na Hifadhi ya Ngorongoro.

TAWA kwa jinsi ilivyoanzishwa sasa haisimamii hifadhi zilizo chini ya TANAPA wala Hifadhi ya Ngorongoro. Naipongeza Wizara kwa kuweza kufikia uamuzi huo, hasa kwa vile kufanya vinginevyo ingeathiri tija kitaasisi, na ufanisi wa uhifadhi kitaifa. 

Jambo la pili kuu linalofanya Wizara ya Maliasili na Utalii na Idara ya Wanyamapori kustahili pongezi ni umuhimu wa chombo hicho katika juhudi za Serikali kuhifadhi wanyamapori.

Umuhimu wa kwanza wa kuwa na TAWA ni kuwa na chombo huru chenye mamlaka kisheria kusimamia uhifadhi na matumizi ya wanyamapori.

Kutokana na kuwa na mamlaka haya kisheria, TAWA inaweza kufanya uamuzi wowote kwa wakati, jambo ambalo litapunguza urasimu na kuziba mianya ya rushwa, ziwe za kweli, au kufikirika. Hili ni jambo litakaloongeza tija katika shughuli zote za uhifadhi na matumizi ya wanyamapori.

Kadhalika, imani yangu kwamba kwa kuwa na mamlaka kamili kisheria, na inayoongozwa na bodi, TAWA itaweza kuwa na rasilimali za kuiwezesha kushinda pale Idara ya Wanyamapori inapoonekana kuelemewa ama kushindwa, kama vile kupambana na ujangili.

Kwa kutimiza majukumu yake kwa ufanisi, si tu kutaiwezesha TAWA kuhifadhi wanyamapori kwa mafanikio zaidi, bali pia kutaongeza pato la Taifa  kutokana na matumizi bora ya wanyamapori, ikiwa ni pamoja na  utalii na uwindaji. Hata hivyo, TAWA haiwezi kupata mafanikio hayo niliyoyataja hapo juu kwa vile tu ni mamlaka huru iliyowekwa kisheria. Kuna mambo ambayo yanatakiwa kuwapo ili chombo hicho kiweze kupata mafanikio yanayolengwa.

Kama ilivyo kwenye jina lake, TAWA inatakiwa kuwa chombo cha usimamizi zaidi kuliko vinginevyo. Usimamizi hapa ina maana ya kutenda shughuli za kustawisha wanyamapori, na siyo kuwalinda tu.

Kwa bahati mbaya, ukiangalia kilichoainishwa kwenye rasimu ya sheria kwa sifa kuu ya wafanyakazi wa Mamlaka, utaona kuwa sheria inalenga zaidi ulinzi wa kijeshi kuliko usimamizi (management) wa wanyamapori. Usimamizi umetajwa tu kwenye sifa za Mkurugenzi Mkuu!

Aidha, inaelekea katika kuunda Bodi ya Wakurugenzi inayosimamia Mamlaka, kilichozingatiwa zaidi ni uwakilishi wa wadau kitaasisi, na si taaluma ya usimamizi wa ustawi wa wanyamapori na mazingira yake. 

Taaluma ya usimamizi wa ustawi wa wanyamapori na mazingira yake kutopewa kipaumbele stahili katika sheria ya Mamlaka na chombo kinachoisimamia, in dosari kubwa sana katika jitihada za kuongeza juhudi, maarifa na tija katika uhifadhi wa wanyama nchini.

Na hasa sheria hii inapokuwa imetungwa katika zama ambazo ulimwengu mzima unafanya jitihada za makusudi kuondokana na matumizi ya bunduki na kujikita zaidi katika usimamizi na ulinzi shirikishi, kwa maana ya kushirikisha wananchi na taasisi husika. 

Ni jambo ambalo kwa sasa linaeleweka katika medani za uhifadhi kuwa ili uhifadhi wa maliasili yoyote uwe endelevu na ulete maendeleo endelevu, hakuna budi kushirikisha na kuwa rafiki kwa wananchi husika. Hivyo, kuegemea zaidi mtutu wa bunduki inakuwa kurudi nyuma.

Hapa kwetu Tanzania, mbali na uhitaji wa kushirikisha wananchi katika uhifadhi wa wanyamapori, ipo haja ya kuzama zaidi kwenye masuala ya kustawisha wanyamapori kutokana na athari za tabia nchi, matumizi mabaya ya ardhi, na ongezeko la mahitaji ya ardhi kwa shughuli nyinginezo za maendeleo. Hii itakuwa mada ya siku nyingine. 

Mbali ya kasoro hizo zinazoonekana ndani ya rasimu ya TAWA, kuna kasoro za kimchakato ambazo ni muhimu zikaangaliwa mapema iwezekanavyo, ama sivyo Mamlaka inaweza kushindwa kutekeleza majukumu yake kwa muda mrefu kutokana na kukosa uhalali, ama kukosa kanuni na miongozo muhimu katika mfumo wa utendaji.

Mwandishi wa makala hii ni Mshauri Mwelekezi wa Maliasili, Mazingira na Maendeleo Endelevu. Anapatikana kwa namba ya simu: 0784-463723 na kadhalika barua pepe: [email protected] au [email protected]