Kupokelewa kwa Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kama mwanachama wa Chadema na kuteuliwa kwake kuwa mgombea urais wake ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kunapaswa kuwaacha hoi Watanzania wengi.
Hoi kwa maana ya kushuhudia namna ambavyo chama cha siasa kilichojipambanua kuwa mstari wa mbele kupinga watu na mifumo inayokiuka misingi ya utawala bora kumtanguliza mbele kiongozi ambaye, kwa kauli mbalimbali za viongozi wa CHADEMA, alikuwa hafanani na misingi hiyo. Tungawaelewa CHADEMA iwapo Lowassa angepokelewa kama mwanachama wa kawaida; tatizo ni kwao kuamua kuwa anafaa kuwa rais wa Tanzania.
Tunakumbuka harakati nyingi za kisiasa zilizoongozwa na Chadema katika miaka ya hivi karibuni dhidi ya ufisadi na hata kauli za baadhi ya viongozi wao dhidi ya watuhumiwa wa ufisadi, akiwemo Edward Lowassa. Katibu Mkuu wao, Dk. Willibrod Slaa, katika mkutano uliofanyika uwanja wa Mwembe Yanga Dar es Salaam Septemba 2008 alimtaja Lowassa kuwepo kwenye orodha ya kundi la mafisadi. Alivuka hatua moja zaidi kwa kusema kuwa alikuwa ni kati ya watu 11 waliofilisi Tanzania na hawajafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake, mwenyekiti wa CHADEMA Freeman Mbowe amewahi kutamka kuwa Lowassa ni kiongozi dhaifu asiyekuwa na uwezo wa kukemea.
Mwaka 2008 John Mnyika, katika wadhifa wake kama Mkurugenzi wa Vijana wa CHADEMA, alisema mengi zaidi. Aliishutumu serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa kumlinda Lowassa akihoji kwanini Lowassa hakujumuishwa kuchunguzwa kama ambavyo ilipendekezwa kwa mawaziri Nazir Karamagi na Ibrahim Msabaha na kamati teule ya bunge iliyochunguza kashfa ya Richmond. Kwa maelezo ya Mnyika, Lowassa alikuwa ni mmoja wa mizizi ya ufisadi wa Richmond na serikali ilipaswa kumkamata, kumhoji, na kumchukulia hatua za kisheria.
Leo hii Chadema wanasemaje? Kwanza wanatuambia kuwa yule yule ambaye miaka nenda rudi walituambia anapaswa kukamatwa, kuhojiwa, na kufikishwa mahakamani sasa ameibuka na sifa ya kuwa kiongozi mmoja wa viongozi wao mwandamizi. Na siyo wao kwao tu, lakini wameamua kuwa anafaa kuwa rais wa Tanzania.
Hebu tuchukulie vigezo vya kisheria ambavyo CHADEMA sasa wanavitumia kuhalalisha kwao kumpendekeza Lowassa kuwa mgombea urais wao. Tundu Lissu amenukuu vipengele vya katiba ambavyo, kisheria, havimzuwii Lowassa kuwa mgombea wa urais. Hiyo ni mbinu ya kukwepa hoja. Hoja ya msingi haimhusu Lowassa; inahusu chama ambacho kiko tayari, kwa sababu ambazo kinapasa kuzieleza kwa ukamilifu, kuwa siku moja ni jeshi la makamanda vinara wanaokemea watuhumiwa wa ufisadi na siku inayofuata kutuambia kuwa mmoja wa watuhumiwa hao sasa anafaa kuwa rais.
Mimi ningekuwa mwanachama wa Chadema ningetaka kuwa na uhakika kuwa nikilala leo, nitaamka asubuhi nikiwa mwanachama wa chama kile kile ambacho jana kilihubiri kuwa watuhumiwa wa ufisadi wanapaswa kupelekwa sehemu moja tu: mahakamani. Sitaki kukosa usingizi nikiwa na hofu kuwa nikiamka asubuhi nitakuta Chadema siyo ile niliyokuwa naifahamu jana.
Ushabiki wa kisiasa uko wa aina tofauti, lakini naamini kuwa ushabiki wa kisasa unaoleta manufaa kwa jamii ni ule wa wanachama ndani ya chama cha siasa ambao wanaunga mkono chama cha siasa kutokana na sera zake, kampeni zake, taasisi zake, kanuni zake, misimamo ya kisiasa, na mitazamo ya kisera kiujumla.
Chadema kinajidhirihisha sasa kama chama cha siasa ambacho kinaweza kubadilika kama kinyonga, kutegemea na hali ya siasa inayojitokeza. Ni chama ambacho kipo tayari kuweka pembeni baadhi ya misimamo yake kwa kusudio la kutimiza lengo la muda mfupi la kisiasa bila kujali kama linabadilisha sifa na hadhi iliyojengeka awali. Hii siyo Chadema tunayoifahamu. Au tuseme kuwa labda ni Chadema ile ile iliyokuwepo siku zote ila ni sura ya Chadema ambayo tulikuwa hatujaibaini.
Wawakilishi wa vyama vinavyounda Ukawa waliposusia bunge la katiba walikishutumu CCM kwa kubadilisha kwa kiasi kikubwa vipengele vya rasimu ya katiba vilivyowasilishwa na tume ya Jaji Warioba. Mojawapo ya mambo muhimu yaliyomo kwenye rasimu ya katiba ya tume ya Jaji Warioba ni vifungu vinavyohusu maadili na miiko ya viongozi wa umma.
Katika Pendekezwa, chini ya bunge la katiba liliobaki na wajumbe wanaounga mkono CCM, iliviondoa na kubakia na vipengele vilivyrahisisha kiongozi yoyote asiye muadilifu kuendelea kushika nafasi ya uongozi wa umma bila kuhofu kikuika katiba. Swali la kujiuliza baada ya kushuhudia Chadema hii ya leo iliyokuwa na misimamo gongana ni iwapo tutaweza kuamini kuwa ile katiba ya awali itarudi vile vile kama walivyoahidi endapo mgombea wa UKAWA atashinda uchaguzi wa rais. Ni suala linapaswa kuulizwa kwa sababu kuibuka kwa ufisadi ni matokeo ya ukiukwaji wa maadili na miiko ya viongozi wa umma.
Kigezo cha mwisho cha kupima uamuzi huo wa Chadema yanabaki kwa wanachama wake, siyo kwenye matokeo ya uchaguzi mkuu kama wengi wanavyodai. Kushinda uchaguzi mkuu hakutafuta ukweli kuwa Chadema imejitumbukiza kwenye mkanganyiko wa kisiasa ambao ni mgumu kuutetea. Lakini iwapo wanachama wa Chadema wanaridhika na uongozi wa chama chao, uamuzi ambao hauleti uhakika wowote wa msimamo wa kesho, basi haina haja ya mtu yoyote ambaye siyo mwanachama wa Chadema kulalamika.
Sisi wengine ambao siyo wanachama wa Chadema (wala CCM, wala ACT, n.k.) tunahoji mfumo unaoitwa wa demokraisa ya vyama vingi ambapo tuliamini kuwa unaweza kutoka CCM ukahamia chama kingine na ukakuta msimamo unaodumu kwa muda fulani, na pale unapobadilika basi unategemea kupata maelezo ya kuridhisha ya muelekeo mpya. Lakini, la msingi zaidi, ni ile fursa ya kuweza kuunga mkono chama kingine cha siasa ukiamini kitaweza kuleta mabadiliko ambayo hukuyapata kule ulikotoka.
Kwa hali hii iliyopo naanza kuamini kauli za wale wanaosema kuwa wanasiasa wengi wa sasa wanatofautiana kwa rangi za vyama vyao tu.