Na Marco Maduhu, JammhuriMedia, Shinyanga
WANAWAKE 16 ambao wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la Ugonjwa wa Fistula mkoani Shinyanga,wamefanyiwa upasuaji wa tatizo hilo, huku wengine Nane wakitarajiwa kufanyiwa leo na kufika 24.
Zoezi hilo la upasuaji limefanyika bure katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga kupitia Kambi ya Madaktari Bingwa wa Magonjwa ya wanawake kutoka Hospital ya Rufaa Bungando Jijini Mwanza, Matibabu yaliyofadhiliwa na Shirika la Americares.
Mwakilishi kutoka Shirika hilo la Americares Dk. Jonas Kagwisage, amesema wana miaka 13 sasa wamekuwa wakitoa huduma hiyo ya Matibabu bure ya Fistula kwa wanawake kwa kushirikiana na Madaktari Bingwa wa wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa ya Bugando, na sasa wamefanya kambi mkoani Shinyanga kutoa huduma hiyo.
Amesema katika Mkoa wa Shinyanga wameanza Kambi hiyo tangu Juni 23 na itahitimishwa kesho Juni 29, na kwamba hadi sasa wameshawafanyia Upasuaji wa Ugonjwa huo wa Fistula wanawake 16 na wengine nane watawafanyia kufikisha idadi ya wanawake 24.
“Huduma hii ya Matibabu ya Ugonjwa wa Fistula inatolewa bure, na Shirika letu la Americares ndiyo tuna gharamia kila kitu hadi chakula na nauli pia za kuwaleta hapa Hospitali na tutawarudisha kwao,”amesema Dk.Kagwisage.
Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya Rufaa Bugando Jijini Mwanza Dk. Elieza Chibwe, amesema tatizo la ugonjwa wa Fistula bado ni kubwa sana kwa wanawake na husabishwa na uchungu pingamizi kwa mwanamke anapokuwa mjamzito, na hutokea Tundu ambalo linaunganisha njia ya uzazi na sehemu ya haja kubwa na ndogo na Mwanamke hutokwa na kinyesi na haja ndogo muda wote.
“Ugonjwa wa Fistula ni ugonjwa wa aibu na matibabu ya Fistula ni upasuaji tu, na tunataka hadi kufikia 2030 tatizo la Fistula liwelimekwisha kabisa,”amesema Dk.Chibwe.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Shinyanga Dk. Luzila John, ameshukuru kwa utolewaji wa Tiba ya Fistula Hospitalini hapo, huduma ambayo pia imewajengea uwezo Madaktari wao wa Magonjwa wa wanawake, na watakuwa wakitoa huduma hiyo na siyo tena kuwapa wagonjwa Rufaa ya kwenda Bugando.
Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Zamda Shabani, amelishukuru Shirika la Americares kwa kufadhili wa Tiba hiyo, pamoja na Madaktari kutoka Bugando na kutoa wito kwa wanawake wajitokeze kwa wingi kupata huduma hiyo,ili waondokane na tatizo hilo11 na kufanya shughuli zao kwa uhuru.
Diwani wa Mwawaza Juma Nkwabi, ameiomba Serikali ipeleke pia Madaktari Bingwa wa kutoa huduma ya Fistula katika Hospitali hiyo ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, na kutotegemea Madaktari wa Bugando.
Naye Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto Mkoa wa Shinyanga Halima Hamis, ambaye ndiye aliyeratibu zoezi hilo la Madaktari Bingwa, ametoa wito kwa wanawake wa Mkoa huo wapende kujifungua kwenye huduma za Afya sehemu ambayo ni salama sababu tatizo la Fistula huwakumba Wajawazito ambao hujifungulia Majumbani.
Mmoja wa wanawake ambaye amefanyiwa upasuaji Terezia Mayunga kutoka wilayani Kahama, amesema ameishi na tatizo la Fistula kwa miaka 38, lakini sasa amepatiwa Tiba na hali yake ni nzuri, huku mwingine akibainisha kwamba baada ya kupatwa na tatizo hilo mumewake alimkimbia na sasa amepona na kushukuru Shirika la Americares na Madaktari kwa kumpatia tiba bure.