Ujio wa Katiba mpya unasubiriwa kwa shauku kubwa na wananchi ambao naweza kusema wanapenda kumaliza matatizo kwa njia za kujipa matumaini.

Matarajio ya wananchi (hasa walioaminishwa uzuri wa hii Katiba tarajiwa) ni makubwa mno. Wanaota mambo makubwa na mazuri yatakayoletwa na Katiba mpya.

Wanasiasa wanaounga mkono Katiba inayopendekezwa wanazidi ‘kuwatia kichaa wananchi’ pale wanapowaambia; kwa mfano, kwa mara ya kwanza tangu Mungu aumbe ulimwengu, sasa wafugaji wa Tanzania wametajwa kwenye Katiba! Kwa mara ya kwanza tangu tupate Uhuru mwaka 1961 wakulima wametambuliwa kwenye Katiba! Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu wasanii na kazi zao sasa wametambuliwa rasmi! Wavuvi wanapewa maneno matamu wakiambiwa Katiba sasa itawatambua rasmi! Tumekuwa wa kwanza Afrika na hata ulimwenguni kuwa na Katiba itakayotoa uwakilishi sawa wa asilimia 50 kwa 50 kati ya wanaume na wanawake bungeni.

Kuna maneno mengi yanayozungumzwa na watetezi wa Katiba inayopendekezwa, alimradi tu kuwakonga nyoyo wananchi ili siku ya siku waweze kuipigia kura ya kuikubali.

Mitaani nako kuna tambo nyingi – kuanzia kwa vijana hadi kwa wazee. Nimewasikia wazee wakisema sasa haki ya matibabu na pensheni kwao ni mambo ya kikatiba! Waendesha bodaboda nao wanafurahi kweli kweli. Kila mmoja anaonekana kujawa na furaha isiyo kifani. Wanafurahi kwa sababu Katiba inakuja kufuta madhila yote yanayowakabili!

Huko nyuma nilipata kusema kwamba mimi nitakuwa wa mwisho kuishangilia Katiba mpya. Nilisema hivyo kwa sababu naamini kwa dhati kabisa, tatizo la Tanzania si ukosefu wa Katiba nzuri, bali ni ukosefu wa viongozi makini. Hapa naomba nisisitize – tatizo la Tanzania na Watanzania si Katiba, bali ni ukosefu wa viongozi makini na wenye weledi na uzalendo wa kuitumikia nchi na wananchi wake.

Nimekuwa nikiisoma Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 mara kwa mara. Sijaona ibara yoyote iliyobariki mabaya yanayofanywa sasa na baadhi ya viongozi wetu. Nimeipitia Katiba hiyo sijaona mahali popote ambako imesema tufanikiwe katika maeneo fulani na tufeli kwenye maeneo mengine. Hakuna.

Sijaona kwenye Katiba, kwa mfano, mahali ambako waziri fulani ameamuriwa kikatiba awe mchapakazi, lakini mawaziri wengine wawe wa kukamilisha akidi tu! Tena basi, sijapata ibara inayomtaka rais awe kimya – asimwajibishe kiongozi asiyefaa hata kama umma unaona hafai.

Hakuna mahali kwenye Katiba ya mwaka 1977 ambako kumehalalisha rasilimali za nchi hii zitumiwe na watawala kadri wanavyosikia. Maana tunaweza kulalama kuwa matumizi haya mabaya tunayoshuhudia sasa ni matokeo ya Katiba ya mwaka 1977 kutokuwa na ibara inayozuia hicho kitu.

Katiba ya mwaka 1977 imeweka ibara nzuri inayohusu haki za binadamu. Je, haki za binadamu nchini mwetu kwa sasa zikoje? Juzi tumesikia polisi Arusha, tena waliofundishwa kutenda kazi zao barabara, wakimsindikiza mtuhumiwa wa ulipuaji mabomu, na walipofika njiani eti akajaribu kuwakimbia. Wakampiga risasi. Akaaga dunia. Tukaambiwa alipigwa mguuni na kiunoni. Picha zinaonesha moja kapigwa tumboni!

Tumeshuhudia polisi wakimuua Daudi Mwangosi huku Kamanda wa Polisi wa Mkoa husika, akipandishwa cheo. Mauaji ya watuhumiwa yamekuwa mengi mno. Ndio maana najiuliza, mauaji haya au ukiukwaji huu wa haki za binadamu upo kwa sababu ya Katiba hii ya sasa ambayo inaonekana mbaya? Je, ujio wa Katiba mpya utayamalizaje?

Matukio hayo yataisha kwa mbinu gani kama aina ya viongozi ndio hawa hawa tulio nao? Je, si kweli kwamba haya tunayolilia sasa ni sawa na kuwa na chungu kipya (Katiba mpya), lakini mvinyo (mfumo wa uongozi) ukawa ule ule?

Kama tumeshindwa kuhakikisha watoto wetu wanapata madawati na wajawazito wakahudumiwa vizuri, haya ya pensheni kwa wazee wote Tanzania yatawezekana kwa mbinu gani? Je, tutakuwa tayari kuwabadili marais na mawaziri kila mwezi kwa kuvunja Katiba kwa kushindwa kwao kuwalipa pensheni wazee?

Hiyo Katiba mpya itakuja na miujiza gani ya kumaliza ajali ambako watu 40 wanafariki dunia, lakini hata kamanda kwa kikosi cha usalama barabarani wa wilaya hajiuzulu?

Taifa letu linakabiliwa na janga kubwa mno la vita ya wenyewe kwa wenyewe inayowahusisha wafugaji na wakulima. Haya mauaji ya sasa kati ya makundi hayo yanafanyika huku tukiwa na Katiba ya mwaka 1977 inayotambua haki na wajibu wa Serikali wa kuhakikisha kila kundi linatendewa haki. Haya yanafanyika wakati katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kukiwa na sheria inayohusu matumizi bora ya ardhi. Tujiulize, kitu gani kimekwamisha upimaji maeneo ya vijiji kwa kutumia Katiba na sheria za sasa ambacho ghafla kitarekebishwa na Katiba mpya?

Hapa naomba nirejee mgogoro wa ardhi kule Loliondo. Mwaka juzi na mwaka jana mwanzoni, Waziri wa Maliasili na Utalii wa wakati huo, Balozi Khamis Kaghasheki, alikwenda Loliondo akatangaza eneo la uhifadhi kwa mujibu wa sheria. Yeye alikuwa akitekeleza kile kilichokwishafanywa au kupendekezwa na Tume nyingi zilizopita. Akatenga eneo la uhifadhi wanyamapori. Eneo la mapitio ya wanyama (ushoroba) likaainishwa; na pia maeneo kwa ajili ya kilimo na kazi nyingine yakatengwa.

Wanasiasa wakaingilia kati kwa maslahi yao kupinga mpango huo. Hawakuwa na hoja zenye mashiko. Waziri Mkuu Mizengo Pinda akatishwa, na yeye akafunga safari kwenda kupindua uamuzi halali wa Kaghasheki. Hofu iliyomwingia, tena baada ya kujazwa uongo na makada kadhaa wa CCM, ni kwamba endapo msimamo wa Kagasheki ungeendelea, basi wana Loliondo walikuwa wamejiandaa kurejesha kadi za chama hicho na kujiunga upinzani.

Kwa hofu ya kupoteza wanachama (ambao si wengi), Pinda akaona njia sahihi ni kuua uhifadhi ili akiokoe chama chake na awafurahishe wale walioupinga mpango huo mzuri.

Sakata hili la ufutaji mpango wa Kagasheki halikumfurahisha kabisa kiongozi huyo, na kukawapo taarifa kwamba alikuwa radhi kujiuzulu. Lakini si hivyo tu, bali hata Rais Kikwete mwenyewe akikasirishwa. Yeye kama kiongozi mkuu wa nchi, na kama ilivyo ada yake, naye akabaki kimya. Hakuna mahali ambako Katiba ya mwaka 1977 ilipomtaka akae kimya wakati uhifadhi ukivurugwa. Hapa utaona maradhi ni viongozi, na wala si Katiba au sheria za nchi.

Ndugu zangu, kwa kigezo hiki ndio maana nasisitiza kuwa tatizo la Tanzania hadi hapa tulipo sasa si Katiba, bali ni ukosefu wa viongozi wenye maono na wasimamiaji wa kweli wa sheria za nchi. Viongozi wachapakazi hawapo, na kama wapo, basi ni wachache mno.

Sina lengo la kumwandama Mheshimiwa Pinda, lakini ebu tuangalie na hili. Mwaka jana Mheshimiwa huyu akaingia tena kwenye mvutano na Waziri wa Ujenzi, John Magufuli. Safari hii ilikuwa uzito wa malori. Magufuli akaamuru sheria zifuatwe kwa kuhakikisha uzito hauzidi ule uliowekwa kisheria tangu mwaka 1974. Sheria ziko wazi kabisa. Wafanyabiashara wakaona wanakosa faida maradufu kama walivyozoea kwa kuzidisha uzito. Wakatoa vitisho vya hapa na pale. Pinda, kwa kutumia kofia yake kama kiranja mkuu, akapindua tena agizo la Magufuli bila kujali lilikuwa la kisheria. Malori yameendelea kuzidisha uzito na kuharibu barabara ambazo hazitengenezwi kwa fedha za wenye malori, bali Watanzania wote kupitia kodi.

Ndugu zangu, kwenye jambo kama hili la barabara kuharibiwa vibaya, tatizo ni kukosa Katiba nzuri au kukosa weledi wa viongozi wetu katika kusimamia sheria? Hata tukiwa na Katiba mpya ambayo suala la uwajibikaji litawekwa kando, itasaidia nini? Je, si kweli kwamba tunahitaji viongozi walio tayari kupoteza nafasi zao alimradi tu wawe wasimamizi wa Katiba na sheria za nchi?

Nchi hii tuna sheria nyingi mno, tena zikiwamo za kuweka watu kizuizini na hata kunyongwa hadi kufa. Ebu angalia lile jengo la umma la Sh milioni 89 ambalo limejengwa kule wilayani Igunga! Fedha za umma zinatafunwa. Ushahidi unawekwa wazi, lakini hakuna wa kuwajibishwa wala hakuna mwajibishaji. Haya yanafanywa katika nchi yenye Katiba na sheria, lakini ikiwa haina wasimamizi wa Katiba na sheria hizo. Adhabu kubwa kabisa hapa tuliyonayo ni ya mtu kunyongwa hadi kufa. Tumeshindwa kumnyonga huyo aliyejenga jengo hafifu. Je, Katiba mpya itakuja na adhabu gani kali kuliko hiyo? Tunajidanganya.

Tunaweza kuwa na Katiba mpya hata 100 lakini kwa udhaifu huu wa kuwajibishana, tusitarajie muujiza.

Nasubiri kuona Katiba mpya ikiwapa vijana maisha bora ambao wanasiasa wamewaaminisha kuwa bodaboda ndiyo ajira! Nasubiri kuona namna ambavyo Katiba mpya itakavyomaliza ubakaji na utiwaji mimba wanafunzi, huku jamii yenyewe ikiwa kama haina habari.

Nasubiri kuona miujiza ya Katiba mpya namna itakavyoongeza idadi ya samaki katika mito, maziwa kwa kuzuia mabomu na sumu vinavyotumiwa sasa mbele ya macho ya polisi na walinzi wengine wa rasilimali za nchi.

Nasubiri kuona namna ambayo Katiba mpya itamaliza ajali zinazoua maelfu ya Watanzania kila mwaka huku watoa leseni wakiwa wameendelea kutopea kwenye rushwa.

Katiba mpya njoo uondoe mauaji ya vikongwe na albino huku viongozi wenyewe wakiwa ndio washirikina wakuu. Hiyo Katiba mpya ije haraka tuone kama ndiyo itakayoziamuru halmashauri za vijiji, miji, manispaa na majiji kuondoa mabango ya waganga matapeli wakidai wana uwezo wa kumuongeza akili mwanafunzi ili ashinde mitihani hata kama hakuna maabara, walimu wa kutosha, vifaa vya kufundishia na kwa kutumia hivi vitabu vya chenji ya rada vilivyojaa makosa na upotoshaji mkubwa.

Vitabu hivyo vina  kasoro za ubora licha ya kupata Hati ya Ithibati (Certificate of Approval) kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Kuna vitabu vya kiada vya darasa la saba vinavyokinzana katika mada moja. Mfano, mada ya ‘Ubongo wa Nyuma,’ ambako kitabu cha mchapishaji mmoja kikiandika kuwa ‘Serebelamu’ huhusika na matendo yasiyo ya hiari huku kitabu kingine kikielezea Serebelamu huhusika na uratibu wa matendo ya hiari.

Kwa Watanzania wengi, ili kuondokana na upotoshaji huu unaoharibu kizazi cha watoto wetu, dawa ni Katiba mpya! Wanaamini, si Katiba wala sheria za sasa zinazoweza kuondoa uzembe na upuuzi wa aina hii, isipokuwa kwa Katiba mpya tu! Haya ndio maajabu ya wote waliotopea katika kuamini kuwa Katiba mpya ndio mwarobaini wa upuuzi huu.

Uingereza hawana Katiba ya kuandikwa, lakini wako mbali sana kimaendeleo. Wako mbali kwa sababu kwao wameamini kuishi katika mila, kanuni na desturi zao zinazotawaliwa na uadilifu na dhamira ya kulijenga taifa lao hata kuutawala ulimwengu.

Kwangu mimi, Tanzania haijawahi kuwa na tatizo la Katiba, isipokuwa ukosefu wa viongozi wenye weledi na walio tayari kulitumikia taifa lao. ITAENDELEA.