Nikitaka kusema kweli (na ni lazima niseme kweli), Serikali ya Tanzania si mbaya kama watu wengine wanavyotaka kutuaminisha.
Kama ingekuwa mbaya basi mwaka 2012 isingewekwa katika kundi la Serikali kumi bora barani Afrika na wale wanaoshughulikia masuala ya utawala bora. Tatizo la Serikali yetu ya Tanzania ni kufuga matatizo bila kuyashughulikia hadi yanapoleta madhara makubwa.
Kabla sijazungumzia suala hili kwa undani, nizungumzie kauli aliyotoa Rais Jakaya Kikwete katika hotuba yake kwa Watanzania Machi 31, mwaka huu. Ilikuwa hotuba yake ya mwisho wa mwezi kuhusu uhusiano mbaya uliopo leo kati ya Waislamu na Wakristo.
Rais Kikwete alisema, “Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa mimi na Serikali ninayoiongoza, hatupendelei upande wowote. Hatufurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake. Ndiyo maana wako wahadhiri wa dini ya Kiislamu na wahubiri wa dini ya Kikristo wamekamatwa na kufunguliwa mashitaka kwa nyakati mbalimbali.”
Inawezekana huko serikalini hawafurahishwi na kitendo cha mtu kudhalilisha dini ya mwenzake. Lakini kitendo cha Serikali kufuga mihadhara ya Waislamu iliyoendelea kudhalilisha na kukashifu Ukristo kwa muda mrefu, kilileta picha kwamba walioko serikalini wanafurahishwa na kusikia Ukristo ukidhalilishwa.
Ukweli ni kwamba walioanza kudhalilisha dini ya wenzao ni Waislamu kuanzia miaka ya 1990. Wakristo, kama kawaida yao, walivumilia.
Zilitajwa sababu mbili zilizofanya Wakristo wavumilie. Kwanza dini yao inawataka wawe wavumilivu. Pili, imedaiwa kuwa Wakristo walijua sababu iliyowafanya Waislamu waukashifu Ukristo. Yalikuwa matokeo ya Waislamu kuwaonea wivu Wakristo, kwa mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na maendeleo yao katika sekta ya elimu.
Wakristo walifanya mikakati ya Injili ambayo ilizungumzia dini yao tu haikugusa Uislamu. Lakini Waislamu waliendelea kudhalilisha Ukristo hadharani kwa kutumia vipaza sauti, kwa mfano maeneo ya Temeke, Manzese na Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Wakati huo huo, mitaani kote kuna maofisa watendaji wa kata na polisi ambao waliendelea kusikia Ukristo ukiendelea kudhalilishwa, lakini hawakuchukua hatua yoyote. Wakristo wakaona kwamba Serikali ilikuwa inafurahishwa kusikia Ukristo ukidhalilishwa. Wakaanza kujibu mapigo.
Ndipo Serikali ilipoanza kuwakamata wahubiri wa dini ya Kikristo na wahadhiri wa dini ya Kiislamu, kana kwamba ilikuwa inatetea Uislamu kisisiri. Maana kabla ya Wakristo hawajaanza kujibu mapigo, wahadhiri wa dini ya Kiislamu waliokuwa wakiendelea kuudhalilisha Ukristo hawakuguswa.
Kwa kuwa Serikali ilileta picha kwa muda mrefu kwamba Waislamu wana haki ya kuudhalilisha Ukristo, Waislamu wakafika mahali ambapo waliona kwamba ni haki yao pia kuchoma makanisa na kuua viongozi wa makanisa. Hayo ni matokeo ya Serikali kufuga tatizo la udini.
Lakini Serikali haikufuga tatizo la udini tu. Imefuga matatizo mengi ambayo matunda yake tunayashuhudia.
Mwaka 2008 Serikali ililiambia Bunge kwamba ilikuwa inaandaa utaratibu mzuri wa masuala ya ujenzi, ambapo ungehakikisha kwamba maghorofa yanayojengwa hayahatarishi maisha ya wananchi. Leo jengo lililotakiwa liwe na ghorofa 10 limeachwa na Serikali liendelee kujengwa hadi kufikia ghorofa 16, likaporomoka na mmiliki wa kampuni ya ujenzi ni Diwani!
Orodha ya wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya ilipelekwa serikalini siku nyingi. Serikali ikafuga tatizo hadi kufikia mahali ambapo Tanzania inaongoza barani Afrika kwa dawa za kulevya. Leo wafanyabiashara hao wana nguvu kuliko serikali. Nani anabisha?
Halafu, kuna tatizo la mgomo wa walimu. Baada ya Serikali kufanikiwa kuishawishi mahakama ipige marufuku mgomo huo ilikaa kimya. Hadi leo haijawasiliana na walimu. Athari za kufuga tatizo hilo tumeziona.
Kisha kwa muda mrefu wadau wa elimu wamepiga kelele na kulaani matumizi ya vitabu vingi vya kiada, kwa darasa moja na kwa somo moja. Kwa kuwa huko serikalini wapo wanaonufaika na utitiri huo wa vitabu vya kiada, serikali imekaa kimya. Imefuga tatizo kwa hiyo walimu wamebaki mashuleni wakishindana kwa kufundisha mambo potofu. Tumeaingusha elimu.
Haiwezekani kuorodhesha matatizo yote ambayo Serikali imeendelea kufuga. Hali hii inasababisha wananchi kuona kwamba nchi yao imekosa utawala bora. Je, tabia hii ya Serikali kufuga matatizo haitaathiri chama tawala (CCM) katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2015? Twende tusubiri.