Ninatoka kusini mwa Tanzania mkoani Mtwara. Matukio yaliyotokea humo hasa kuanzia Desemba 2012 hapana shaka yamewashtua na kuwashangaza watu wengi.
Tumeshuhudia au tumesikia habari za ghasia zilizosababisha uharibifu mkubwa wa mali, ghasia zilizotokana na wakazi wa mkoa huo kupinga kiwanda cha gesi kujengwa mahali pengine badala ya huko Mtwara inakopatikana.
Binafsi ghasia hizo hazikunishtua wala hazikunishangaza kwa sababu nawajua vizuri sana watu wangu wa Kusini. Kwanza, watu wa kusini ni wamoja na hawakumbatii ukabila. Kwa hiyo wakitaka kufanya kitu hufanya kwa umoja. Ndiyo maana enzi za Mjerumani wakati maeneo mengine ya Tanzanyika ni kabila moja moja lililopambana na Mjerumani, Vita ya Majimaji ilivyopiganwa kusini mwa Tanganyika ilishirikisha makabila yasiyopungua 20!
Pili, watu wa kusini ni wavumilivu sana lakini uvumilivu wao una kikomo, baada ya hapo hufanya mambo ya kushangaza ulimwengu. Kule kusini kabila mojawapo ni la Wamakua. Wao wanapozungumzia ukomo wa uvumilivu husemwa, “Inwa yallumenlle wocha,” wakiwa na maana kwamba nyoka aliamua kuuma baada ya kuchoka kuvumilia.
Wakati wakazi wa kusini walipokuwa wakidai gesi ijengewe kiwanda Mtwara, tulisikia maneno ya kejeli yakisemwa dhidi ya wakazi wa Mtwara. Baadhi ya watu walidai kuwa kusini ni wanyonyaji tu ambao hawajatoa mchango wowote katika ustawi wa nchi hii. Huo ni ujinga wa kukosa kujua historia ya kusini.
Chukua, kwa mfano, Vita ya Majimaji ilivyonufaisha wananchi wa maeneo mengine ya Tanganyika. Baada ya vita hiyo, Mjerumani alipunguza sana ukatili wake. Adhabu ya viboko ilipungua sana. Tena, baada ya vita hiyo mwanajeshi hakuteuliwa tena kuwa gavana. Kwa hivyo, magavana wawili wa mwisho wa Kijerumani hawakuwa wanajeshi.
Basi unafuu uliopatikana nchi nzima baada ya Vita ya Majimaji ulitokana na mchango mkubwa waliotoa wananchi wa kusini katika kupambana na Mjerumani. Halafu wakati wa mapambano ya kutafuta Uhuru wa Msumbiji, wananchi wa kusini walisimama kidete kuwaunga mkono wananchi wa Msumbiji wakiongozwa na chama cha TANU. Wakaleta heshima kubwa Tanzania.
Kwa kuwa wakati ule Mreno akitokea Msumbiji alizoea kushambulia maeneo ya kusini kutokana na kitendo cha Tanzania kukiunga mkono chama cha ukombozi cha Msumbiji (FRELIMO), wananchi walikiomba chama cha TANU kiwape bunduki wawe na nafasi nzuri ya kupambana na Mreno.
Wakapewa wakafanikiwa kuiangusha ndege ya Mreno kule Kitaya. Ndipo mwaka 1971 chama cha TANU kikawaanzishia wakazi wa kusini Jeshi la Mgambo ambalo sasa linafanya kazi Tanzania nzima. Ni matunda ya wenyeji wa Kusini. Mwaka 1964 wakati FRELIMO ilipoanza kupambana na Mreno kwa silaha, wananchi wa kusini walipokea mamia ya wakimbizi kutoka Msumbiji, wakawapa kila msaada uliowezekana hadi walipotafutiwa makazi Rutamba.
Kiuchumi kuna wakati ambao zao la korosho lilichangia kwa kiasi kikubwa pato la Taifa kuliko zao la pamba. Basi, kejeli zinazotolewa leo dhidi ya wakazi wa kusini si kama tu zinawaudhi wananchi hao, bali pia zinasababisha wao kuona kwamba wanaonewa.
Kwamba wananchi wa kusini wanaona wanaonewa si mawazo yaliyoanza jana. Ni mawazo ya siku nyingi. Lakini wakati ule wabunge wa kusini waliongozwa na Mbunge machachari wa Newala, Stephen Nandonde (pichani kulia), hawakukaa kimya. Hali hiyo iliwaaminisha wakazi wa kusini kuwa wana watetezi. Hii ilisaidia sana kudumisha hali ya amani na utulivu. Wananchi hawakuchukua sheria mkononi.
Kwa mfano, Serikali iliposita kujenga barabra ya kusini wabunge wa huko walihamasisha wananchi kutoa michango kwa ajili ya kuanzisha ujenzi wa barabara hiyo. Ndipo mwaka 1980 Waziri Mkuu wa pili wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine, akazuia wananchi hao kuendelea kutoa michango hiyo akiwaambia kuwa ujenzi wa barabara haukuwa jukumu lao bali ni la Serikali.
Leo mambo ni tofauti. Wananchi wa kusini wanaona wanaonewa lakini hawana watetezi, kwa hiyo wamechukua sheria mkononi. Kuna uamuzi wa Serikali wa kuwahamisha wafugaji kutoka Bonde la Ihefu, Mbeya na kuwapeleka mikoa ya kusini ambako wamevuruga amani badala ya kuwarejesha walikotoka.
Kuna habari za kuhamishwa kwa vifaa Uwanja wa Ndege wa Mtwara na kupelekwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Arusha. Kuna habari za kuhamishwa kwa mradi mkubwa wa afya Tandahimba na kupelekwa Dodoma. Kuna tatizo la muda mrefu la wakulima wa korosho kukopwa korosho zao huku viongozi na wabunge wa kusini wakikaa kimya. Kuna kuchelewa sana kukamilishwa kwa ujenzi wa barabara ya lami kipande kilichopo kusini mwa Rufiji na kadhalika.
Vitendo hivyo vyote wakazi wa kusini wanaviona kuwa ni vya kuwaonea kwa sababu wamekosa watetezi. Matokeo yake tumeyaona. Wananchi wanapambana na wabunge wao kama walivyopambana na Mjerumani. Ni bora basi, viongozi na wabunge wa Mtwara wakijipambanua kwa vitendo kwamba wao ni watetezi halisi wa wananchi. Hii itasaidia kurejesha amani kusini ambayo imeanza kupotea.