ZANZIBAR
Na Masoud Msellem
Juni 29, 2021, Mahakama ya Katiba ya Afrika Kusini ilimhukumu aliyewahi kuwa Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma (79) kwenda jela kwa miezi 15 kwa kupuuza amri ya mahakama.
Amri hiyo ilimtaka atoe utetezi wa tuhuma za rushwa zinazomkabili kwa Tume ya Zondo (The Zondo Commission), inayoongozwa na Naibu Jaji Mkuu, Raymond Zondo.
Tume hiyo ilipewa jukumu na serikali kuchunguza madai ya ufisadi na rushwa yanayomkabili Zuma kwa kipindi chote cha miaka tisa ya urais wake.
Zuma alisitasita kujisalimisha kwa polisi ambao walipaswa kumtia nguvuni, pia akatumia haki ya kimahakama kupinga uamuzi wa mahakama.
Hata hivyo, hukumu ikabaki kama ilivyo na ikawa kwake lazima kutumikia kifungo kama ilivyoamuliwa na mahakama, na kufanya kuwa rais wa kwanza Afrika Kusini kufungwa jela.
Hali hiyo iliwafanya wafuasi wake na watu wengi kupinga kifungo hicho na kuanza kampeni kabambe ya kupigania Zuma kuachiwa huru.
Kampeni iliyoanza katika kumi la mwanzo la mwezi Julai ikiambatana na maandamano, vurugu na machafuko makubwa yaliyosambaa kila mahali kama moto katika nyasi kavu, kiasi cha kugharimu uhai wa watu zaidi ya 200, majeruhi wengi na mahabusu hadi jeshi likalazimika kuingilia kati!
Japo kwa juu juu, tutaona sababu ya vurugu za mara hii ni tofauti na vurugu nyingi zilizotangulia, hususan zile dhidi ya wahamiaji wa kigeni miaka ya 1994, 1995, 2008 na 2015 zilizolenga wahamiaji na wageni kwa kutenda uvamizi wa silaha, kuwaua, uvunjaji wa nyumba zao, kuwafukuza na kuwatoa kwenye makazi yao na kuvitaka vyombo vya dola viwarejeshe makwao. Lakini katika msingi wake ni sawa.
Vurugu za safari hii zilizoasisiwa na wafuasi wa Zuma zimeanza kwa sababu za juu juu za kuonyesha kutoridhishwa kwao na uamuzi wa kimahakama na vyombo vyao vya kusimamia haki pia kuwa na hisia kuwa kuna mkono wa kisiasa katika kuchafua jina na haiba ya Jacob Zuma.
Kwa upande wa serikali, msimamo wake juu ya ghasia hizi umedhihirishwa na Rais Cyril Ramaphosa, ambaye tangu kuzuka vurugu hizo ameshahutubia raia kupitia runinga mara tatu, ambapo serikali yake inaona kwamba machafuko hayo ni hujuma yenye lengo la kudhoofisha mamlaka ya katiba, kuharibu uchumi, kuondosha uthabiti wa kijamii na wa kidemokrasia.
Vurugu hizi na machafuko haya yenye kuambatana na kuzuia barabara nyeti za kibiashara, kupiga moto viwanda na vitega uchumi vikubwa, kuharibu mali na wizi uliovuka mipaka, hazionekani kuwa ni suala la kupigania uhuru wa Zuma tu, bali kadhia ya Zuma ni kama imedandiwa kuwakilisha machungu mengi ya wananchi hususan katika hali ya kisisa na kiuchumi.
Afrika Kusini licha ya kutajwa kuwa miongoni mwa vinara bora wa demokrasia, nchi ya pili kuwa na uchumi wa juu Afrika, ikiwa na miundombinu bora, nidhamu mwanana iliyoboreshwa ya masuala ya kifedha na kuwapo uzalishaji wa hali ya juu wa madini na viwandani, lakini nusu ya raia wake wanaishi chini ya mstari wa umaskini, na ukosefu wa ajira umetapakaa kiasi cha Rais Ramaphosa kuutaja kama “mgogoro mkubwa na wa hatari”. Hivi sasa ukosefu wa ajira ni asilimia 32 kwa miezi mitatu iliyopita ndani ya mwaka huu.
Profesa Mcebisi Ndletyana ambaye pia ni mchambuzi wa kisiasa nchini humo, ameiambia Al-Jazeera kwamba nchi hiyo ni miongoni mwa zile zenye hali mbaya sana katika kukosa usawa baina ya raia wake, jamii inajihisi kama imetelekezwa na serikali, hivyo kuamsha ghadhabu.
Uchumi wa kibepari umeisukumiza Afrika Kusini kama zilivyo nchi nyingine changa katika shimo la maangamizi ya ufukara na umaskini, licha ya rasilimali nyingi zilizopo.
Kukosekana uwiano wa kiuchumi baina ya wenye nacho na wasiokuwa nacho (maskini na matajiri), na kubwa na la hatari zaidi ni kuzalisha ghadhabu na kuchanganyikiwa kwa raia, na kusubiri tu fursa yoyote kupunguza chuki na ghadhabu zao.