Ni vizuri watu wakutathmini kuliko kujitathmini mwenyewe, lakini ninaloweza kusema ni kwamba kesho ndiyo natimiza mwaka mmoja tangu niwe Rais. Ninamshukuru Mungu kwamba tumeutimiza huo mwaka, lakini pia nawashukuru Watanzania kwa sababu ndani ya ushirikiano wao wa pamoja nchi yetu imeendelea kuwa ya amani, umoja na upendo na nchi yetu imezingatia malengo ya pamoja kama Watanzania kwenda mbele kwa ajili ya maendeleo.
Ninafahamu nilipokuwa nimechaguliwa kuwa Rais, ni nyakati tulipokuwa tukiomba kura kwa wananchi, yapo tuliyokuwa tunayaahidi, kwangu mimi niliyokuwa nikiyaahidi ni yale ya kutekeleza Ilani yangu ya Chama Cha Mapinduzi.
Tangu nilipoingia madarakani, nilitoa hotuba yangu ya kwanza kuelezea mwelekeo wangu wa Serikali nitakayoiongoza kule bungeni, na kwamba nilitaka niwe na Serikali ya ‘hapa kazi tu’. Kwamba kila mmoja ajitahidi kufanya kazi, tujenge nchi, iwe nchi ya viwanda, na mambo yaende mbele kwa manufaa ya Watanzania wote, ninafikiri nimetimiza hilo lengo.
Ninapozungumza hivi leo, makusanyo yameongezeka kutoka bilioni 800 kwa mwaka uliopita hadi wastani wa trilioni 1.2, na kwenye mwezi wa tisa yaliongezeka zaidi mpaka trilioni 1.592, na kwa sababu hiyo imetuwezesha kupanga bajeti ya trilioni 29.5.
Na kwa sababu hiyo, imetuwezesha katika bajeti ya 2016/17 tupange bujeti ya shilingi trilioni 29.5. Na katika bajeti hiyo tuliweka msisitizo kwamba fedha ambazo zitakwenda kwenye miradi ya maendeleo ifike asilimia 40, bahati nzuri Bunge lilipitisha kwa miaka ya nyuma ilikuwa inafikia asilimia 26 tu.
Mfano, kwenye miradi ya miundombinu, bajeti iliyotengwa na kupitishwa ilikuwa ni trilioni 5.47 na kwa sababu hiyo mipango inayoendelea na mipango mingine ambayo imeanza kutekelezwa ni mikubwa zaidi.
Kwenye kujenga reli, tumeamua tujenge reli sisi wenyewe, na ndiyo maana tumetenga shilingi trilioni 1. Mpaka sasa hivi makandarasi ambao wamechukua zile tenda ni zaidi ya 40, nina uhakika wanatakiwa kurudisha mwezi huu ili tujenge ‘standard gauge’, awamu ya kwanza itaanzia Dar es Salaam hadi Morogoro na fedha ipo.
Kutokana na kutenga hizo trilioni 5. 47 za miundombinu, tumeweza kununua ndege, na ndege zote tumezilipia, ndege mbili zimeshafika ambazo ni Bombardier Q400, tulilipa advance payment na zilipofika hapa tulilipa kiasi kilichobaki.
Mbali na hizo ndege, tumeagiza ndege nyingine tatu na tumeshatoa advance ya asilimia 30, ndege moja ni Bombardier itafika mwezi wa sita mwakani na nyingine mbili ni Jet aina ya SC 300 ambazo zinabeba watu kati ya 137 hadi 150, hizo nazo zitafika mwazoni mwaka 2018, kwa sababu sasa ziko viwandani zinatengenezwa.
Tumelipa advance payment ya dola milioni 10 kwa ajili ya ndege nyingine ya nne kutoka Boeing yenye uwezo kubeba watu 242. Nadhani watakuja kwa ajili ya mazungumzo ya awali mwezi huu.
Kama tunataka kujenga utalii, hatuwezi kufanya hivyo kwa ndege za kubahatisha, lazima tuwe na ndege zenye uwezo wa kutoka Marekani, Beijing, China na Urusi, mpaka kufikia mwanzoni mwa 2018, Tanzania tutakuwa na ndege saba hivi, tutakuwa mahali pazuri kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha usafiri wa anga. Kuhusu madaraja na barabara wote mnafahamu.
Katika suala la kilimo, tumeweza kutenga bajeti ya trilioni 1. 56, bahati nzuri katika kuonesha reflection kwamba tuko serious, na masuala ya kilimo, wawekezaji wengi wameanza kujitokeza, mfano kuna wawekezaji wa kampuni ya Ujerumani, ambao wanataka kujenga kiwanda kikubwa kule Lindi, ambacho kinaweza kuajili hata watu 10,000.
Lakini kutokana na hilo na masharti ambayo tumeamua kuyaweka kwenye kilimo, kwa sasa hivi wakulima wameanza kuona matunda ya kuweka maelekezo mazuri katika kilimo chetu.
Kwa ndugu zangu wa Mtwara na Lindi, kama wako hapa wanafahamu, siku za nyuma kilo moja ya korosho ilikuwa inauzwa kwa wastani wa sh 1000, kwa mwaka huu na katika mwezi huu tulioumaliza kilo moja ya korosho imeuzwa sh 4000, hiyo ni mara nne zaidi. Kwa hiyo nina uhakika watu wa Mtwara na Lindi watakuwa hawalalamiki sana kwamba mifuko imekosa hela, kwa sababu wamefanya kazi, wamezalisha korosho. Hata kwenye zao la pamba kuna baadhi ya maeneo imenunuliwa kwa sh 1300 kwa kilo, tunafanya hivyo ili kuhakikisha yale makodi ya hovyo hovyo, ambayo yamekuwa ni kero kwa wakulima tunayatoa.
Nishati
Bajeti iliyopitishwa ni ya sh trilioni 1.3, katika hilo tumeanza sasa kuboresha miundombinu yetu inayohusu nishati, ile Kinyerezi 1, tumeshalipa zaidi ya dola milioni 20 ili kufanya upanuzi wa ili tuzalishe umeme wa megawati 335, tumeweka mradi mwingine Kinyerezi 2, ambao utatoa megawati zaidi ya 240 na kampuni ya Sumitomo inafanya kazi pale na tayari tumeshaweka jiwe la msingi, lakini tunataka kuwa na Kinyerezi 3, ambayo itatoa megawati 600, tutafikisha pia Kinyerezi 4, itakayozalisha megawati 350, tunafanya hivi ili kufika mwaka 2020 Tanzania iweze kuzalisha zaidi ya megawati 5,000 kutoka kwenye tulizonazo sasa hivi za megawati 1,500. Tunafanya hivi ili kuhakikisha kwamba nchi ya viwanda inapatikana.
Elimu
Bajeti ya mwaka huu 2016/17, ni sh trilioni 4.47, tulipoingia madarakani tuliahidi kwamba Watanzania sasa lazima wapate elimu bure kuanzia darasa la kwanza mpaka sekondari. Lakini wakati tunaingia fedha hizo za elimu bure hazikuwapo, ila kutokana na makusanyo makubwa ya kodi yaliyopatikana tukawa tumepata ziada, ndiyo maana tukaanza kuwa tunatoa sh bilioni 18.77 kila mwezi kwa ajili ya kwenda kutoa na kutekeleza hili suala la elimu bure.
Limekuwa na changamoto zake, moja ya changamoto ni kwamba, idadi ya wanafunzi iliongezeka kwenda kusoma, darasa la kwanza usajili umeongezeka kwa asilimia 84, kidato cha kwanza umeongezeka kwa asilimia 26, pakawapo na changamoto za madawati, tunashukuru kwamba hizi changamoto za tumezitatua kwa zaidi ya asilimia 90.
Mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu, katika bajeti iliyopita fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi wa elimu ya juu zilikuwa sh bilioni 340, kwa sababu ya mapato yaliyokuwa yanakusanywa kwa wingi, tukaongeza mpaka zimefikia sh bilioni 473, wanafunzi waliokuwa wanatakiwa kupata mkopo ni 98,000, sasa wamefika 124,320.
Katika bajeti ya mwaka huu tumeongeza sh bilioni 10, kwa hiyo zimetengwa sh bilioni 483, kwa ajili ya kuwakopesha wanafunzi, kila jambo zuri halikosi changamoto zake, wakati tumechukua hatua za kuwakopesha wanafunzi wengi, wamejitokeza wanafunzi wengine hewa na wamekopeshwa.
Wapo wengine waliokuwa wamemaliza vyuo vikuu lakini wakaamua kurudi tena vyuo vikuu ili wakapate mikopo, kwa hiyo zikawa zimekopeshwa zaidi ya sh bilioni 3.5 kwa wanafunzi ambao hawakustahili kupata mikopo.
Katika shule za msingi nako mnafahamu zimejitokeza changamoto ambako baadhi ya walimu wameandikisha wanafunzi wengi zaidi, uhakiki umefanyika nako tumekuta wanafunzi hewa. Changamoto hizi zipo pia katika watumishi hewa, ambapo kwa sasa hivi wamefikia karibu 17,500, tunaendelea kufanya haya yote katika kujenga nidhamu ya kutengeneza Tanzania iliyo mpya na yenye mwelekeo mpya.
Maji
Kwenye sekta ya maji, bajeti ni sh trilioni 1.02. Kwa ujumla tu naweza kusema tunaelekea kizuri na tuko kwenye mstari mzuri. Tunapata sapoti kubwa ya Watanzania na ninyi waandishi, na ndiyo maana uchumi wa nchi yetu mwaka jana ulikua kwa asilimia 7, tumelenga katika mwaka huu ukue kwa asilimia 7.2, katika robo mwaka mbili za mwanzo viashiria vya uchumi vinaonesha kwamba uchumi wetu umekuwa kwa asilimia 7.9 na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi tano ambazo uchumi wake unakwenda vizuri, nafikiri ya kwanza ni Ivory Coast na ya pili ni Tanzania. Mfumuko wa bei umeshuka kutoka asilimia 7 hadi 4.5 haya yote yanaonesha ni kiashiria kizuri.
Najua watu watasema uchumi unakua, mbona pesa hazipo? Pesa haziko mifukoni mwa wale waliokuwa wamezoea kupiga dili, na zitaendelea kukosa tu, huo ndiyo ukweli. Lakini kwa watu wanaofanya kazi na kujituma, pesa watapata tu. Ni kama wale wa Mtwara waliolima korosho wameuza korosho zao, kwa sh 4000 kwa kilo badala ya sh 1000, walivyouza mwaka jana.
Kwa hiyo kwa tathmini ya haraka haraka naweza kusema tuko kwenye mwelekeo mzuri lakini hatujafikia mahali penyewe ninapopataka kwa sababu nataka nchi hii siku moja Tanzania isiwe nchi ya kupata misaada bali iwe inatoa misaada, na huo ndiyo mwelekeo wangu na ndiyo nia yangu na nina uhakika ndiyo nia ya kila Mtanzania kwamba Tanzania ifike mahali iwe nchi tajiri.
Tanzania ina kila kitu madini ya aina zote yapo, kule Ruangwa sasa hivi kuna graphite, ambayo imeshavumbuliwa, madini hayo ndiyo hutumika kutengeneza magari yanayojiendesha bila kutumia betri, ni madini maada ya almasi, madini hayo ni hydrocarbons, kama almasi ilivyo.
Lakini Tanzania tuna Ethanol ya kutosha ambayo ni gesi inatoka kule kusini mpaka Ruvu ipo, ambayo inatumika kwenye nishati ya mafuta, tumepata madini mengine ambayo ni nadra kupatikana, gesi ya helium, gesi hiyo iko nchi tatu tu duniani, kwa hiyo Tanzania ni tajiri na kinachotakiwa ni kujua tunatumiaje utajiri wetu kusonga mbele.
Kubana matumizi serikalini
Palikuwa na safari za hovyo hovyo tu, watu wanapishana angani, niliamua kuzuia safari hizo kwa kuanzia na mimi mwenyewe, kwamba ukitaka kutoa maagizo lazima uanze na wewe mwenyewe, nimealikwa mialiko zaidi ya 47, nimeweza kwenda mialiko mitatu, sikwenda hata kwenye mikutano mingine mikubwa maana naamini bado tunaweza tukawakilishwa na mabalozi wetu walioko kule, na wakaleta matokeo yaleyale.
La sivyo hapakuwa na sababu ya kuwa na mabalozi halafu sisi wenyewe tena twende huko, watu zaidi ya 100, tunahitaji kulipwa posho, wakati wananchi wetu wanahangaika kwenye mahospitali kupata matibabu. Kwa hiyo, nimefanya hivyo kwa lengo la kuhakikisha kwamba tunakuwa na Tanzania mpya yenye mwelekeo, katika kufanya hivyo bado mataifa mengine wametuheshimu na kututembelea na ndiyo maana mmeona katika kipindi hiki tumetembelewa na Rais kutoka Vietnam, Waziri Mkuu wa India, Mfalme wa Morocco, Rais wa Rwanda, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo. Zaidi ya maraisi saba wametutembelea hapa na tumeingia nao mikataba mbalimbali.
Katika hilo la kuonesha ninavyobana matumizi, wenzangu wakaamua kuwa wananipa vyeo, wakanichagua kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, juzi juzi wamenichagua kuwa mwenyekiti wa taasisi ya siasa, ulinzi na usalama ya SADC (SADC-Troica).
Sasa sifahamu kama hayo niliyoyasema yanafaa katika kujitathmini, lakini nilitaka tu kueleza tumepanga Tanzania kuwa ya viwanda, mwelekeo ni mzuri, wawekezaji wapo, juzi nilikuwa Kenya, nilieleza tu na wao wakashangaa kwamba makampuni yaliyowekeza Tanzania kutoka Kenya, yako 524, yamewekeza dola za Marekani bilioni 1.7 na kutengeneza ajira 56,260.
Hiyo ni Kenya tu, na imeifanya nchi hiyo kuwa moja ya nchi zenye makampuni mengi yaliyowekeza hapa nchini, najaribu kueleza hili na sifahamu kama nimejibu vizuri swali lako lakini ninachotaka kukueleza kwa maoni yangu, ninaona tunakwenda vizuri na ndiyo maana nimepunguza sherehe, sherehe za Uhuru nilichukua hizo fedha tukatengeneza barabara ya Mwenge, nina uhakika hata wewe Ayub Rioba unapita palepale, inawezekana hata msongamano umepungua kidogo.
Palikuwa na sherehe nyingine fedha zake nikapeleka Mwanza zikajenge barabara. Tunayafanya haya katika kuwatumikia Wwatanzania, Bunge nao walibana matumizi tukanunua vitanda pale Muhimbili, akina mama na watoto wanalala vizuri.
Ndiyo maana utaona katika bajeti ya Wizara ya Afya mwaka huu, tumetenga sh trilioni 1.99 kwa mara ya kwanza pesa zilizotengwa kununua dawa mwaka jana zilikuwa sh bilioni 31 lakini mwaka huu ni sh bilioni 250 na ndiyo maana palikuwa na upungufu wa chanjo sasa zimeingia zote. Sasa nisije nikamaliza utamu, kama ulikuwa ni utanguli basi ni huo.
>>ITAENDELEA>>