Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoa wa Dar es Salaam umeamua kuboresha viwango vya ubora wa barabara zake katika mitaa.
Akizungumza na Gazeti la JAMHURI, Mratibu wa TARURA Mkoa wa Dar es Salaam, Mhandisi George Tarimo, amesema wameamua kutumia njia ya ubunifu zaidi wakati wa kujenga barabara hizo kuliko huko nyuma ili ziwe imara na kupitika wakati wote.
Mhandisi Tarimo amesema mtindo wanaoutumia kujenga barabara sasa hivi, kabla ya mradi kuanza wanatumwa wataalamu kwenda eneo husika kufanya upembuzi kabla ya kuanza ujenzi wowote.
Amesema waliamua hivyo baada ya kutambua changamoto zilizojitokeza wakati wa kuendesha miradi huko nyuma.
Mhandisi huyo amesema kwamba utaratibu huo ulioboreshwa una lengo la kutambua uhalisia wa eneo kama kuna udongo wa aina gani na kiwango cha maji kilichopo katika eneo kabla ya kuanza ujenzi.
Amesema wameamua kutumia mfumo huo wa kisasa wa kuanza kupima eneo kabla ya ujenzi, kwani umefanya barabara nyingi za mitaa kuwa imara kuliko huko nyuma.
Tarimo amesema kwamba wanaendelea kuboresha barabara za mitaani kadiri wanavyopata pesa kutoka Benki ya Dunia (WB), ambapo katika awamu hii miradi inayoendelea imegawanyika katika sehemu mbalimbali za wilaya.
Kinondoni wameboresha barabara ya Sokoni – Makuburi km 1.5, Nzasa km 1.25, Viwandani km 2.21, Tanesco – Sokoni km 0.16, ujenzi na gharama nyingine vimegharimu jumla ya Sh bilioni 22.81.
Barabara nyingine ni Makanya kilometa 5.1, Tandale Kisiwani km 0.4, Kilima km 1.3, Kilongo Wima km 2.1, CBD – Makumbusho km 0.8, gharama zake ni sawa na Sh bilioni 28.93.
Maji Chumvi – Kilungule, Africana – Kinzudi, Shimboni, Msasani, Moringe, Mabatini, Changanyikeni Shule, Tegeta Nyuki, Magomeni Dosa, Mkadini, Dunga na Arsenal Magoti.
Katika Wilaya ya Kigamboni, TARURA imetengeneza barabara zenye urefu wa kilomita 40, barabara hizo ni Tungi Mjimwema na Upondo Vijibweni.
Katika Wilaya ya Ubungo barabara iliyojemgwa ni ya Kibamba – Segerea.
Kwenye Wilaya ya Temeke, TARURA imejenga barabara za Mango – Chihota km 0.860, Mdosi – Alafu km 1.5, Kijichi – Toangoma km 3.3, Mwanamtoti km 1.8, Chang’ombe km 1.9, Mchicha km 1.8 na Temeke – Mbagala km 3.5.
Katika Wilaya ya Ilala, Buguruni Mnyamani km 2.3, Barakuda -Chang’ombe km 0.5, Olympio km 0.68, Kiungani km 0.7, Kongo km 0.4, Kingu km 0.53 na Ndanda km 0.35.