Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma
WAKALA wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) umesema unaendelea na ujenzi wa barabara na madaraja katika maeneo mbalimbali nchini ili kuhakikisha wakulima wanayafikia masoko kwa haraka.
Hayo yamebainishwa kwenye Maonesho ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) ambayo kitaifa yanafanyika jijini Dodoma, na Mratibu wa Madaraja na Barabara za Mawe kutoka Tarura, Mhandisi Mshauri, Phares Ngeleja.
“Tumekuwa tukitumia mbinu mbalimbali ambazo zimewezesha ujenzi wa madaraja na barabara. Hii imesaidia wananchi vijijini kufika sehemu ambazo hazifikiki, ina kuwawezesha wakulima kusafirisha mazao yao kutoka vijijini mpaka maeneo ya masoko na kwenye maghala,” amesema Mhandisi Ngeleja.
Amesema kuwa Wakala huo umekasimiwa kusimamia kilomita 144,429.77 ambapo kazi kubwa inayofanywa ni ujenzi na ukarabati wa miundombinu hiyo.
Amefafanua kuwa, tangu wakala huo ulipoanzishwa mwaka 2017 wamejenga madaraja 275 nchi nzima yaliyogharimu Sh. Bilioni 10 huku Mkoa wa Kigoma ukiwa unaongoza na kwamba kama wangejenga kwa kutumia zege na nondo wangetumia zaidi ya Sh. Bilioni 50.
Aidha amesema ili kuwafikia wananchi kwa haraka wanajenga barabara kwa kutumia mawe ambapo katika Mkoa wa Mwanza wamejenga kilomita 20 za mawe, Kigoma (kilomita 3.34), Rukwa (mita 350), Morogoro (mita 310).
“Licha ya kutumia mawe pia tunatumia teknolojia zingine, mfano katika Mkoa wa Dodoma tuna barabara ya daraja dogo kilomita moja, Chamwino tuna zaidi ya kilomita saba, Iringa tuna zaidi ya kilomita sita pamoja na Mkoa wa Simiyu. Tutatumia teknolojia hizi kufungua barabara nyingi zaidi tuwawezeshe wakulima wafike maeneo yasiyofikika na kuyafikia masoko kirahisi,” amesema.
Kaimu Meneja wa Tarura Jiji la Dodoma, Mhandisi Kasongo Morijo, amesema wanahudumia kilomita 1,189 za barabara na kati ya hizo 224 ni za changarawe, 715 za udongo na 248 za lami.
Amesema wana miradi ya matengenezo na miradi mikubwa ya lami ambayo inalenga kuhakikisha maeneo yanafikika kuwezesha upatikanaji huduma za kijamii na kutolea mfano ujenzi wa Barabara ya Kisima cha Nyoka – Nkuhungu kuhakikisha wananchi wanafika mjini bila kikwazo.
“Tunataka kuhakikisha mpaka mwaka 2025 maeneo mengi ya Jiji la Dodoma yawe na lami na yaweze kupitika kwa wakati,” amesema Mhandisi Morijo.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano Tarura, Catherine Sungura, amesema wanatumia maonesho hayo kuelimisha umma namna wanavyojenga miundombinu ya barabara, madaraja na mifereji.
“Kazi kubwa imefanyika nchini, vijijini tumefanya kazi kubwa ya kufungua barabara ambazo zimewasaidia wananchi kuinuka kiuchumi na kupata maendeleo. Barabara ambazo tunajenga zimewasaidia wananchi mfano wajawazito walikuwa wanapata shida kufika kwenye huduma za afya lakini hivi sasa wanapata huduma bila changamoto, watoto wanakwenda shule na wakulima wanasafirisha mazao yao,” amesema Sungura.
Aidha amesema wana miradi katika mashamba ya Chai Kilolo mkoani Iringa na Tukuyu mkoani Mbeya ambako kuna barabara za lami zinazowarahisishia wakulima kusafirisha chai na kwenda kiwandani.
“Kufunguliwa kwa barabara hizi kumewezesha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na wa eneo husika kubadilika na tunaingiza kipato kwa serikali, tunajivunia kazi kubwa ambayo tumeifanya. Bado tuna vipaumbele vya kuhakikisha tunafika kusikofikika…tunawakaribisha wananchi wafike katika banda letu waone kazi kubwa inayofanywa na Tarura,” amesema Sungura.