Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Morogoro
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) ina lengo la kuhakikisha barabara zote nchini zinapitika kwa asilimia 85 ili kuinua uchumi na kuwezesha huduma za kijamii kwa wananchi ifikapo mwaka 2025/2026.
Hayo yamesemwa na Mtendaji Mkuu wa TARURA Mhandisi Victor Seff wakati wa ufunguzi wa kikao cha Baraza la Wafanyakazi wa TARURA kilichofanyika mkoani Morogoro leo tarehe 4 Aprili, 2024.
Mhandisi Seff amesema Baraza hilo ambalo lipo kisheria ni njia ya kuwashirikisha wafanyakazi ili kutoa michango yao ikiwemo masuala mbalimbali kuhusiana na utendaji wa Wakala.
Mhandisi Seff amesema kwa sasa zaidi ya Km 100,000 ya Mtandao wa Barabara za Wilaya ni za udongo na zinaathirika zaidi wakati wa mvua zinaponyesha hivyo lengo lao ni kuwezesha barabara hizo ziweze kupitika msimu wote.
“Mtandao wetu wa barabara za Wilaya una urefu wa Km 144,429.77, lengo letu ni kuhakikisha barabara zote zinapitika msimu wote kwa asilimia 85 ifikapo mwaka 2025/2026″, amesema Mhandisi Seff.
Pia ameongeza kuwa vikao hivyo vinasaidia kuboresha maslahi ya wafanyakazi na namna ya kuweza kuboresha utendaji kazi wa TARURA kutokana na maoni na mapendekezo yao.
Naye, Kaimu Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi Serikali za Mitaa Tanzania (TALGWU) Dkt. Almas Suleiman amewapongeza TARURA kwa kurudisha mawasiliano ya barabara katika msimu wa mvua na kuwakumbusha Watendaji wa TARURA kuisikiliza jamii ili kuepuka migogoro inayoweza kutokea katika maeneo yao.
Wakati huo huo Mwakilishi kutoka Chama cha Wafanyakazi wa Migodi, Nishati na Ujenzi (TAMICO) Bw. Paternus Rwechungura ameipongeza TARURA kwa kufanya kikao hicho na kuwaomba wajumbe kujiunga na chama hicho ili kuweza kuwasaidia wafanyakazi mara wapatapo changamoto za kikazi.
Bi. Tulia Msemwa Mwakilishi wa Kamishna wa Kazi, kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu, amesema wao kama wasimamizi wakuu wa vyama vya wafanyakazi mahali pa kazi awewaasa wajumbe kuweza kuchangia maoni na mapendekezo ambayo yatasaidia Wakala kufikia malengo na dhima kwa yale waliyojiwekea ili kuleta ufanisi kulingana na dira ya Wakala hiyo.