Na Mwamvua Mwinyi,JamhuriMedia,Kibaha
WAKALA wa barabara mijini na Vijijini (TARURA) wilaya ya Kibaha , mkoani Pwani imependekeza jumla ya sh.bilioni 59.3 kwa ajili ya kugharimu miradi 26 ya maendeleo ya barabara katika kipindi cha kwa mwaka 2023/2024.
Kaimu meneja TARURA Kibaha , Mhandisi Bupe Angetile alitoa taarifa hiyo katika kikao cha baraza maalum la madiwani cha kupitia na kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti ya kazi za matengenezo na ujenzi wa barabara kwa mwaka wa fedha 2023 /2024 TARURA-Kibaha katika Halmashauri Mji Kibaha.
Mhandisi Bupe aliiomba Serikali kupitisha mapendekezo hayo ili kuweza kufungua milango ya maendeleo.
Vilevile alitoa mchanganuo wa rasimu ya mapendekezo kwenye matengenezo ya kawaida km .131 sh.milioni 398.46, matengenezo ya maeneo korofi km.46.22, matengenezo ya muda maalum km.16.87 sh.milioni 417.06, makalavati 11 milioni 77, usimamizi milioni 71.27,adrics milioni 31.43.
Hata hivyo alieleza,lengo kuu la mpango wa bajeti ya mwaka 2023-2024 kama ilivyokuwa kwa mipango iliyopita ni kuondoa mapungufu ndani ya mtandao wa barabara uliyo chini ya usimamizi wa TARURA wilaya.
Alielezea, katika rasimu ili kuimarisha mtandao wa barabara mahitaji halisi ya matengenezo ni sh.bilioni 10.6 kwani barabara zilizo nyingi zina malimbikizo ya matengenezo ambayo husababisha hali ya barabara kuwa duni na hivyo kuhitaji kiasi kikubwa cha fedha za kuzirudisha kwenye hali nzuri na ya kuridhisha.
Katika hatua nyingine Bupe alisema ,Utekelezaji wa mpango na bajeti ya miradi ya maendeleo na matengenezo kwa mwaka 2022-2023 katika mwaka wa fedha 2022-2023 Halmashauri ya Mji wa Kibaha ,wilaya ya Kibaha ilitengewa Bilioni 2,770,910,000.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha,Mussa Ndomba aliwataka TARURA kuwa na barabara alizoahidi mbunge wa Jimbo la mji wa Kibaha pamoja na madiwani na kuzipa kipaumbele ili wasije kuhukumiwa na wananchi wakati za chaguzi kutokana na kutotimiza ahadi.
Ndomba alieleza, kwa upande wa Halmashauri imejipanga kutenga kiasi cha fedha ili kuongeza nguvu kwa maboresho ya barabara.
Akichangia taarifa hiyo ,diwani wa kata ya Visiga Kambi Legeza aliiomba TARURA kuangalia kwa umuhimu barabara ya Kidugalo -Mihande kuimarisha miundombinu ya barabara.
Alisema wameisemea kipindi kirefu barabara hiyo lakini utekelezaji bado, barabara nyingine ni Visiga-Mbwawa yenye km .9 na ile ya kuelekea Bwawa la Chumvi na ya kuelekea ofisi ya kata na Visiga Sekondari.
Nae diwani wa kata ya Mailmoja, Ramadhani Lutambi alieleza , TARURA haijafika miezi 15 kwenye kata hiyo, na kuomba barabara ya BP-Sheli yenye km 3.8 iangaliwe namna ya kuiboresha.
Akijibu hoja hizo, Mhandisi Bupe alieleza , changamoto wanayokabiliana ni ufinyu wa bajeti, wanahitaji nguvu ya ziada kuombea fedha barabara ambazo zilishaombewa lakini bado utekelezaji wake.
Alitaja changamoto nyingine zinazokwamisha kazi zao ni uwepo wa miundombinu mbalimbali ikiwemo ya DAWASA, TANESCO katika barabara zinazojengwa suala linalosababisha gharama ya kuiondoa kuwa kubwa