DC, Mwenyekiti CCM Mkoa hapatoshi
Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa yaketi
TARIME
NA MWANDISHI WETU
Hali si shwari kati ya Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime mkoani Mara, Glorious
Luoga, na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara,
Samuel Kiboye (Namba Tatu).
Kumekuwa na kurushiana maneno makali kati ya viongozi hao, na sasa mvutano
huo unaelezwa kwamba umepanuka hadi kuhusisha wapambe wa kambi mbili za
viongozi hao.
Kiboye anamtuhumu DC Luoga kwenye uwekezaji wa shamba la miwa, akidai
ametafuna fedha zilizotolewa na Mgodi wa North Mara kwa ajili ya kufanikisha
malipo ya kazi zilizohusu upimaji eneo la shamba hilo.
Pia Mwenyekiti huyo anamtuhumu DC kwa ahadi ya Mgodi wa North Mara ekari
800 kama sehemu ya uwekezaji kwenye shamba la miwa kutokana na kuisaidia
wilaya Sh milioni 214 zilizotumika kuandaa mpango wa uwekezaji huo; huku
akisema wilaya haina ardhi.
Wiki iliyopita, Halmashauri ya CCM Mkoa wa Mara iliketi mjini Musoma, ambako
suala la uwekezaji huo wa shamba la miwa lilichukua sehemu kubwa ya
majadiliano.
Mwenyekiti huyo, akionekana mwenye hamaki, akasema, “Hatuwezi kuacha
mambo kama haya bila kumsaidia Rais Magufuli. Haya mambo ndiyo
yanayosababisha CCM tutukanwe. Huyu DC anayo ekari 800 Tarime wapi?
“Lakini, hao watu [wawekezaji] wakaniletea malalamiko wakasema, ‘wewe ndiyo
Mwenyekiti wa Mkoa wa CCM, DC yupo chini yako, mwambie atupe ekari zetu
800 alizotuahidi sawa sawa na eka 2,040’. Hizi hekta 800 alizomuahidi mwekezaji,
atazitoa wapi na ushahidi upo? Nikisema mwenyewe mtasema nina malumbano
na yeye. Leo nimeamua kulisema mbele ya kikao hiki,” alisema Kiboye.
Mwenyekiti huyo amedai kuwa mwekezaji, kampuni ya Nile Agro Industries Ltd
kutoka Uganda, amekataa kuendelea na mradi huo hadi DC Luoga atakapokuwa
ameondolewa Tarime. Mwekezaji huyo wa kigeni atashirikiana na wawekezaji
wazawa ambao ni CMG Investment Ltd na Pravin Shah.
Luoga hakuhudhuria mkutano huo licha ya kuwapo wakuu wa wilaya kadhaa za
Mkoa wa Mara na Mkuu wa Mkoa huo, Adam Malima.
“Mwambieni DC wa Tarime aache kunitukana…angekuwapo leo humu DC
asingetoka. Na mimi nisingetoka. Nimekuja na hasira sana leo, ndiyo maana
nimekuja na helikopta [hapakuwapo helikopta].
“Matusi yake sasa yafike mwisho. Amenitukana, anaendelea kunitukana,
ananidhalilisha mbele ya wananchi. Nasema leo mwisho. Akirudia atapata
anachokitaka, basi. RC najua umelichukua hilo. Mwambie asinitukane. Aniache
niendelee na kazi yangu na yeye aendelee na kazi yake. Kazi yangu na yake
haziingiliani. Asinitukane, nimesema leo mwisho,” alisema Kiboye.
Mara zote Luoga amekanusha kufuja Sh milioni 214 alizoomba Mgodi wa North
Mara.
Barua ya North Mara Community Trust Fund, ya Machi 29, mwaka jana
iliyosainiwa na Meneja wa Mfuko huo, John Waigama, inaonesha mgodi huo
kukubali kumpatia DC Luoga fedha hizo kama alivyoomba kwa ajili ya mradi wa
miwa. Luoga alishukuru kupokea msaada huo kupitia barua yake ya Machi 30,
mwaka jana.
Mradi huo unakusudiwa kutekelezwa katika vijiji sita vya Mrito, Weigita, Matongo,
Keisaka, Bisarwi na Kerende.
Aprili 13, mwaka jana, fedha hizo ziliingizwa kwenye akaunti ya DAS-IMPREST
katika Benki ya NMB, Tawi la Nyamongo zikitoka akaunti ya North Mara
Commercial Business Limited.
Barua ya DC Luoga inasema kiwanda cha miwa kitajengwa ndani ya eneo la
hekta 40.
“Mara mradi utakapoanza, mwekezaji wa mradi huo atakuwa anachangia asilimia
fulani (hakuitaja) kwa ajili ya kuendeleza mfuko (Trust Fund),” inasema sehemu ya
barua ya North Mara Community Trust Fund ikinukuu maelezo ya barua ya Mkuu
wa Wilaya ya Tarime.
Baada ya maombi ya fedha kuridhiwa, Luoga alishukuru uongozi wa mgodi: “Kwa
furaha, natoa shukrani zetu kwa msaada uliotupatia na nia uliyoonesha ya
kushiriki katika mradi huu, kama ambavyo tulikutaka uwe sehemu ya mradi huu
kwa manufaa ya jamii.
“Kutokana na kukutambua kama mmoja wa wadau wakuu wa maendeleo ndani ya
wilaya hii (ya Tarime), imekubaliwa kutenga hekta 800 kwa ajili ya kilimo na hekta
40 kwa ajili ya uwekezaji wa miundombinu kwenye kijiji ambapo kiwanda
kitajengwa.
“Mazungumzo yatafanyika na mwekezaji, kuhakikisha wewe unapewa kipaumbele
punde mradi utakapoanza. Zaidi ya hayo, tunayo furaha ya kukutaarifu kwamba,
wazo lako la kushiriki kwenye huu mradi tayari limewasilishwa kwa viongozi wa
vijiji na kukubaliwa moja kwa moja.”
Kwa mujibu wa DC Luoga, fedha hizo aliziomba ili kufanikisha mambo yafuatayo:
1: Gharama za utambuzi na uhakiki wa mipaka ya vijiji vyote vinavyohusika
kwenye mradi wa kilimo cha miwa.
2: Kugharimia ziara za viongozi na wataalamu kutembelea viwanda vya
sukari na maeneo yanayolimwa miwa, kwa lengo la kujifunza na kujionea
jinsi kilimo hiki kinavyoendeshwa.
3: Kugharimia mafunzo kwa kamati ya usimamizi na wataalamu juu ya
uwekezaji katika kilimo cha miwa.
4: Ununuzi wa matrekta mawili na vifaa vyake.
5: Kununua gari kwa ajili ya kusimamia na kufuatilia
shughuli za mradi.
6: Usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za mradi kwa mwaka mzima.
7: Kugharimia tathmini za athari za kimazingira (Environmental Impact
Assessments-EIA).
(8) Kugharimia mpango wa matumizi bora ya ardhi katika vijiji
vinavyohusika kwenye mradi.
(9) Uchoraji wa ramani za msingi.
(10) Ununuzi wa mbegu na usafirishaji wake.
(11) Usanifu na ujenzi wa bwawa kwa ajili ya kilimo, mifugo, maji kwa binadamu
na ufugaji samaki.
(12) Kugharimia miundombinu ya barabara katika maeneo ya mradi.
(13) Kushiriki kuanzisha na kulinda mashamba ya miwa yatakayomilikiwa na
mfuko wa dhamana.
Hisa 30,000 zitamilikiwa na Nile Agro Industries Ltd, hisa 10,000 zitamilikiwa na
CMG Investment Ltd, na hisa nyingine 10,000 zitakuwa chini ya Pravin Shah wa
jijini Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Dk. Peter Nyanja,
anasema kiwanda hicho kitazalisha sukari kwa mita za ujazo wa tani 450 kwa
siku. Pia kitazalisha pombe kali lita 50,000 kwa siku na mtambo wa kuzalisha
umeme megawati 20.
DC Luoga amezungumza na JAMHURI, lakini amekataa kuingia kwenye undani
wa suala hilo.
“Najua unataka kuniuliza suala lilelile (tuhuma za kupewa fedha) lililozungumzwa
kwenye kikao cha CCM. Mimi siwezi kulizungumzia, maana itapelekea
(itasababisha) niitwe na kuulizwa na RC (Mkuu wa Mkoa).
“Mambo yaliyozungumzwa na CCM siwezi kuyazungumzia. Viongozi wa chama
wanafahamu utaratibu wa kumuuliza kiongozi wa Serikali. Sijui lilikoibukia jambo
hili.
“Kwa hiyo siwezi kuzungumzia suala hilo. Nakushukuru sana kunipigia simu
kuniuliza,” alisema.
Hata hivyo, JAMHURI limefanikiwa kupata maelezo ya video ya DC Luoga, akijibu
tuhuma zinazoelekezwa kwake za kupokea Sh milioni 214, lakini pia na kiasi
kingine cha Sh bilioni 1.
Amesema, “North Mara Trust Fund nimeambiwa nimekopeshwa bilioni moja.
Ningekopeshwa hiyo mimi nina biashara gani ya kusimamia mpaka nikope bilioni
moja?
“Naomba niwaambieni, tusiwe watu sasa wa kuendeshwa kisiasa kisiasa na
majungu majungu kwenye jamii zetu. Mimi leo ningekuwa na bilioni moja
ningesimama na nyie hapa saa hizi. Nina bilioni moja! Kinachozungumzwa
haukijui; uliza. Sasa leo naomba niutumie mkutano huu kuwapeni faida. Faida
kubwa kweli kweli. Kubwa kweli kweli. Sisi tumeanzisha mradi wa kilimo cha miwa
kikiwamo kiwanda cha sukari Tarime. Na sasa hivi tunapozungumza wizara zote
zinaulizia hapa, hapa, hapa.
“Kilimo, Wizara ya Ardhi wanapiga simu lete documents. Hawa wanapiga simu,
siku si nyingi Rais atasaini. Mashine zimeshafika. Yaani tunasubiri tu Rais afanye
hivi, uhaulishaji ufanye nini, uishe…tulipoanza wazo hili hatukuwa na bajeti
yoyote. Land use plan tuliifanya kwa kutumia fedha za halmashauri milioni 80.
Halmashauri ilitoa milioni 80.
“Tukapeleka wataalamu wakafanya land use plan vijiji vyote, wakamaliza. Sasa, ili
uweze ku-establish [kuanzisha] mashamba hayo kuna kitu kinaitwa…kiswahili
chake sikijui, watu wa ardhi watusaidie. Land use plan maana yake matumizi bora
ya ardhi. Kwa hiyo, sisi ili tufanye uwekezaji lazima tufanye haya mawili. Land use
plan, vijiji vingapi mmefanya…vinne. Land use plan wastani wa kila kijiji Sh milioni
20. Na hizo hela ni posho wanalipwa wale wenyeviti wa vijiji, wanaokwenda huko
saiti. Hao wataalamu wakaniandikia bajeti ya milioni 214.
“Wakaniletea nikawaambia hizi hela tutazitoa wapi? Nani atu-finance pesa hizi.
Sasa uongozi ni kujiongeza si ndiyo? Mimi nikaenda Acacia, wakati huo Meneja
Mawasiliano alikuwa Sanga. Nikawafuata Acacia nikawaambia mnaweza
kutusaidia hii? Wakasema North Mara Trust Fund kuna pesa, na pesa zao
zinapaswa zifanye kazi kama hizi. Nikaandika maombi, nikayapeleka North Mara
Trust Fund kwenye bodi. Wakaniita kwenye bodi yao. Nikaenda pale
nikaelezeaaa, presentation ile kila kitu, wakasema tupe muda. Wakajadiliana,
wakamuita mwanasheria wao. Wakajadiliana, wakaniandikia barua. Wakasema,
‘ili sisi tufanye hili jambo, tunahitaji na sisi tupewe ekari ekari 800 na sisi tulime
miwa. Tunahitaji utu-guarantee kwamba huyo mwekezaji akihitaji kujenga nyumba
za watumishi, tenda hiyo yaani tuseme siyo tenda, hatajenga nyumba za
watumishi baadhi ya maeneo. Atatuachia sisi tujenge ili watumishi wake wapange,
kwa sababu pia North Mara Trust Fund inaruhusiwa kufanya biashara’ Umeelewa!
“Wakaniambia, huyo mwekezaji akija na yeye akumbuke kuichangia North Mara
Trust Fund asilimia moja ya mapato yake, kama leo tunapopata hizi ambazo
wewe umekuja kufanya nini, kuziomba. Mimi nika-share na wale, wakaniambia
hakuna shida. Nikawajibu kwa barua ‘wamesema hakuna shida’. Kwa hiyo, wale
hawajatupa hela, wamewekeza hela. Wakatupatia pesa, electronic transfer.
Wakaanza kuwaza hizi hela tutazipokelea wapi. Kazi hii wanafanya hawa
wataalamu. Walikuja wataalamu kutoka wizarani.
“Wataalamu wote waliokuja hapa wakiwamo wa Uganda. Na wote tumewalipa
sisi. Haya, sasa hawa wamekaa hapa miezi miwili na nusu hadi mitatu,
wakishirikiana na vijiji. Na ndiyo pesa hiyo ilitumika na tukamaliza. Baada ya
kumaliza, wale wataalamu wa Wizara ya Ardhi wakaondoka na
zile documents wakapeleka wizarani. Mkurugenzi wa Ramani amepitisha,
maramani yamekuja pale, sasa tukawa tumeshapima ardhi yetu. Hiyo ndiyo hela
pekee waliyotoa North Mara Trust Fund kwa ajili ya kusaidia maendeleo na
Serikali. Kuna swali jingine? (kimya). Hiyo bilioni moja ya kwako wewe na baba
yako.
“Na ninawapongeza North Mara Trust Fund kwa maamuzi yale. Hiyo ni sehemu
ya shughuli ya jamii. Na leo tunafanya upimaji wa Nyamongo. Kesho tunaweza
kuwaomba North Mara Trust Fund wasimamie kazi ya uwekaji umeme wa
Nyamongo wote uwe na umeme. Sasa haya mambo ya siasa siasa sijui nani
kalonga tatizo, nani ana ugomvi na fulani, nani amefanya nini. Kwanza
tunawapotosha wananchi. Nafikiri tutafanya vitu ambavyo havipo.
“Nimeamua niwaeleze mjue na documents zipo na kazi imefanyika. Na wewe
bwana mara ya mwisho tumekutuma Mwanza…Ulikwenda Mwanza kwa ajili ya
kuwasiliana na wawezeshaji. Na hizi taarifa zote, Waziri Mkuu anazo, Makamu wa
Rais anazo sababu wote walikuja hapa. Zote wanazo. Na pale kila kitu
kimeshafanyika. Yaani sasa hivi katika mradi wa kilimo cha miwa tunasubiri saini
tu ya Rais ambaye kwa sababu Sera ya Viwanda ni ya kwake, tuna uhakika
hatachelewa kuweka saini. Na kama mnakumbuka alipokuja Makamu wa Rais
nilimwambia hata ule muda wa kuhaulisha ardhi upunguzwe. Na kwenye barua
yetu pia tumeandika vivyo hivyo.”
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Malima, kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM
Mkoa wa Mara wiki iliyopita alisema mradi aliukataa kwa ule mpango wake wa
awali.
Alisema sababu za kuukataa unatokana na Wilaya ya Tarime kuwa na eneo la
ekari 800 pekee linalofaa kwa kilimo hicho.
“Mradi huu ilibidi nimuulize mkuu mmiliki wa ardhi (Rais Dk. John Magufuli).
Akaniuliza ‘unasemaje (RC Malima)’. Nikamwambia ‘hapana, tuuweke huu mradi
uwe na sura ya Mkoa wa Mara – Mara Sugar badala ya Tarime Sugar’.
“Kwa hiyo, tumechukua ardhi ya Wilaya ya Serengeti ambayo ni kubwa, Wilaya ya
Tarime na Rorya. Jumla mradi utakuwa na ekari 30,000 badala ya ekari 800 za
Tarime,” alisema Malima.