TANZIA: Beki wa kati(Sentahafu) wa zamani wa Klabu ya Yanga na Timu ya Taifa(Taifa Stars), Athuman Juma Chama maarufu kama Jogoo amefariki asubuhi ya leo,

Mchazaji huyo amefariki katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa presha na kupooza

=====

Athuman Chama Jogoo ni nani?

Alianza kucheza soka akiwa mdogo, mwenyewe anasema alipenda kucheza namba mbili na namba nne tangu akiwa na umri mdogo.

Akiwa mtoto wa kwanza kati ya watano kwenye familia yao, Chama alichezea timu mbalimbali kabla ya kujiunga na Pamba United ya Mwanza.

“Hii ilikuwa ni timu ya mkoa nilikozaliwa na kukulia huko, ninakumbuka siku moja tulikuwa na mechi, baada ya ile mechi aliyekuwa Katibu wa Yanga wakati huo, Issa Makongoro alinifuata na kunishawishi nikacheze Yanga.

“Kiukweli, nilikuwa shabiki mkubwa wa Yanga, Makongoro aliponifuata sikutaka kujivunga, nilikubali moja kwa moja kujiunga na klabu hiyo, ndipo mwaka 1981 nilisajiliwa rasmi Yanga, lakini si kwa fedha bali mapenzi niliyokuwa nayo dhidi ya timu hiyo,” anasimulia.

Akizungumza kwa taratibu, Chama anasema alicheza Yanga kwa miaka zaidi ya 10 lakini wakati huo walicheza kwa mapenzi zaidi na walicheza kwa moyo ikilinganisha na wachezaji wa sasa.

Kikosi cha kwanza cha Yanga waliocheza na Chama miaka ya 1983 na 1985 ni; Joseph Fungo, Yusuf Bana, Ahmed Amasha ‘Mathematician’, Athumani Juma Chama ‘Jogoo’, Isihaka Hassan Chuku, Juma Mukambi ‘Jenerali’, Hussein Iddi, Charles Boniface Mkwasa, Abeid Mziba ‘JJ Masiga’, Elisha John na Ali Mchumila.

Pia walikuwepo; Makumbi Juma ‘Homa ya jiji’, Omari Hussein ‘Keegan’, Juma Kampala na wengine wengi.

Apachikwa jina la Jogoo

Wakati wa michuano ya Kombe la Chalenji mwaka 1981, kulikuwa na mchezaji mmoja wa Harambee Stars ya Kenya, Sammy Onyango ‘Jogoo’. Alikuwa makini sana katika ngome.

Alikuwa na uwezo wa kukabiliana na washambuliaji mbalimbali hasa katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Baada ya mashindano yale ya 1981 ambayo pia kulikuwa na mtu aliyekuwa akiitwa Ambroce Ayoi ‘Golden Boy’ wengi waliufananisha uwezo wa Sammy Onyango na Athumani Juma Chama na taratibu jina likafika kwa mwenyewe.

“Nilipewa na mashabiki hili jina ninajua kutokana na umahiri wangu wa kukaba. Si unajua jogoo anavyokaba (anatabasamu).

“Nilipolisikia kwanza nililikubali lakini sikuishia hapo, niliwafuata baadhi ya mashabiki na wanachama na kuwauliza, kwanini wameniita Jogoo. Wakaniambia majina yote wanayoyafikiria kunipa hayatoshi, lakini Jogoo ndilo linalonifaa kutokana na uhodari wangu wa kucheza soka, nililiridhia jina hilo na kiukweli nililipenda.

Chama na Mogella

Chama na Mogella…..Chama na Mogella. hii ni kumbukumbu ambayo Chama ameiacha kwenye soka la Tanzania wakiwazungumzia, aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, Zamoyoni Mogella na beki huyo wa Yanga (Chama).

Itakumbukwa Yanga walitishika na soka ya Mogella katika moja ya mechi za watani, ndipo waliamua kumwekea ulinzi mkali, wa Athumani Juma Chama ambaye aliambiwa popote anapokwenda Mogella awe naye.

Chama alifanya kazi yake, basi ikawa kazi moja, Chama na Mogella kiasi cha Mogella kuumia na kufanyiwa huduma ya kwanza, Mogella alifunga bandeji mfano wa ‘lumundi’ kichwani na kurudi uwanjani, hata hivyo Mogella hakutikisa nyavu siku hiyo.

“Namkumbuka sana Zamoyoni Mogella, sijui huyu rafiki yangu huyu kwa sasa yuko wapi?,” anasema huku akionyesha tabasamu hafifu na kuendelea.

Anasema: “Sijisifu lakini nilikuwa beki kisiki, hakuna mshambuliaji aliyekuwa akipita kwangu, Mogella mwenyewe ambaye alikuwa mshambuliaji mashuhuri wa Simba, kwangu hakufua dafu, kazi yangu likuwa moja tu ‘kum block’ asipite na kweli nilimdhibiti.

Hata hivyo, Chama anasema: “Nilicheza mpira na sikuwahi kumtoa kovu Mogella, mimi nilikuwa nikicheza mpira bhana.”

Spoti Mikiki iliwahi kuzungumza na Zamoyoni Mogella ambaye alisema ingawa wengi wanajua Chama ndiye pekee aliyekuwa akimpa wakati mgumu Mogella uwanjani hasa mechi ya Simba na Yanga, lakini mwenyewe aliwataja pia Yusuf Ismail Bana, Allan Shomari na Isihaka Hassan Chuku kwamba nao walikuwa wakimuumiza kichwa

Maisha baada ya soka

Chama anasema, alistaafu soka mwaka 1990 baada ya kuitumikia Yanga kwa miaka 10.

Anasema baada ya kustaafu aliendelea kufanya biashara zake ndogo ndogo kabla ya kuugua mwaka 2014 na kushindwa kufanya chochote hadi sasa.

Alivyoanza kuumwa

“Ninakumbuka ilikuwa ni Oktoba 2014, nikiwa katika mihangaiko yangu ya maisha, nilianguka barabarani, nikapewa msaada wa kupelekwa Hospitali ya Temeke na wasamaria wema, baada ya vipimo, niliambiwa nina presha na stroke,” anasema Chama ambaye anahitajika umakini wa hali ya juu na utulivu ili kumuelewa kutokana na namna anavyozungumza kwa taabu.

Anasema ugonjwa huo ulisababisha kushindwa kutembea, mdomo kwenda upande na kushindwa kuongea, maisha yake yakabaki kuwa ya hospitali na yeye, yeye na hospitali kwa siku 700.

“Nilikuwa mtu wa kubebwa na kufanyiwa kila kitu, ndiyo maana kauli yangu ya kwanza nilikwambia mwanangu mwache Mungu aitwe Mungu, ilifikia mahali nikazushiwa nimefariki na baadhi ya vyombo vya habari (sio Mwananchi) vikaripoti nimekufa.

“Watu walijaa nyumbani kwangu wakiamini nimefariki, familia ilipata wakati mgumu mno, lakini namshukuru Mungu kwa hatua niliyofikia, kwa ushirikiano wa wanafamilia ambao walichangishana ili kuhakikisha afya yangu inaimarika japo si kwa vile ambavyo inatakiwa,” anasema.

Ugonjwa wa kupooza

Dk Samwel Shita anasema ugonjwa huo una vyanzo vingi lakini mara nyingi huwapata watu ambao wana mafuta mabaya mwilini.

“Mara nyingi shinikizo la damu, sukari au unene uliopitiliza vinachangia kuharibika kwa mishipa ya damu. “Hali hii inachangia mishipa ya damu kufunga, ubongo unakosa hewa na kusababisha kiharusi ambacho husababishwa na mishipa ya damu ya ubongo kuziba,” anasema Dk Shita ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya afya kwenye gazeti hili.

Anavyowaona mabeki wa sasa

“Kwa sasa sioni beki kabisa, watoto wanachezacheza tu na kuangalia fedha wanacheza soka ya shule sio profeshno…enzi zetu kulikuwa na vipaji vya mpira kweli kweli, lakini si sasa,” anasisitiza kwa ishara ya kugonga mkono licha ya sauti yake kuonekana kufifia kutokana na kuzungumza muda mrefu na kwa tabu.

Chama anawataka wachezaji wa Tanzania kuonyesha kuwa wanaheshimika kwa kucheza kwa nguvu, kujituma na kuonyesha kuwa kweli wanafikra za kufika mbali.

Hali ya Chama

Waliomshuhudia Chama enzi zake, ni wazi wanamtambua uwezo wake uwanjani wakati huo akiitumikia Yanga na Taifa Stars.

Wakati ninajiandaa kuondoka nyumbani kwa Chama baada ya mazungumzo na mahojiano mafupi, niliingiwa na hofu juu ya hali yake na kujikuta nikipata kigugumizi wakati wa kuaga ili nipate kuondoka.

Chama anayeonekana mtu mcheshi lakini hali ya ugonjwa imemrudisha nyuma, alijitahidi kuonyesha tabasamu hafifu na kuzidi kuzungumza kwa tabu akisema: “Hatua niliyofikia ninajiona nimepona ukilinganisha na nilikotoka.

“Mbali na Mungu na madaktari, ninaishukuru familia yangu kwa hatua hii, ilijichangisha na inaendelea kufanya hivyo ili nipate matibabu.

“Ninaendelea na dozi yangu, ninaamini kwa uwezo wa Mungu nitaimarika na kurejea kwenye uzima kama ilivyokuwa zamani,” anaongeza Chama.

Mogella amzungumzia Chama

Akimzungumzia Chama, mshambuliaji wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella anasema enzi wakicheza soka, beki huyo alikuwa kisiki.

“Nikiwa Simba, yeye akiwa Yanga, tuliweka rekodi, Chama alikuwa beki mwenye kipaji, anajua nini anachokifanya lakini pia naweza kusema alikuwa msaada mkubwa Yanga na Taifa Stars,” anasema Mogella na kuongeza.

“Kwa kipaji cha Chama, kama ndiyo angekuwa akicheza soka hivi sasa, naamini angekuwa mchezaji mkubwa Ulaya, sema zamani tulicheza kwa mapenzi, hakukuwa na fedha kama sasa, kuna watu wanadai Chama alinipa wakati mgumu.

Huku akicheka Mogella anaendelea: “Yeye mwenyewe alikuwa akinihofia, uwezo wangu uwanjani ulikuwa ukimfanyisha mazoezi ya ziada ili amudu kasi yangu nikiwa Golden Boy wa Simba na Taifa Stars, nilipenda kucheza na Chama timu ya taifa,” anamaliza Mogella.

Aidha Mogella hakuacha kutoa pole kwa Chama na familia yake kwa maradhi yanayomkabili na kumtaka kumtumai Mwenyezi Mungu kipindi chote pamoja na kutaka wachezaji kusaidiana katika shida na raha.