Kocha wa zamani wa Yanga, Jack ‘Africa’ Chamangwana amefariki dunia jana jioni Mei 6, 2018 baada ya kuugua ghafla na kulazwa katika Hospitali ya Malkia Elizabeth jijini Blantyre.

Kocha huyo aliyefariki akiwa na umri wa miaka 61 ameripotiwa kuwa alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu.

Chamangwana aliyeifundisha Yanga mwanzoni mwa miaka ya 2000, alikuwa pia nyota wa zamani wa timu ya taifa ya Malawi.

Mtalaam huyo alikuwa akifanya kazi na klabu ya Be Forward Wonderers inayoshiriki ligi kuu ya Malawi kama Mkurugenzi wa Ufundi.

Jack aliichezea timu ya taifa ya Malawi kwa mara ya kwanza mwaka 1975 akiwa na umri wa miaka 18, kwenye mechi dhidi ya Kenya jijini Lilongwe. Pia aliiongoza Malawi kutwaa ubingwa wa Kombe la Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) mwaka 1978/79.