Kampuni ya TanzaniteOne Ltd inayochimba madini ya tanzanite katika eneo la Mererani mkoani Manyara, inaendelea kuchimba madini hayo licha ya leseni iliyoiruhusu kufanya kazi hiyo kwisha muda wake, JAMHURI imeelezwa.
Kampuni hiyo kutoka Afrika Kusini, inamiliki mgodi huo kwa asilimia 100; ikiwa inakinzana na Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 inayotaka madini ya vito yasichimbwe kwa asilimia 100 na wageni.
Habari za uhakika zilizopatikana zinaonesha kuwa TanzaniteOne ilitakiwa iwe imesitisha shughuli zake tangu Julai, mwaka huu; mwezi ambao leseni yake ilikuwa inamaliza muda wake.
Kampuni hiyo imekuwa ikichimba tanzanite kwa miaka zaidi ya 15 sasa; ikiwa imepata eneo hilo katika kile kinachoaminiwa na wachimbaji wadogo wengi kuwa ni mizengwe.
Hata hivyo, katika kile kinachoonekana kuwa ni ushawishi na kubebwa na baadhi ya wanasiasa waliojiingiza kwenye biashara, kampuni hiyo imeendelea kuchimba madini ikiwa haioneshi dalili zozote za kuondoka.
Mwaka jana, TanzaniteOne iliandika barua kwa Wizara ya Nishati na Madini ikiomba iendelee kuchimba madini hayo yenye thamani kubwa. Hata hivyo, haikujibiwa. Lakini habari za uhakika zilizopatikana baadaye zilisema kuwa mipango ilikuwa ikisukwa kwa kuwahusisha baadhi ya viongozi waandamizi serikalini pamoja na familia zao, ikiwa ni pamoja na kuwapa hisa ili kampuni hiyo iendelee kuchimba tanzanite.
TanzaniteOne imekuwa ikipambana na misukosuko mingi kutoka kwa wachimba tanzanite wazalendo, lakini mara zote imeshinda changamoto zote.
Kampuni hiyo inabebwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Balozi Ammy Mpungwe, ambaye ni Mtanzania. Balozi Mpungwe ndiye aliyeikaribisha kampuni hiyo kuja kuwekeza hapa nchini, wakati huo akiwa Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini.
Habari zilizopatikana zinasema kwamba Serikali imewapa masharti mapya TanzaniteOne endapo wanataka kuendelea kuchimba madini hayo. Masharti hayo ni kuhakikisha kuwa asilimia 50 ya hisa inamilikiwa na Watanzania.
TanzaniteOne wanasita kulikubali jambo hilo moja kwa moja, kutokana na ukweli kwamba kwa miaka yote ni wao pekee waliofaidi utajiri huo na kujinasibu duniani kote kwamba ndiyo wachimbaji na wauza tanzanite halali.
Mwenyekiti wa Chama cha Wauzaji Madini ya Vito Tanzania (TAMIDA), Sammy Mollel, anasema, “Tumesubiri kwa muda mrefu sana, sasa muda umefika wa Serikali kutimiza ahadi yake ili eneo hilo ligawanywe kwa wachimbaji wadogo nao wajikomboe kiuchumi, baada ya kukandamizwa kwa muda mrefu na mfumo wa uchimbaji usio na uwiano sawa.”
Mollel ameongeza kusema, “Hawa jamaa hawataki kuondoka, Serikali haijawaongezea muda, lakini wanaendelea kuchimba na kusafirisha. Hii ni kinyume cha sheria…ni uhuni. Hatuamini kama wameiweka Serikali mfukoni, hawawezi hawa. Kwa sasa tuna uongozi imara sana katika Wizara ya Niashati na Madini, matarajio yetu ni kuona hawa wanaondoka.
“Rais alitoa ahadi ya wazawa kumiliki tanzanite hii mbele ya hadhara na pia muda umefika sasa wa Serikali kuwawezesha wazawa badala kuwakumbatia wageni ambao wamekuwa wanamaliza rasilimali zetu.”
Soko la hisa
Habari zilizopatikana zinasema kwamba TanzaniteOne wanajiandaa kuanza kuuza hisa zao kwenye Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE). Mmoja wa viongozi wa kampuni hiyo aliyezungumza kwa masharti ya kutotajwa jina, aliiambia JAMHURI kuwa kwa utaratibu huo, hata wafanyakazi wa kampuni hiyo wataweza kununua hisa. Kwa sasa kampuni hiyo ina wafanyakazi 680.
Hata hivyo, kundi la baadhi ya viongozi wa kisiasa limeungana na baadhi ya wafanyabiashara wakubwa wa tanzanite, kutwaa mgodi huo.
Msingi wa hujuma hiyo unaelezwa kuwa ni ahadi ya Rais Jakaya Kikwete wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kikwete aliwaahidi wachimbaji wadogo kuwamegea eneo la mgodi huo baada ya TanzaniteOne Ltd kumaliza mkataba wake. Aliitoa ahadi hiyo akiwa Kijiji cha Lengast wilayani Simanjiro.
TanzaniteOne yaendelea kujiimarisha
Kampuni hiyo imeendelea kujenga nyumba mpya za wafanyakazi, maghala na kuajiri wafanyakazi, hatua iliyotafsiriwa kuwa ni uhakika wa kuendelea kuwapo kwenye eneo hilo la Kitalu ‘C’.
Kampuni hiyo imekuwa ikibadili majina yake mara kwa mara, ikiwa ilianza kwa kuitwa SAMAX, AFGEM kabla ya jina la sasa la TanzaniteOne.
Imekuwa kwenye mivutano mikali na wachimbaji wadogo kutokana na mitobozano ya mara kwa mara. Hivi karibuni walinzi wake waliwajeruhi kwa risasi za moto wachimbaji wadogo watano katika mapambano yaliyotokea chini ya ardhi.
Wachimbaji wadogo wamekuwa wakilalamika kwamba wanaonewa na kampuni hiyo, na wakati mwingine wenzao wameuawa na hata kung’atwa na mbwa wa kampuni hiyo.
Wachimbaji wadogo wamekuwa wakiendesha shughuli zao katika vitalu A, B, D na eneo la Karro ambalo hata hivyo, si maarufu kwa uzalishaji tanzanite.
Serikali iliwaahidi wachimbaji wadogo tangu mwaka 1995 kwa nyakati tofauti kuwa watapewa eneo la kitalu C.
Vigogo wajipanga
Kuna shinikizo kutoka kwa baadhi ya wamiliki wa migodi walioungana na baadhi ya wanasiasa, ili kuhodhi kitalu C endapo TanzaniteOne wataondoka.
Mapema mwaka huu, gazeti moja liliandika kuhusu jambo hilo na kusema, “Tayari wako katika mipango ya kuanzisha kampuni itakayoomba leseni ya kuchimba eneo la kitalu C, baada ya wawekezaji kutoka Afrika Kusini kuondoka. Kigezo chao ni kwamba, kampuni hiyo ni ya wazawa hivyo wana haki ya kupewa leseni kwa mujibu wa sheria za sasa.”
Balozi Mpungwe hakupatikana kuzungumzia hatima ya kuwapo kwa TanzaniteOne katika eneo hilo. Muda wote simu yake ya mkononi ilipopigwa kulitolewa maelekezo ya kuacha ujumbe. Pamoja na kuacha ujumbe, hadi tunakwenda mitamboni hakuweza kuzungumza na JAMHURI.
Pia Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, simu yake ya mkononi haikupokewa kwa siku mbili alizotafutwa. Hali kama hiyo ilikuwa pia kwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa TanzaniteOne, Bernad Oliver.
Madini ya tanzanite yaligunduliwa mwaka 1968 na mkazi wa Makanya wilayani Same, Jumanne Ngoma; na Serikali ilimkabidhi cheti cha kumtambua kwa ugunduzi huo. Hata hivyo, kuna madai mengine kwamba mgunduzi ni Ali Juuyawatu.
Miaka zaidi ya 40 sasa tangu madini hayo yagunduliwe, Mererani imetambuliwa kuwa ndipo mahali pekee duniani yanakopatikana madini hayo.
Pamoja na kuzalishwa Tanzania, Kenya na Afrika Kusini ndizo nchi zinazotambulika kuwa wauzaji wakuu wa madini hayo. Mji wa Jaipur nchini India ndiko madini hayo yanakochongwa. Watu milioni moja wanafaidika na ajira hiyo ya tanzanite katika mji huo.
Tanzania ilipotangaza kupiga marufuku usafirishaji tanzanite ghafi nje ya nchi, India ilituma ujumbe mzito kuja kuibembeleza Serikali ya Tanzania kuacha mpango huo. Lengo la India lilikuwa kulinda ajira za wananchi wake ambao wangeathiriwa na msimamo wa Tanzania.