Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zambia zimekubaliana kuimarisha mifumo ya utendaji kazi ili kumaliza changamoto ya migomo ya madereva katika mpaka wa Tunduma – Nakonde unaozitenganisha nchi hizo mbili.

Makubaliano hayo yamefikiwa leo tarehe 14 Oktoba 2022 katika Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia katika Ngazi ya Mawaziri uliofanyika jijini Lusaka, Zambia.

Tanzania, Zambia zakubaliana kumaliza migomo ya madereva mpakani
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Dkt. Stergomena Tax akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu ya Ushirikiano kati ya Tanzania na Zambia Ngazi ya Mawaziri unaofanyika tarehe 14 na 15 jijini Lusaka, Zambia.

Akifungua mkutano huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,Dkt. Stergomena L. Tax ameeleza dhamira ya wazi ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuendelea kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Jamhuri ya Zambia kwa kufanya maboresho na usimamizi wa karibu katika sekta za kiuchumi baina ya nchi hizo mbili.

“Tunatakiwa kuchukua hatua na kuweka mazingira wezeshi kwa sekta za umma na binafsi ili kurahisisha shughuli za biashara na usafirishaji ili kuinua uchumi wa nchi zetu; kuboresha utendaji wa kampuni ya reli ya TAZARA na kuboresha mtandao wa barabara kati ya Tanzania na Zambia ili kuifanya Kapiri Mposhi kuwa kitovu cha usafirishaji wa mizigo nchini Zambia kwa kushirikiana na Bandari ya Dar es Salaam (TPA).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia, Mhe. Stanley Kakubo akihutubia wakati wa ufunguzi wa Mkutano wa Kumi wa Tume ya Pamoja ya Kudumu kati ya Tanzania na Zambia Ngazi ya Mawaziri unaofanyika tarehe 14 na 15 Oktoba 2022 jijini Lusaka, Zambia.

Aidha,Tax ameeleza umuhimu wa kuwa na mikakati ya pamoja na ya kudumu ya kutatua migomo ya madereva mpakani; kuimarisha utendaji kazi katika kituo cha pamoja cha mpakani Tunduma/Nakonde (OSBP) kwa kukiwezesha kituo hicho kuwa na huduma bora na rafiki kwa usafirishaji wa mizigo pamoja na abiria; kufufua mradi wa bomba la mafuta la TAZAMA ambapo mradi huo utaenda sambamba na mradi wa kuunganisha umeme wa nchi za Tanzania na Zambia (TAZA).

Kwa upande wa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Zambia,Stanley Kakubo alieleza kuwa Serikali ya Zambia inathamini ushirikiano uliopo baina ya Zambia na Tanzania ambao umewezesha Marais wa nchi zote mbili kukutana jijini Dar es Salaam na kupelekea kutoa maelekezo ya kufanyika kwa mkutano huo unaojadili na kutoa maamuzi ya utekelezaji wa maazimio ya Mkutano wa Tisa wa Tume ya Pamoja ya Kudumu Kati ya Tanzania na Zambia uliofanyika mwaka 2016.

Picha ya pamoja Mawaziri, Makatibu Wakuu na Viongozi Waandamizi kutoka Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Zambia.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu umeongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax ambaye ameambatana na Waziri wa Uwekezaji, Biashara na Viwanda, Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Bw. Atupele Mwakibete, Makatibu na Naibu Makatibu Wakuu na Maafisa Waandamizi kutoka katika Wizara, Idara na Taasisi za Serikali.