Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Wakala wa Nishati Vijijini (REA),hadi sasa umetumia takribani Shilingi trilioni 3 kwa ajili ya kazi ya kupeleka miradi ya umeme vijijini ili kuhakikisha nishati ya umeme inafika na kutumika kwa ajili ya matumizi mbalimbali ikiwemo ya uzalishaji, kuboresha huduma na shughuli za kiuchumi.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi Mkuu wa REA Mhandisi Hassan Saidy wakati wa mkutano wa Wakala huo na wadau wake kuelezea masuala mbalimbali ya nishati vijijini uliorushwa mubashara na kituo cha televisheni cha Azam ambapo amesisitiza kuwa mradi unaoendelea hivi sasa (mradi wa usambazaji umeme vijijini awamu ya tatu mzunguko wa pili) pekee unagharimu kiasi cha shilingi trilioni 1.2.

Mhandisi Saidy ameongeza kuwa, kutokana na kazi zinazoendelea na mipango waliyoijiwekea, vijiji vyote nchini vitapata umeme kabla ya muda ulioelekezwa (mwaka 2025).

“Ilani ya Uchaguzi ya CCM imeahidi kufikisha umeme katika vijiji vyote ifikapo mwaka 2025, sisi kama REA hatutafika huko, tutakamilisha vijiji vyote kuvipatia umeme kabla ya mwaka huo” alisema Mhandisi Saidy na kuongeza kuwa

“Wananchi wakipata nishati ya umeme itasaidia sana katika uhifadhi wa mazingira, kwani hivi sasa zaidi ya asilimia 90 ya Watanzania wanatumia kuni na mkaa jambo ambalo linapelekea kuathiri mazingira kwa kuharibu misitu. Takwimu zinaeleza kuwa kwa mwaka mmoja, Tanzania inapoteza hekta 400 za misitu”

Ameendelea kwa kusema kuwa, REA inatumia gharama kubwa kupeleka miradi ya umeme vijijini hivyo amewataka wananchi wa vijijini kuchangamkia fursa hiyo kwa kuutumia kwa shughuli za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Sera, Mipango na Utafiti wa REA , Mhandisi Elineema Mkumbo, amesema hali ya upatikanaji wa umeme vijijini imepanda kutoka asilimia 2 mwaka 2007 hadi kufikia asilimia 69.6 kufikia mwaka 2020. “Lengo letu ni kuhakikisha vijiji na vitongoji vyote nchini vinapata umeme nyumba kwa nyumba.

Mhandisi Mkumbo ameeleza kuwa, kazi ya kupeleka umeme vijijini inaenda sambamba na kupeleka umeme katika vitongoji ambapo hadi sasa zaidi ya vitongoji 27,000 vimepatiwa umeme.

Naye Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi wa REA, Mhandisi Jones Olotu ameeleza kwamba, kufuatia kasi ya upelekaji miradi ya umeme vijijini na nishati hiyo kuwafikia wananchi wengi wa vijijini, Tanzania imeweka rekodi na kuongoza katika nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambao wananchi wake wamepunguza kuhama kutoka vijijini kwenda mijini na badala yake watu mijini kuhamia vijijini kwa ajili ya kufanya shughuli mbalimbali.

“Tanzania imekuwa nchi ya kwanza kwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwa kubadilisha mtazamo wa watu kuhama kutoka vijijini kuja mjini, siku hizi ni kawaida kabisa watu wanahama kutoka mjini na kuhamia vijijini” alisema Mhandisi Olotu.

Mhandisi Olotu amebainisha kwamba, matokeo ya kasi ya upatikanaji umeme vijijini hivi sasa ni matokeo ya REA kuandaa mipango kabambe na mikubwa ukiwemo mpango mkubwa wa miaka mitano wa kupeleka umeme katika vijiji vyote nchini ambao REA inaendelea kuutekeleza huku vipaumbele vikiwa ni taasisi za umma ikiwemo zahanati, shule, vituo vya maji, polisi, nyumba za ibada kwa lengo la kuboresha huduma za jamii.

Akichangia katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Uendelezaji Masoko na Teknolojia wa REA, Mhandisi Advera Mwijage amesema, kazi ya REA syo tu kupeleka umeme vijijini bali ni kupeleka nishati mbalimbali vijijini ili ziweze kutumika na wananchi wa maeneo hayo katika shughuli mbalimbali ambapo katika kusambaza gesi asilia kwa ajili ya matumizi ya majumbani wanashirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kazi hiyo wanaifanya katika mikoa ya Lindi, Mtwara na Pwani.

Mhandisi Mwijage ameongeza kuwa, katika maeneo ya visiwa, REA imekuwa ikitumia nishati ya jua katika kupeleka miradi ya umeme ili kuhakikisha visiwa vyote nchini vinapata nishati hiyo ambapo kwa sasa mpango uliopo ni kuvipelekea umeme visiwa 36.

“Tanzania tuna visiwa 196, visiwa 53 havina makazi ya kudumu, vyenye makazi ya kudumu ni 143. Kati ya visiwa 143 vyenye makazi ya kudumu, visiwa 72 vina umeme na visiwa 71 havina umeme. Tulianza na visiwa 20 kuvipelekea umeme na sasa tuna mpango wa kupeleka umeme katika visiwa 36” alisisitiza Mhandisi Mwijage.

Akizungumzia suala la mawakala wa wauzaji mafuta vijijini ambao watakopeshwa ili kutoa huduma hiyo kwa wananchi wa vijijini, Mhandisi Mwijage amesema

“Kitu kikubwa kitakachozingatiwa kwa wauzaji na vituo vya mafuta vijijini ni usalama, mazingira ya kuuzia mafuta, eneo na kituo husika. Watakaokidhi vigezo watawezeshwa kupitia mikopo na lengo letu ni kuhakikisha kwamba katika utekelezaji wa zoezi hili walengwa na wanufaika wote watoke vijijini”

Nao wahariri wa vyombo vya habari Joyce Shebe, Salome Kitomali na Neville Meena wakizungumza katika mkutano huo wameishauri REA kuendelea kutilia mkazo suala la usawa wa kijinsia katika fursa na matumizi ya nishati, kuchangia na kukuza uchumi.

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 umekuwa na desturi endelevu ya kukutana na wadau mara kwa mara kueleza na kutoa mrejesho wa masuala mbalimbali ya nishati vijijini lengo likiwa ni kujenga uelewa wa pamoja kwa wadau na mwananchi mmoja juu kazi zinazoendelea kufanywa na Wakala huo.