Tanzania imechukua hatua ya kusitisha safari za ndege za kimataifa kama sehemu ya jitihada zinazochukuliwa na nchi nyingi duniani kukabiliana na kuenea kwa kasi kwa virusi vya corona (COVID-19).

Mashirika mbalimbali ya ndege ulimwenguni yamesitisha safari zao kwa lengo la kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona (COVID-19) katika mataifa mbalimbali kote duniani.

Shirika la ndege nchini (ATCL) nalo limeamua kusitisha safari za ndege zake kwenda China na India kama hatua za kuhakikisha nchi inakuwa salama.

Kama sehemu ya hatua za kukabiliana na uwezekano wa ugonjwa huo kuingia nchini, Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) tayari limetangaza kusitisha mpango wa kuanzisha safari kati ya Dar es Salaam na Guangzhou, China, ukiwa ni mkakati wa kujilinda.

Wiki iliyopita, wakati akizundua karakana ya kisasa ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Rais John Magufuli alitangaza pia kuwa safari za ATCL nchini India nazo zimesitishwa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuwa makini na kuchukua hatua za kujikinga kuhusu maambukizi ya corona.

Amewataka Watanzania kuzingatia ushauri unaotolewa na wataalamu wa afya kama vile kuacha kusalimiana kwa kushikana mikono, kuacha kupigana mabusu na kuhakikisha wananawa mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni.

“Ndugu zangu Watanzania, ni vizuri sana tukaendelea kuchukua tahadhari kwa nguvu zote. Ugonjwa huu unaua kwa haraka, tusiupuuze hata kidogo ugonjwa huu. Kama una safari ambazo si za lazima sana usisafiri,” anasema Rais Magufuli.

Nchi kadhaa zimechukua hatua ya ‘kujifungia’, kwa maana ya kutoruhusu safari za kuingia au kutoka katika nchi hizo, huku watu ndani ya nchi wakitakiwa kukaa majumbani na kutoka iwapo watakuwa na jambo la lazima tu.

Kwa upande wake, Marekani imesitisha safari zote za ndege kutoka na kwenda nchi za Ulaya na ilitarajiwa kuwa marufuku hiyo itawekwa pia kwa safari za baadhi ya nchi za Asia, ikiwamo China.

Takriban nchi 103 duniani kote zimethibitika kuwa na watu wenye maambukizi ya corona, hali inayoyaweka mataifa mengine katika tahadhari kubwa.

Kusitishwa kwa safari hizo kunatarajiwa kuathiri kwa kiasi kikubwa sekta ya utalii.

Aidha, kusitishwa kwa safari hizo kutasababisha kupungua kwa bidhaa ambazo huagizwa kutoka China na nchi nyingine za Asia.

Siku kadhaa zilizopita, JAMHURI liliripoti wasiwasi ulioonyeshwa na wafanyabiashara katika Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam, hasa wale wanaochukua biadhaa kutoka China, kuwa bidhaa hizo zimeanza kuadimika baada ya China kupiga marufuku ya usafirishaji wa bidhaa hizo kama njia ya kukabiliana na corona.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (AITA), mapato ya sekta ya anga yameporomoka kwa asilimia 19 tangu kuibuka kwa corona mwishoni mwa mwaka jana.

IATA inaeleza kuwa mashirika ya ndege yanatarajiwa kupata hasara ya dola bilioni 113 za Marekani, huku kiasi hicho kikitarajiwa kuongezeka iwapo ugonjwa huo hautadhibitiwa haraka.

Nchi za Italia na Hispania zinatajwa kuathiriwa zaidi na maradhi haya na inaelezwa kuwa zimekwisha kupoteza asilimia tisa ya mapato kupitia sekta ya usafiri wa anga. Takriban watu milioni 16 husafiri kwa kutumia ndege kati ya nchi hizo mbili kwa mwaka.

Aidha, Norway imepunguza safari za ndege kutoka nchini humo kwa asilimia 15, hali inayotajwa kuwa chini ya kiwango cha uwezo wake.

Hata Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) linatarajia kuzuia zaidi ya safari 3,600 huku mashirika ya ndege ya Marekani kama American Airline na Delta nayo yakitangaza kupunguza safari zao kwa mwaka 2020.

Nalo Shirika la Ndege la Korea Kusini limewatangazia wafanyakazi wake kuwa limo hatarini kuporomoka kutokana na ugonjwa wa corona kuendelea kushika kasi.