Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Serikali kupitia Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli Tanzania (PURA) imeendelea kuhamasisha wawekezaji mbalimbali duniani kushiriki katika Duru ya Tano ya Kunadi Vitalu vya utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia katika Bahari Kuu ya Hindi na Nchi Kavu itakayozinduliwa mwezi Machi mwaka huu.
Matangazo ya fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia yanaendelea kupitia Kongamano na Maonesho ya Wiki ya Nishati ya India yanayofanyika katika Jiji la New Delhi, India tukio ambalo linawashirikisha zaidi ya watu 70,000 kutoka nchi zaidi ya 50 Duniani.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/image-47.png)
Katika Banda la Tanzania kwenye Maonesho hayo washiriki wengi wamevutiwa na taarifa za kijiofizikia zinazobainisha utajiri wa rasilimali ya mafuta na gesi asilia zilizopo Tanzania.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ambaye anashiriki Kongamano hilo, ametembelea banda hilo la Tanzania na kuipongeza PURA kwa kutumia majukwaa ya kitaifa na kimataifa kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia.
Dkt. Biteko ameeleza kuwa, lengo la Serikali ni kuhakikisha vyanzo vyake vyote vya nishati vinaendelezwa ili kuwa na uhakika wa nishati ya kutosha wakati wote.
Katika kuelekea kwenye duru hiyo ya Tano ya Kunadi Vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mhandisi Charles Sangweni amesema PURA imekamilisha masuala mbalimbali ikiwemo kupata Kampuni ya Kijiofizikia iitwayo TGS ASA yenye utaalam wa kuchakata data za mafuta na gesi asilia ambayo pia inahusika na utangazaji wa data hizo katika masoko mbalimbali duniani .
Mhandisi Sangweni amesema kampuni hiyo itatakiwa kukusanya na kuchakata data za mitetemo katika maeneo mengine ya bahari kuu ambayo hayajafanyiwa kazi ili kuongeza taarifa na data za petroli kwa wawekezaji.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/image-48.png)
Ameongeza kuwa, PURA imeshakamilisha uandaaji wa ramani inayoonesha maeneo ambayo yatatangazwa kwenye duru ya tano inayojumuisha vitalu 26 ambapo vitalu 23 viko kwenye kina kirefu cha Bahari ya Hindi na vitalu vitatu vipo Ziwa Tanganyika.
Amesema Duru ya tano ya Kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia itafanyika mwezi Machi, 2025 katika Mkutano na Maonesho ya Petroli ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (East African Petroleum Conference and Exhibitions (EAPCE’25) Jijini Dar es Salaam.
Maonesho hayo yatakwenda pamoja na maonesho ya kitaalam kuhusu jiolojia ya mafuta na gesi asilia ya Tanzania; wawekezaji kuangalia taarifa za kijiolojia, kununua zabuni, kuwasilisha zabuni, kufanya tathmini ya zabuni zilizowasilishwa na kupokelewa, kufanyika kwa majadiliano ya mikataba (PSAs), kupata idhini ya Serikali ya kusaini PSAs kutoka Wizara ya Nishati na Baraza la Mawaziri na Kusaini Mikataba kati ya Serikali na Wawekezaji wawatakaoshinda.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/image-50.png)
Ametaja faida mbalimbali zitakazopatikana baada ya Serikali kunadi vitalu hivyo kuwa ni kuongezeka kwa mapato ya kodi kwa Serikali, mirabaha na gawio la faida itokanayo na rasilimali itakayogundulika, mauzo ya data na tozo za leseni pamoja na kutoa fursa ya ajira kwa Watanzania na kazi kwa makampuni ya kitanzania,.
katika Kongamano hilo linaloendelea nchini India, Dkt.Biteko alipata fursa ya kutembelea na kuzungumza na Watendaji wa Wizara ya Umeme ya India pamoja na Watendaji wa kampuni ya Shell ambayo ni moja ya wawekezaji katika mradi wa LNG ambapo aliwaeleza Watendaji wa Shell kuwa Serikali inataka kuona majadiliano yanakamilika na mradi unaanza kutekelezwa.
Dkt. Biteko alifuatana na baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini ambao ni Mhe. Juliana Masaburi, Mhe. Ussi Pondeza na Mhe. Iddi Kassim Iddi.
![](https://www.jamhurimedia.co.tz/wp-content/uploads/2025/02/image-49.png)