Na Benny Mwaipaja, JamhuriMedia Dar es Salaam

Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa Tanzania inatambua mchango mkubwa wa Serikali ya Uswisi katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii tangu nchi hizo mbili zilipoanza uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi zaidi ya miaka 43 iliyopita.

Dkt. Nchemba amesema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi mpya wa Uswisi hapa nchini, Nicole Providoli, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam ambaye alifika kujitambulisha.

Katika kikao hicho walijadili masuala kadhaa ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Uswisi, kupitia miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na nchi hiyo, ukiwemo mradi wa kusaidia kaya maskini kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambapo tangu mwaka 2023, Uswisi imechangia shilingi bilioni 88.1 katika Mfuko huo.

Kwa upande wake, Balozi Mpya wa Uswisi hapa nchini, Mhe. Nicole Providoli, alisema kuwa uhusiano wa Tanzania na nchi yake umekuwa imara na kwamba Uswisi itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kutekeleza mipango na miradi yake ya maendeleo inayoinufaisha jamii.

Aliyataja maeneo ya kimkakati ambayo nchi yake imekuwa ikiisaidia nchi ikiwemo sekta ya afya, elimu na kusaidia mpango wa kukabiliana na umasikini, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii-TASA

Mkutano huo umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha ambaye pia ni Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Melkzedeck Mbise, na Maafisa Waandamizi kutoka Ubalozi wa Uswisi hapa nchini, Wizara ya Fedha na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.