Na WAF DSM

Serikali ya Uingereza imeendelea kuimarisha ushirikiano wake na Tanzania kwa kutoa Bilioni 45 kusaidia kufanikisha huduma za uzazi wa mpango nchini.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel, wakati wa hafla ya kumpokea Waziri wa Maendeleo na Maswala ya Afrika kutoka Uingereza, Mhe. Andrew Mitchell, aliyetembelea Zahanati ya Vingunguti na kujionea huduma za uzazi wa mpango zinavyofanya kazi.

Dkt. Mollel ameeleza kuwa ufadhili huo ni matunda mazuri ya juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuimarisha mashirikiano na mataifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Uingereza.

“Kupanga uzazi ni sehemu muhimu ya afya ya mama na mtoto, inayosaidia jamii kupata nafasi ya kuzingatia uzazi na kuhakikisha usalama wa mama na mtoto unapatikana kwa kuacha nafasi baina ya watoto mmoja na mwingine, hasa katika kipindi cha unyonyeshaji, ili kila mtoto apate muda sahihi wa kunyonya pale anapozaliwa,” amesisitiza Dkt. Mollel.

Ameishukuru Serikali ya Uingereza kwa ufadhili huo na kusema kuwa serikali itahakikisha jamii inapata elimu sahihi kuhusu uzazi wa mpango ili fedha hiyo itumike kusaidia wananchi na Watanzania kwa ujumla katika kupanga uzazi.

Waziri wa Maendeleo na Maswala ya Afrika kutoka Uingereza, Mhe. Andrew Mitchell, amesema kuwa lengo la ufadhili huo ni kuwawezesha Watanzania, hususan vijana, kufanya maamuzi sahihi kuhusu wakati wanapotaka kuwa na watoto ili kuhakikisha shughuli za uzazi hazikwamishi shughuli za maendeleo nchini.

“Kupitia ufadhili huu, vijana watapata elimu ya kujikinga na maradhi mbalimbali kama vile UKIMWI na kuelewa umuhimu wa kutumia uzazi wa mpango katika familia zao ili kusaidia taifa kuwa na mpangilio mzuri wa watoto kupishana na kupeana muda wa kunyonya”, ameeleza Mhe. Mitchell