TANZANIA imekabidhi mapendekezo ya maandiko ya mradi 3, kwa ajili ya kuombea fedha kutoka katika Mfuko wa Hasara na Upotevu unaosababishwa na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi.

Hayo yamejiri wakati Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Christina Mndeme alipokutana na kufanya mazungumzo na Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Hasara na Upotevu unaosababishwa na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, Ibrahima Cheikh Diong katika mji mkuu wa Philippines, Manila leo Desemba 04.

Mndeme akiwa ameambatana na Mkurugenzi wa Tathmini na Ufuatiliaji Ofisi ya Makamu wa Rais, Sigsbert Kavishe wamefanya mazungumzo hayo wakati wa Kikao cha nne cha Bodi ya Mfuko wa Kukabiliana na Hasara na Uharibifu unaosababishwa na Athari za Mabadiliko ya Tabianchi ambapo Tanzania ni Mwanachama wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabinchi (UNFCCC).

Aidha, katika mazungumzo hayo Ibrahima ameahidi kufanyia kazi maombi hayo na pia kuipongeza Tanzania kwa kuwa nchi ya kwanza kuwasilisha mapendekezo ya miradi.