Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,
Dar es Salaam
Tanzania imepandishwa kwenye orodha ya kimataifa ya viwango vya nchi vya kukopa kutokana na kuimarika kwa uchumi wake ndani ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la kukadiria uwezo wa mataifa wa kuchukua mikopo liitwalo Moody’s.
Sababu kubwa iliyotajwa kwa Tanzania kupanda hadi kiwango cha B1 kutoka B2 ni uchumi himilivu, mageuzi chanya yanayofanywa na Serikali ya Rais Samia na ongezeko kubwa la uwekezaji wa ndani na nje.
Kwa mujibu wa Moody’s, Tanzania sasa iko kwenye kiwango cha B1 (stable outlook), kutoka kiwango cha B2 (positive outlook).
Maana ya Tanzania kupanga viwango hivyo ni kuwa Serikali inaweza kukopa mikopo ya kimataifa kwa riba nafuu zaidi kwani uchumi wake unaonekana kuwa himilivu na Serikali inaweza kulipa deni lake.
Kwa sasa Tanzania ina kiwango cha juu zaidi cha kukopesheka kwa nchi zote za Afrika Mashariki, ikiwa juu ya Kenya (B3 negative), Uganda (B2 negative) na Rwanda (B2 stable).
Kiwango hicho kizuri cha Tanzania pia kitasaidia kuchochea wawekezaji kutoka nje wazidi kuja nchini kwani wanakuwa na uhakika wa utulivu wa uchumi.
Moody’s imesema katika taarifa yake jana kuwa uamuzi wa kuipandisha Tanzania kiwango cha ukopeshaji unatokana pia na ukuaji imara wa uchumi na deni la taifa ambalo ni himilivu.
“Kupandishwa kwa kiwango cha Tanzania hadi B1 kunaashiria rekodi nzuri ya uhimilivu wa uchumi wake miaka hii ya karibuni licha ya misukosuko kadhaa duniani na hivyo kujenga imani kuwa uchumi wake una uwezo wa kukabiliana na changamoto zozote siku zijazo,” Moody’s wamesema.
Kwa mujibu wa Moody’s, uchumi wa Tanzania umekuwa kwa kasi kubwa ya wastani wa asilimia 6 kwa mwaka kati ya mwaka 2015 hadi 2022, ukiongozwa na sekta za kilimo, utalii, madini na ujenzi.
Ongezeko la mauzo ya nje ya bidhaa na huduma, deni la taifa himilivu na sera madhubuti za fedha zimechangia Tanzania kupandishwa kiwango hadi B1, taasisi hiyo imesisitiza.
Moody’s imesema kuwa mageuzi ya kiuchumi yameshika kasi chini ya uongozi wa Rais Samia, ikiwemo kujenga taasisi imara.
Taasisi hiyo imesema kuwa Tanzania inapaswa kuendelea na mageuzi ya kiuchumi kama inataka kupanda zaidi kwenye kiwango chake cha kukopesheka.