Tanzania inatarajia kunufaika na Dola za Marekani milioni 13 kwa ajili ya kuongeza wigo wa utekelezaji wa miradi ya kijamii kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa katika Halmashauri 15 zaidi kupitia Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mitaji na Maendeleo (UNCDF).
Hayo yamebainika wakati wa Mkutano Uwili baina ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais Mhandisi Cyprian Luhemeja na UNCDF uliofanyika wakati wa Mkutano wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mabadiliko ya Tabianchi unaoendelea jijini Baku nchini Azerbaijan.
Mkutano huo umelenga kujadiliana kuhusu maeneo ya ushirikiano zaidi katika miradi ya kijamii ya kuhimimi mabadiliko ya tabianchi ambapo kiasi hicho cha fedha kitatolewa kupitia utekelezaji wa Mpango wa Local Climate Adaptation.Living Facility (LoCAL) na Kujenga uwezo wa Ufuatiliaji wa Fedha za Mabadiliko ya Tabianchi.
Akizungumza wakati wa mkutano huo Mhandisi Luhemeja amesema Tanzania itaendelea kunufaika na miradi hiyo katika sekta za maji, mifugo, uvuvi na miundombinu kupitia utekelezaji wa Mpango wa Kuhimili Mabadiliko ya
Tabianchi (NAP) na Mchango wa Taifa wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi (NDC).
Wakati huo, Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD) na NDC Partnership wamekubali kuongeza fedha zaidi za kuandaa na kutekeleza mchango wa taifa katika kupunguza gesijoto kqa kiasi cha zaidi ya Dola za Marekani 19.2 bilioni zinahitajika kuutekeleza.
Itakumbukwa kuwa tayari Halmashauri tatu za Wilaya za Chamwino, Kondoa na Mpwapwa zilizopo katika Mkoa wa Dodoma zilikwishanuifaka na mradi huo.
Mkutano huo wa uwili uliwashirikisha Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Bi. Amina Khamis Shabaan, Mkurugenzi wa Mazingira Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Bi. Farhat Mbarouk, Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Kanizio Manyika na wataalamu kutoka idara za kisekta na taasisi za Serikali.