Na Mwandishi Maalumu

Ubalozi wa Tanzania umetamba kwenye Tamasha la Mabalozi 2024 (Embassy Festival) nchini Uholanzi, ambalo limevutia watazamaji zaidi ya 50,000 mwishoni mwa wiki iliyopita katika jiji la The Hague.

Idadi hiyo ya wahudhuriaji ilijumuisha makumi ya Watanzania waishio Uholanzi pamoja na wawekezaji kutoka Tanzania kama vile kampuni ya PetroBas NL.

“Tamasha hili ni fursa ya kipekee ya kuonyesha utajiri wa utamaduni wa Tanzania, nasi hatukuiacha ipite bure,” alisema Balozi wa Tanzania nchini Uholanzi, Mhe. Caroline Kitana Chipeta.

Balozi Chipeta alibainisha kuwa tamasha hilo lilitoa fursa za kukuza utalii, lugha ya Kiswahili, na mitindo mchanganyiko ya zamani na ya sasa, ambapo Tanzania iliibuka kuwa kivutio kikubwa.

“Banda la Tanzania lilivutia sana kwa vyakula vya kitamaduni na vifaa vya asili kiasi kwamba Mstahiki Meya wa The Hague, Jan Van Zanen, alitembelea na kutilia sifa nyingi, akiongeza heshima zaidi kwa Tanzania katika tukio hilo,” aliongeza Balozi Chipeta.

Pia, Tanzania ilifanya onyesho la kuvutia la mitindo, likiongozwa na mbunifu wa Kitanzania, kwa kuchanganya mavazi ya zamani na ya sasa, jambo lililopata umaarufu mkubwa.

Balozi Chipeta, akiwa amevalia vazi la kimwambao la khanga na baibui, alishangiliwa sana kwa ushiriki wake. Alisema onesho hilo lilikuwa njia nzuri ya kuendeleza tamaduni za jadi kwa mtazamo wa kisasa.

Banda la Tanzania pia lilitoa burudani kwa muziki wa Bongo Fleva, huku wimbo wa “Coma Cava” wa Diamond Platnumz ukiwa kivutio kikubwa. Diamond atafanya onyesho jijini Amsterdam mnamo Septemba 30, 2024.

Please follow and like us:
Pin Share