Mkutano wa Biashara na Uwekezaji (Business and Investment Forum) uliofanyika kwa siku mbili katika Mji wa Marseille, nchini Ufaransa, kuanzia Februari 11 hadi 12 mwaka huu, umefungua fursa mpya kwa Tanzania katika kuvutia wawekezaji wa kimataifa.

Ujumbe kutoka Tanzania, uliongozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, katika mkutano huo wenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Ufaransa.

Mkutano huo uliofunguliwa na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Ali Jabir Mwadini, alisisitiza amri kumi za uwekezaji na umuhimu wa ushirikiano wa kibiashara kati ya mataifa haya mawili.

Katika hotuba yake, alibainisha kuwa Tanzania ni miongoni mwa nchi zenye fursa kubwa za uwekezaji Barani Afrika, hasa katika sekta za kilimo, utalii, miundombinu, na nishati.

Aidha, katika mkutano huo Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPPC), David Kafulila, alifafanua zaidi namna miradi ya PPP inavyofanya kazi nchini, huku akiwakaribisha wawekezaj kutoka Ufaransa kuja kuwekeza Tanzania kupitia mfumo wa PPP ambao tayari umeanza kuonyesha mafanikio mkubwa.

Pia Kafulila alisaini mkataba wa makubaliano kati ya Tanzania Chamber of Commerce na Marseille, akimwakilisha Rais wa chemba hiyo katika mkataba huo wa makubaliano.

Aidha, katika mijadala iliyofanyika, Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kilitoa wasilisho maalum likielezea fursa mbalimbali zinazopatikana nchini Tanzania, huku likitoa mwanga kwa wawekezaji kuhusu mazingira wezeshi ya biashara.

Ujumbe wa Tanzania pia ulihusisha wawakilishi kutoka Wizara ya Kilimo, Ofisi ya Rais, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), pamoja na Sekta ya Utalii.

Mbali na majadiliano ya kitaalamu, washiriki wa mkutano walipata nafasi ya kushiriki katika shughuli za mtandao, ambapo wawekezaji wa kimataifa walipata fursa ya kujadili uwezekano wa kushirikiana na sekta mbalimbali nchini Tanzania.

Mkutano huo ulimalizika kwa ziara ya kutembelea kiwanda cha CMA kilichopo Ufaransa, ambapo wajumbe wa Tanzania walipata nafasi ya kujifunza mbinu za kisasa za uzalishaji viwandani.

Mkutano wa Biashara na Uwekezaji wa Marseille umedhihirisha dhamira ya Tanzania katika kujenga ushirikiano imara na mataifa ya Ulaya, huku ukifungua njia kwa wawekezaji zaidi kuchangamkia fursa zilizopo nchini.