Tanzania kupitia Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imechaguliwa kuwa Makamu wa Rais wa Tume ya Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) inayosimamia uangazi, miundombinu na mifumo ya taarifa za hali ya hewa (WMO Commission for Observation, Infrastructure and Systems – INFCOM).
Katika uchaguzi huo Tanzania iliwakilishwa na Mkurugenzi wa Miundombinu na Huduma za Ufundi, TMA, Dkt. Pascal Waniha.
Dkt. Waniha amechaguliwa katika nafasi hiyo leo tarehe 18 Aprili, 2024 katika uchaguzi wa viongozi wa Tume ya INFCOM uliofanyika katika Mkutano wa tatu wa Tume hiyo (Third Session of the WMO Commission for Observation, Infrastructure and Systems- INFCOM-3)”, unaoendelea katika makao makuu ya WMO, Geneva- Uswisi tarehe 15 hadi 19 Aprili, 2024.
Uchaguzi wa Tume ya INFCOM umefanyika kufuatia muda wa viongozi waliokuwa madarakani kumaliza muda wao ambapo viongozi hao walichanguliwa mwaka 2021 na waliongoza Tume ya INFCOM katika kipindi cha miaka minne (2020/21 – 2023/24).
Uongozi wa juu wa Tume ya INFCOM unaundwa na Rais wa Tume akisaidiana na Makamu watatu wa Rais. Wagombea katika nafasi ya Makamu wa Rais walikuwa wanne (4), kutoka Tanzania, Czech, Hong Kong-China na India.
Katika kinyang’anyiro hicho zilihitajika nafasi tatu na viongozi wapya waliochaguliwa ni Rais wa Tume hiyo, Bw. Michel Jean (Canada) ambaye anaendelea katika nafasi yake, na Makamu wa Rais ambao ni Dkt. Pascal Waniha (Tanzania), Dk. Chan Pak Wai (Hong Kong, China) na Dkt. Jan Danhelka (Jamhuri ya Czech
Tume ya INFCOM ni mojawapo ya mihimili mikuu mitatu inayounda Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), Mihimili hiyo ni: (1) Tume inayosimamia uangazi, miundombinu ya hali ya hewa na mifumo ya Taarifa za Hali ya Hewa (Commission for Observation, Infrastructure and Systems – INFCOM); (2) Tume inayosimamia Matumizi ya Taarifa za Hali ya Hewa (Commission for Weather, Climate, Hydrological, Marine and Related Environmental Services and Applications – SERCOM) na Bodi ya Utafiti (Research Board).
Dkt. Waniha atakuwa miongoni mwa viongozi wapya wa Tume ya INFCOM watakaoiongoza Tume hiyo katika kipindi cha miaka minne (2024- 2028).
Dkt. Waniha ni Mtaalamu mbobezi wa hali ya hewa katika eneo la utabiri wa hali ya hewa kwa kutumia modeli (Climate Modelling and Numerical Weather Prediction -NWP) kwa takribani miaka 29.
Ametoa mchango mkubwa katika fani ya hali ya hewa ndani na nje ya Tanzania hususan katika WMO kupitia vikosikazi mbalimbali vya kuboresha miundombinu na huduma za hali ya hewa.
Kuchaguliwa kwake katika nafasi hii ni muhimu kwa Tanzania na Afrika kwa ujumla ikizingatiwa kuwa nchi nyingi za Afrika zina changamoto ya upungufu wa miundombinu na teknolojia ya miundombinu ya hali ya hewa.
Miundombinu ya hali ya hewa ni muhimu katika kupima na kufuatilia mienendo ya mifumo ya hali ya hewa na kukabiliana na changamoto ya mabadiliko ya hali ya hewa na tabianchi.