Maelfu ya wananchi wa mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam wamejitokeza katika zoezi la kuanza ujazaji wa maji kwenye Bwawa la Mwalimu Nyerere (JNHPP), lililopo wilayani Rufiji mkoani Pwani.

Zoezi hilo la ujazaji maji linazinduliwa leo na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameambatana na viongozi mbalimbali wa serikali na kisiasa.

Bwawa hilo ambalo ujenzi wake umegharimu Sh.trilioni 6.5 linatarajiwa kuzalisha megawati za umeme 2,115 ambazo zitaingizwa kwenye gridi ya taifa na kumaliza changamoto ya umeme nchini.

Mwitikio wa wananchi zaidi ya 2,000 katika tukio hilo la ujazaji maji unatokana umuhimu wa mradi huo kwa maendeleo ya nchi kwa miaka ijayo.

Mradi huo ulianza kujengwa kupitia Serikali ya Awamu ya Tano ambayo ilikuwa ikiongozwa na Rais John Magufuli ambapo Rais Samia ameendeleza na leo atazindua zoezi la ujazaji maji.

Kwa mujibu wa Waziri wa Nishati, January Makamba mradi huo umefikia asilimia 78 ya ujenzi na unatarajiwa kukamilika 2024.

Mradi huu wa JNHPP ambao utazalisha megawati 2,115 utakuwa mkubwa kwa Afrika Mashariki na wanne kwa Afrika.

Akifafanua kuhusu ujenzi wa mradi huo Mhandisi Said Kimbanga alisema kuna mitambo tisa ambapo kila mmoja utakuwa unazalisha megawati 235, hivyo kwa jumla kuzalisha megawati 2,115.

Amesema maji ambayo yataingia kuzalisha umeme yanatoka Mto Kilombero, Ruaha Mkuu na Kuwegu.

Mhandisi Kimbanga amesema eneo la mradi bwawa huo lina ukubwa wa hekta 915 ukubwa ambao ni sawa na ziwa ambapo ujazo wa maji lita bilioni 32.

Amesema valvu iliyofungwa katika mradi huo wakuzalisha umeme ni ya tatu kwa ukubwa duniani ambapo ya kwanza ipo Pakistani na ya pili ipo India.

Baadhi ya viongozi walioungana na Rais Samia ni pamoja Rais wa Awamu ya Pili, Alhaj Ally Hassan Mwinyi, Rais wa Awamu ya Nne, Dk Jakaya Kikwete, Makamu Mwenyeki wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kanali mstaafu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, Waziri wa Fedha na Mipango Mwigulu Nchemba, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnaye, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa na wengine wengi.