Rais wa Awamu ya Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli, amesema anapochukua hatua yeye si kichaa, si dikteta, si shetani wala si mnyama, ila ni mpole, lakini amefika mahali lazima afanye hivyo kwani ndani ya Serikali yanafanyika mambo ya ajabu.

Kauli hiyo ameitoa wiki iliyopita jijini Dar es Salaam katika kilele cha Siku ya Sheria nchini, alipokuwa mgeni rasmi kwa mara ya kwanza katika uzinduzi wa Mwaka wa Mahakama tangu alipoapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kiu ya Watanzania wengi ilikuwa ni kumpata Rais mkali, atakayepambana na rushwa na ufisadi ambao umeigharimu nchi kwa tawala zilizopita. Nchi yetu ilionekana ni shamba la bibi lililokosa mlinzi wala mtunzaji.

Raia wa kigeni kwa jeuri iliyosababishwa na kutojitambua kwa viongozi waliokuwa madarakani, walithubutu kutamka wazi wazi kwamba Tanzania ni kama choo! Mtu anaingia na kutoka kama apendavyo na pia kufanya jambo lolote analolitaka. Hakuna anayejali isipokuwa viongozi na watendaji karibu wote waliwaza manufaa yao binafsi.

Watanzania kwa karibu miongo mitatu ya utawala wa nchi hii wamepitishwa katika machungu mengi. Kwani, wako waliopoteza maisha kutokana na njaa, kuporwa mali zao na wale walio na ukwasi, na wengine kupoteza maisha kwa kushindwa kumudu kununua dawa kutokana na maradhi yaliyowapata na adha nyingine nyingi.

Lakini baada ya kuingia madarakani Rais Magufuli, kundi la ‘watafuna nchi’ lililojiwekea mirija kuwanyonya Watanzania kama watakavyo kwa kujijenga kikamilifu ndani ya CCM na Serikali yake, limeanza kutapatapa na kudai Rais ni dikteta, mbabe, hataki kusikia ushauri wa wenzake wala hana huruma na watu.

Wanaolalamika wengi wao ndiyo waliojigeuza madalali wa wakoloni wanaokuja kwa hadaa mpya ya uwekezaji na kuwasaidia kuwapa mbinu za kukwepa kodi na kufanya lolote walitakalo ndani ya nchi yetu.

Hata hivyo, napenda kumkumbusha Mheshimiwa Rais, Dk. Magufuli, kwamba majipu ndani ya nchi hii ni mengi mno. Mengine yameoza, yananuka kweli kweli. Pamoja na kazi hiyo ngumu inayohitaji daktari jasiri kama wewe, inapaswa kuelewa chanzo chake ni nini?

Kuanzia mwaka 1989 hadi 1995, uchumi wa nchi yetu uliporomoka huku thamani ya shilingi nayo ikiporomoka kwa kasi, viwanda vingi vya umma vikafa na tegemeo kubwa la Watanzania likiwa kufanya biashara ya kuuza bidhaa za mataifa ya nje. Tukakosa fedha za kigeni. Chanzo kikubwa ni viongozi wa Tanzania kuilaani Israeli kwa nguvu zao zote. Badala ya kulaaniwa Israeli laana ya kutosha ikalikumba Taifa letu.

Kufafanua laana hiyo nitanukuu maandiko ya Biblia Takatifu yafuatayo:- 

MWANZO 12: 1-3, Bwana akamwambia Abrahamu, toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha; nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa …nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa.

Katika uzao huo huo wa Ibrahimu, tunaona Yakobo akibarikiwa na kuitwa Israeli (MWANZO 32: 24-29) (MWANZO 27:29). Laana ndiyo chanzo kikuu cha madudu yote yanayofanyika serikalini sasa. Nchi ina kila kitu lakini inaitwa nchi masikini duniani.

Kenya wao waliigundua siri hii mapema ndiyo maana hawajatamka laana kwa Israeli, uchumi wao unasonga mbele. Wanapigana vita Somalia wako imara kiuchumi pia wananufaika vile vile na rasilimali za Tanzania. Rais Magufuli tumbua majipu kwa bidii yote; lakini jenga uhusiano mzuri na Israeli.