Na Mwandishi Wetu- Madrid, Hispania

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) zimesaini mkataba wa makubaliano utakaoifanya Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la Pili la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa (The 2nd UN Tourism Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa) linalotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Machi 11 hadi 13, 2025.

Hafla ya utiaji saini imefanyika kati ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili katika kikao kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa jijini Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili na wakionyesha makubaliano waliosaini kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la 2 la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa katika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa jijini Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mhe. Chana amesema Tanzania inafuraha kuwa mwenyeji wa kongamano hilo linalotarajia kukutanisha washiriki zaidi ya 300 kutoka mataifa mbalimbali duniani na kwamba kupitia kongamano hilo Tanzania itajifunza kutoka mataifa hayo namna wanavyofanya katika kukuza utalii wa vyakula.

“Kupitia Kongamano hili tunataka kuwajengea uwezo wapishi wetu jinsi ya kutengeneza aina tofauti za vyakula ili watalii wanapokuja waweze kufurahia vyakula vya nyumbani kwao lakini pia tunahitaji kuona ni fursa gani zitakazotokana na kongamano hilo ili tuweze kujifunza utangazaji utalii wa vyakula” Mhe. Chana alisisitiza.

Mhe. Chana amefafanua kuwa Tanzania na UN Tourism zimekuwa zikishirikiana katika masuala mbalimbali kwa lengo la kukuza utalii.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) katika kikao na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili wakijadili kuhusu namna bora ya kuboresha Kongamano la 2 la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa (The 2nd UN Tourism Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa) litakalofanyika nchini Tanzania mwezi Machi, 2025, kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa jijini Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.

“Miongoni mwa maeneo tunayoomba ushirikiano kwa sasa ni katika masuala ya sera na ukuzaji ujuzi, Rasilimali Watu na Mpango Mkakati wa Kukuza Utalii” alisema Mhe. Chana.

Katika hatua nyingine, Mhe. Chana alisema Tanzania inatambua na kuthamini jukumu muhimu la Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa (UN Tourism) katika kuunda sera za kimataifa za utalii,kukuza utalii endelevu na kukuza ukuaji wa uchumi.

Naye, Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili alisema kuwa Shirika la Utalii Duniani limelenga kuitangaza Afrika kama sehemu ya utalii inayofikika sambamba na kutangaza utalii wa vyakula.

Katika kufanikisha kongamano hilo, Bw. Pololikashvili amependekeza kwa Tanzania kutumia njia zote za mawasiliano ili kulitangaza kongamano hilo ikiwa ni pamoja na kutumia watu maarufu wenye ushawishi katika jamii na kuwatumia wapishi wa vyakula mbalimbali vya kiafrika.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi, Dkt. Pindi Chana (Mb) (kushoto) na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili (kulia) na wakisaini Makubaliano ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la 2 la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa (The 2nd UN Tourism Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa) katika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa jijini Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.

“ Pia ningeiomba Tanzania kuhakikisha zoezi la upatikanaji wa viza pamoja na usafiri wa anga kwa ujumla linakuwa rafiki kwa waombaji wanaotarajia kusafiri kuja kwenye kongamano hilo” amesisitiza Pololikashvili.

Mkutano huo umehudhuriwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii Tanzania, Mhe. Balozi Ramadhani Dau, Balozi wa Tanzania nchini Hispania, Mhe. Balozi, Ali Jabir Mwadini, Mkurugenzi wa Utalii, Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Thereza Mugobi, Mjumbe wa Bodi ya TTB, Said Kamugisha na Afisa Balozi, Amos Tengu na sekretarieti ya Shirika la UN Tourism.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) akizungumza katika kikao kati yake na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili(hayupo pichani) kuhusu Tanzania kuwa mwenyeji wa Kongamano la 2 la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa, kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa jijini Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana (Mb) katika kikao na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani (UN Tourism), Zurab Pololikashvili wakijadili kuhusu namna bora ya kuboresha Kongamano la 2 la Kikanda la Utalii wa Vyakula la Shirika la Umoja wa Mataifa (The 2nd UN Tourism Regional Forum on Gastronomy Tourism for Africa) litakalofanyika nchini Tanzania mwezi Machi,2025, kilichofanyika Makao Makuu ya Shirika la Utalii Duniani la Umoja wa Mataifa jijini Madrid, Hispania leo Januari 24,2025.