Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

SERIKALI ya Tanzania imeihakikishia Serikali ya Uingereza kuendeleza ushirikiano kwenye sekta ya madini hususani katika kujengea uwezo watu wake, kubadilishana uzoefu, uongezaji thamani madini na kuwekeza kwenye kufanya tafiti mbalimbali ili kukuza sekta ya madini na kupanua mnyororo wa thamani ili kuongeza ajira na kuchangia katika ukuaji wa pato la taifa.

Kwa mujibu wa Wizara ya Madini, Waziri wa wizara hiyo Anthony Mavunde amesema hayo katika ofisi ndogo za Wizara ya Madini jijini Dar es Salaam alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Marianne Young.

“Kwanza kabisa Mhe. Balozi Young amefika ofisini kujitambulisha kwa kuwa ana muda mfupi nchini tangu awasili lakini pia tumezungumzia ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Tanzania na Uingereza”, amesema Mavunde.

Katika mazungumzo hayo, Tanzania na Uingereza zimekubaliana kuwajengea uwezo watu wake na kubadilishana uzoefu hususani katika Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini nchini (GST) na British Geological Survey (BGS) ya Uingereza ili kuwajengea uwezo Watanzania wawe na ujuzi stahiki katika masuala ya uendelezaji wa sekta ya madini.

Mavunde amesema eneo la pili la mazungumzo hayo ni katika madini mkakati ambapo Uingereza imeonesha utayari kushirikiana na Tanzania eneo la mnyororo mzima wa uongezaji thamani madini mkakati ambapo Tanzania imejipanga kuhakikisha inavutia uwekezaji mkubwa wa ujenzi wa viwanda vya kuongeza thamani madini hapa nchini.

Amesema sasa ni muda muafaka wa kuhakikisha madini ya kimkakati yanawanufaisha Watanzania na taifa, na ndiyo maana Serikali imeandaa mkakati maalumu wa kutekeleza azma hiyo huku ikizingatiwa kuwa madini hayo kwa sasa yana mahitaji makubwa duniani.

Waziri Mavunde amesema Serikali ipo katika hatua za mwisho kukamilisha mkakati huu maalum wa madini mkakati na muhimu ambao pia ni sehemu ya kampeni ya Dunia katika kupunguza hewa ya ukaa kupitia matumizi ya nishati safi.