Tanzania na Ufaransa zimesaini Tamko la Paris (Paris Declaration) katika kuimarisha ushirikiano wa kidiplomasia na kiuchumi uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Tamko hilo limesainiwa leo tarehe 14 Mei, 2024 jijini Paris Ufaransa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Makamba na Waziri wa Ufaransa anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa, Mhe. Chrysoula Zacharopoulou.
Maeneo ya ushirikiano yaliyosainiwa ni pamoja na Nishati na mabadiliko ya tabianchi, usafirishaji na maendeleo ya miundombinu, usawa wa kijinsia na uwezeshaji wanawake.
Hafla ya utiaji saini imeshuhudiwa na Mabalozi wanaowakilisha katika hizo, Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Ali Jabir Mwadini, Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Mhe. Nabil Hajlaoui, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Noel Kaganda na Maafisa wengine Waandamizi walioambatana na Viongozi hao wawili.