Kama tujuavyo, jina Tanzania lina maana mbili. Kwanza Tanzania ni Taifa, na Taifa ni jamii ya watu huru walio chini ya utawala mmoja. 

Hapa tutaendelea kuwashukuru Mwalimu Julius Kabarage Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume walioongoza kwa usalama juhudi za kutafuta uhuru. Tukapata uhuru, tukawa jamii ya watu huru yaani Taifa.

 Lakini pia Tanzania ni nchi. Nchi ni eneo kubwa la ardhi lenye mipaka yake na utawala wake. Utawala wa ndani huongozwa na watu. Watu wanaoongoza nchi hufanya hivyo kwa niaba ya Mungu. Wakitawala nchi bila kuwa na hofu ya Mungu basi hufanya mambo kwa hofu ya shetani. Wanatumikia shetani.

Ukitaka kusema kweli, kadri siku zinavyoendelea kupita, ndivyo hali ya mambo kwetu Tanzania inavyokuwa mbaya. Ni matokeo ya viongozi wa nchi kufanya mambo bila kuwa na hofu ya Mungu.

Tunapomzungumzia Mungu tunazungumza bila kujali kama Taifa letu lina dini au halina dini. Tunasema kwamba Tanzania ni nchi isiyo na dini, lakini watu wake wana dini zao. Hii haina maana kwamba viongozi wa nchi wanatakiwa kufanya mambo kwa utashi wao bila kuwa na hofu ya Mungu. 

Si vyema mambo yetu yakaenda vibaya kiasi cha kuwathibitishia walimwengu kwamba kweli Tanzania ni nchi isiyo na dini. Kwa hivyo, ni muhimu watawala wetu wafanye mambo kwa kumwogopa Mungu bila kujali kama wana dini au hawana dini.

Kuna wakati viongozi wetu wakijigamba mbele ya mataifa mengine kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani. Leo hakuna kiongozi anayeweza kuthubutu kusimama hadharani na kudai kwamba Tanzania ni kisiwa cha amani. Wameifikisha nchi pabaya. Wamevunja amani yetu.

Kwa kweli tukiangalia hali ya kisiasa Tanzania, tutakubaliana kwamba ni mbaya sana. Tumefika mahali ambapo wabunge wa vyama vya upinzani wameapa kutowasalimia wabunge wa chama tawala. Kwa sababu wanaona wanaonewa na kunyanyaswa na chama tawala na Serikali yake.

Kauli hii ya wabunge wa nyumba moja kuacha kusalimiana haijapata kutokea katika historia ya Tanzania. Tumefikaje hapa? Hatukufika wenyewe, tumefikishwa mahali hapa pabaya na viongozi wetu.

Viongozi wa nchi hii iliyokuwa kisiwa cha amani sasa wanafanya mambo ya kutisha sana. Na hapa hakuna anayezungumzia Rais Magufuli peke yake. Hatudhani kwamba kuna jambo Rais Magufuli anaweza kuamua au kufanya peke yake bila kushirikisha viongozi wenzake.

Tukirudi nyuma, tumesikia madai ya chama kikuu cha upinzani bungeni (Chadema) kwamba katika maadhimisho ya sikukuu ya CCM kule Singida Februari mwaka huu, Rais Magufuli aliwaambia wanachama wenzake kwamba amenuia kuua upinzani nchini.

Lakini wananchi wa Tanzania wanaukubali upinzani na wanauunga mkono. Basi kitendo cha kuua upinzani kitazusha mapambano kati ya Serikali na vyama vya wapinzani. Ni kitendo kitakachozusha mapambano kati ya Serikali na wananchi ambao siyo wanachama wa CCM na hao ndiyo walio wengi.

Kwamba tayari Serikali imeanza kupambana na wapinzani ni jambo la wazi kabisa. Hatuwezi kusema kwamba ni siri. Bungeni wabunge wa vyama vya upinzani wanasumbuliwa, wanaonekana kama ni wabunge feki.

Wanachama wa Chadema walipoanza ziara ya kukutana na wananchi wakianzia Kahama, mikutano yao ilipigwa marufuku siku hiyo hiyo nchi nzima kwa kisingizio cha kudumisha amani. Madai hayo ya Serikali yangeweza kuungwa mkono na wananchi kama tu wapinzani wangepewa nafasi ya kufanya mkutano wao Kahama na kuonekana kwamba wamevuruga amani.

Mkutano wa Kahama ulizuiwa eti kwa sababu ungekuwa wa uchochezi wakati Mahakama zipo zinashughulikia wachochezi? Kwa nini hao wapinzani hawakupewa nafasi ya kuchochea kisha wakakamatwa? Na tangu lini kuzuia mikutano ya hadhara ya wapinzani nchi nzima kunamaliza tatizo? 

Viongozi wa Chadema walizuiwa hata kuingia ofisi ya chama chao, sawa hiyo? Kule Dodoma katika Hoteli ya African Drea polisi waliwatawanya kwa mabomu wahitimu wa Chadema wa vyo vikuu kufanya mahafali. Hakuna sababu moja iliyotolewa.

Mara mikutano ya hadhara imezuiwa nchi nzima kuanzia siku hiyo, mara kuna ugonjwa usiojulikana uliotokea Dodoma huku wananchi wakiendelea kukusanyika sokoni, maofisini, makanisani na misikitini, mara kufanyika kwa mahafali hayo hotelini hapo kungezuia wateja wengine kuingia hotelini wakati ni mwenye hoteli mwenyewe aliyetoa nafasi hiyo! Na mara pale palikuwa na bendera za Chadema, Kwa nini mkusanyiko wa wana-Chadema ukose bendera za Chadema?

Sababu hizi zote zilizotolewa na polisi katika kuhalalisha kitendo chao cha kuzuia mikutano ya wapinzani, inathibitisha kwamba Serikali imeamua kupambana na upinzani kwa lengo la kuufutilia mbali.

Kana kwamba hiyo haikutosha, polisi walitumia nguvu kuwatawanya wahitimu wa vyuo vikuu kupitia umoja wa Chadema (CHASO) waliokuwa wamekusanyika mjini Moshi kwa ajili ya mahafali yao katika Hoteli ya Keys. Polisi walidai kuwa mikusanyiko ya aina hiyo ilikuwa imezuiwa. 

Watu wanatumia gharama kubwa kusafiri na kuandaa shughuli zao, kukuta polisi wanazuia shughuli hizo kufanyika. Hali hii inajenga urafiki au uhasama kati ya polisi na raia? Hakika tumefikishwa mahali pabaya.

Hapana shaka mtu atataka kujua kilichosababisha kuzuia mikutano ya wapinzani nchi nzima. Na ni muhimu tutafute sababu hiyo kisayansi na wala si kwa kukurupuka.

Nionavyo mimi (na nina hakika watu wengine wataona hivyo), mambo yote haya yanayotokea leo ni matokeo ya chama tawala na Serikali yake kuhofia kwamba kwenye mikutano yao wapinzani watazungumzia matokeo halisi ya Uchaguzi Mkuu uliopita, ambayo yalitofautiana na matokeo yaliyodaiwa kwamba yalikuwa yamepikwa.

Turudi nyuma, kwa Edward Lowassa, mtu aliyegombea urais kupitia Ukawa. Yeye ameendelea kudai kwamba ni Ukawa iliyoshinda uchaguzi ule ikaporwa ushindi. 

Na majuzi tu alipozungumza katika mahafali ya shirikisho la wanafunzi wa vyuo vikuu wafuasi wa Chadema (Chaso) akieleza watawala walivyomleta nchini rafiki wa Lowassa, mtumishi wa Mungu TB Joshua kutoka Nigeria, ili amshawishi akubali matokeo ambayo hakuridhika nayo! 

Lakini baada ya TB Joshua kupata ukweli wa mambo alichukia kiasi cha kusitisha azma yake ya kuhudhuria sherehe za kumwapisha Rais John Magufuli.

Katika jambo hili, chama tawala na Serikali yake vipo njia panda. Hawawezi kumfikisha Lowassa mahakamani kwa sababu Mahakama itathibitisha ushindi wa Ukawa katika uchaguzi ule. Kwa hiyo, wamekubali kumsema vibaya Lowassa.

Ni muhimu watawala wetu waanze kutuandalia sasa uchaguzi huru na wa haki ili amani yetu isipotee kabisa. Lengo la chama cha siasa ni kushika Serikali au kuendesha nchi. Lakini ni nani kaihalalisha CCM kuwa chama tawala mpaka kiama?