Nà Mwandishi Wetu,JamuhuriMedia, Dar ea Salaam

UONGOZI wa Tanzania Top Record (TTR), umebainisha kuwa wamejipanga kutembea kilometa moja pekupeku ikiwa ni ishara ya kuenzi viongozi na watu mbalimbali ambao wamepambania taifa na kuacha alama hapa nchini.

Hayo yamebainishwa Aprili 7, 2024 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mtendaji wa T TR, Rahimu Idd, wakati wakijitambulisha kwa waandshi wa habari na kufafanua kuwa watakuwa wakishughulika na ukusanyaji, uchakataji wa taarifa za makundi ya watu katika nyanja mbalimbali ikiwemo viongozi wa dini,wanasiasa, wanamichezo na wengineo.

Amesema lengo la kufanya hivyo ni kutambua watu ambao wamepata nafasi katika nyanja tofauti nchini na kufanya vitu vya kuwasaidia jamii na kuacha alama ambazo zinastahili kuigwa kizazi hadi kizazi ili kuleta mfanikio kwa taifa na kudumisha amani iliyopo.

“Tunaamini wapo viongozi na jamii nyingi ambao wamefanya makubwa nchini na inawezekana mchango wao usionekana kwa sababu mbalimbali ingawa ukikaa ukitulia unaona na kitu kimefanywa na mtu na imesaidia kuleta maendelea nchini.

“Mfano Rostam Azizi yeye ndiye aliyekuja na wazo kwa wananchi wake kuwa na bima ya afya wakati huo alipokuwa mbunge jambo ambalo rais wa wakati huo, Hayati Benjamin Mkapa alilibeba na kuwa la kitaifa, sasa hiyo ni alama ambayo Rostam ameiweka na inastahili kusemwa na kuhifadhiwa kama sehemu ya kumbukumbu nchini,” amesema.

Ameongeza ukiachana na Rostam wapo viongozi wengi ama watu wa kawaida wameweka alama nchini na hawatajwi, hivyo wao watakuwa ni sehemu ya kuwaibua kuwaweka kwenye majarida na kuwatangaza ili jamii iwajue na waheshimike kizazi hadi kizazi.


Amesema licha ya kuwa na mikakati hiyo pia watakuwa wakitoa tuzo kwa watu ambao watawaibua kuwa wameacha alama nchini ili kusaidia kusukuma wengine ambao wapo kwenye nafasi kufanya vizuri zaidi kwa ajili ya maendeleo ya nchi na kufanya kitu kitakachokuwa alama kwa wengine.

Amefafanua kuwa siku hiyo ambayo watatembea bila kuvaa viatu katika barabara ambayo watachagua, mwisho wa matembezi hayo watatumia dakika 20, 10 zitakuwa kutoa fursa kwa viongozi wa dini kuliombea taifa ili lidumu kwenye amani na utulivu kuelekea Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Oktoba mwaka huu na Rais, Wabunge na Madiwani mwakani.

“Pia tunaomuomba Rais Dkt Samia Suluhu Hassan ikiwa ataridhia siku hiyo utupe ujumbe kwa ajili ya Watanzania hususan vijana wa kizazi hiki na vijavyo tuwe wamoja licha ya kuwepo changamoto za siasa na kiuchumi,” amesema.