πŸ“Œ Tanzania na Singapore kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara

Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa uhusiano wa Tanzania na Singapore ni wa muda mrefu na kuwa nchi hizo zinatakiwa kuangalia sababu za uwepo wa uhusiano huo na kuongeza kiwango cha ufanyaji biashara kati yake.

Dkt. Biteko ameyasema hayo Oktoba 21, 2024 akiwa nchini Singapore mara baada ya kukutana na kufanya mazungunzo na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Viwanda na Biashara wa Singapore Mhe. Gan Kim Yong.

β€œ Tunatakiwa kujifunza kutokana na uhusiano huu na hasa kutoka Singapore kwa kuwa mmepiga hatua katika sekta ya nishati hadi kuwa na uwezo wa kufikia mahitaji ya juu ya umeme ya zaidi ya Gigawati 8, hicho ni kiasi kikubwa ikilinganishwa na Tanzania yenye takribani Megawati 3000 ambapo hadi mwaka 2030 tumepanga kufikia Megawati 10,000,” amesema Dkt. Biteko.

Amesisitiza β€œ Mpango huo hauwezi kutokea bila kuwa na ushirikiano na wadau na nchi zingine kama Singapore, ni matumaini yetu kuona ushirikiano huu unaendelea kukua kati ya nchi zetu na kuleta manufaa kwa wananchi”

Dkt. Biteko ameipongeza Singapore kwa uzalishaji wa umeme wa jua na kusema kuwa Tanzania inaendelea na jitihada zake za kuzalisha umeme huo.

Akitaja miradi ya nishati inayoendelea kutekelezwa, Dkt. Biteko amesema kuwa kwa sasa nchi inaendelea na utekelezaji wa mradi mkubwa utakaozalisha megawati 2115. Aidha, upembuzi yakinifu unaendelea kuhusu miradi mbalimbali ya uzalishaji umeme.

Fauka ya hayo, Dkt. Biteko amemualika Naibu Waziri Mkuu wa Singapore, Mhe. Yong nchini Tanzania.

β€œ Kwa niaba ya Serikali na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tutafurahi ukija Tanzania na tuna amini kuna maeneo mengi ya kushirikiana nanyi,” amesema Dkt. Biteko.

Naye, Naibu Waziri Mkuu wa Singapore, Mhe. Yong amesema kuwa nchi yake ipo tayari kuendelea kushirikiana na Tanzania na kuwa nchi hizo zina mahitaji ya kufanana.

Aidha, amesema kuwa Singapore inategemea zaidi gesi asilia licha ya kutumia pia umeme unaozalishwa kwa maji, jua na upepe. Vilevile nchi yake iko tayari kushirikiana na Tanzania katika kubadilishana uzoefu wa masuala mbalimbali yanayohusu sekta ya nishati.