Na Tatu Saad, JAMHURI
Baada ya kupokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Yanga Sc katika hatua ya 16 bora wa kombe la shirikisho Azam ‘ASFC’ Tanzania Prisons wamesema wapo tayari kuwakabili Namungo Fc.
Akizungumza kocha mkuu wa Tanzania Prisons Mohamed Abdallah ‘Bares’ amesema wamejiandaa vizuri na wapo tayari kwa mchezo huo wa ligi kuu Tanzania Bara dhidi ya Namungo FC.
Bares amesema maandalizi yao na utayari wao ni kwaajili ya kujinasua katika nafasi waliyokuwepo na kuhakikisha wanabaki katika ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Aidha Bares amekiri kuwa safi yake ya ushambuliaji ndio ilikuwa ikifanya makosa kwa kushindwa kutumia nafasi wanazozipata, lakini amesema amemaliza tatizo hilo na sasa kikosi kipo tayari kwa mchezo.
Hata hivyo Bares alisema katika mechi nne alizosimamia na kupoteza alikua akitafuta muunganiko,kuondoa makosa ya kufungwa mabao mengi na kuwaandaa wachezaji wake kisaikolojia.
Kwa mantiki hiyo Bares ameweka wazi kuwa wataanza kuchukua alama tatu kuanzia kwa Namungo FC watakaovaana nao Jumamosi hii ya Machi 11 hadi mchezo wa mwisho msimu huu.
“Kwa sasa naona nimefanikiwa kutengeneza nafasi,kilichobaki ni namna ya kuzitumia. Ninaamini kuanzia mchezo wa Jumamosi dhidi ya Namungo tunaanza kuhesabu pointi tatu hadi mchezo wa mwisho msimu huu,” amesema Baresi.
Tanzania Prisons watakuwa ugenini Jumamosi ya Machi 11 mwaka huu kuwakabili Namungo FC ambao wapo nafasi ya Saba wakiwa na alama 32.
Maafande hao kutokea jijini Mbeya hawajawa na wakati mzuri katika ligi ya Tanzania bara msimu huu, wakicheza michezo 24, wakishika nafasi ya 14 na umiliki wa alama 22.