Wadau wa mchezo wa soka wameishauri Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania Tanzania (TFF) juu ya kufanya maboresho yatakayo saidia timu ya taifa kupata nafasi ya kushiriki katika mashindano kadha ya kimataifa ikiwemo Olympic inayotarajia kufanyika nchini Japan mwaka 2020.
Hivi karibuni TFF imeitangaza Timu ya Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 23 Kilimanjaro Worriors kwa ajili ya maandalizi ya awali ya kucheza mechi za kufuzu fainali za mashindano ya Olympic zinazotarajiwa kufanyika jiji la Tokyo, Japan 2020.
Katika mpango huo vijana wa Serengeti boys wanatarajiwa kuungana na vijana wa Airtel Copa Cacacala na baadhi ya vijana wa toka ligi ya vijana walio chini ya ummri wa miaka 20.
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti wadau wa michezo wamesema kuwa kuwaweka kambini vijana hao pekee hakutoshi bali ipo haja ya kuwa na mipango endelevu katika soka la vijana.
Mjumbe wa kudumu wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CUF) Said El Maamry, anasema bila kuwa na mipango endelevu tutabaki kuyasikia mashindano hayo kwenye vyombo vya habari.
Anasema pamoja na TFF kujitahidi kuliendeleza soka la vijana lakini bado kuna haja ya wadau wengine kuingilia kati kwa lengo la kusaidiana.
“TFF pekee hawawezi kuliwezesha soka letu kuweza kupata mafanikio tunayoyahitaji, ipo haja ya wadau wengine kuingilia kati kwa lengo la kuliokoa jahazi,” anasema El Maamry.
Anafafanua kuwa nchi ya Uganda walifuzu kushiriki katika fainali za Kombe la klabu Bingwa Afrika 2017 baada ya miaka 38, hivyo na sisi tunaweza kushinda na kuongeza kwa kuongeza nguvu kwani hakuna kinachoshindikana endapo kutakuwa na msimamo mmoja.
Aliyewahi kuwa kocha wa Timu ya taifa ‘Taifa starz’ Charles Mkwasa anasema kuna haja ya kuanza kuwa na mipango ya muda mrefu iwapo nchi inahitaji kupata nafasi ya kushiriki mashindano mbalimbali ya kimataifa ikiwemo Olimpiki nchini Japan 2020.
“Hatuwezi kupata nafasi ya kwenda Japan kama tutakuwa na maandalizi ya zima moto kama ambavyo tumekuwa tukifanya hata katika michezo mingine,” anasema Mkwasa.
Anasema ni vigumu kuweza kutimiza lengo la kushiriki mashindano ya mwaka 2020 kutokana na muda kuwa mchache.
“Miaka mitatu tu imebaki kufanyika kwa mashindano hayo kwa kuhesabu tunaweza kujifariji kwa muda, lakini kiuhalisia muda umekwisha na inatupasa kuwa na maandalizi makali kuanzia sasa,” anasema.
Akiongea na JAMHURI Mkurugenzi wa ufundi wa TFF Salumu Madadi, anasema kuwa kushirikiana na uongozi wa kampuni ya simu ya mkononi ya Airtel ambao wamekuwa na uhusiano mzuri katika kuhakikisha vijana wengi wenye vipaji wanapata nafasi ya kucheza mpira.
“Ni zaidi ya miaka sita TFF kwa kushirikiana na Airtel tumejitahidi kuwaandaa vijana ambao wengi wao ndio wapo kwenye timu zetu za taifa,” anasema Madadi.
Michezo ya Olympic ya kale ilifanyika tangu tarehe isiyojulikana lakini kwa uhakika kuanzia mwaka 776KK hadi mwaka 393 katika mtaa wa mahekalu wa Olimpia kwenye rasi ya peloponesi nchini Ugiriki.
Michezo ya Olympic ya kisasa ya kwanza ilifanyika mwaka 1896 mjini Athens Ugiriki mwanzilishi alikuwa raia toka nchini Ufaransa Pierre de Coubertin aliyetaka kutumia michezo hiyo kujenga uhusiano mzuri kati ya vijana toka mataifa mbalimbali kwa lengo la vijana kushindana viwanjani badala ya vitani.
Michezo ya Olympic imekuwa ikifanyika kila baada ya miaka minne isipokuwa mwaka 1916, 1940 na 1944 kwa sababu ya vita kuu ya kwanza na ya pili ya dunia kwa hiyo ni jukumu letu kama taifa kuunganisha nguvu kuhakikisha timu zetu zinafanya vizuri katika mashindano mbalimbali.