📌 Mpango Mahsusi wa kuharakisha upatikanaji umeme kwa Waafrika milioni 300 (Mission 300) kusainiwa
📌 Kupitia Mission 300 Tanzania itaunganishia umeme wateja milioni 8.3
Tanzania inatarajia kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika kuhusu Nishati baada ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuridhia ombi la Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).
Hayo yameelezwa na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu Mhandisi Innocent Luoga wakati akitoa wasilisho la ujio wa Mkutano huo katika Warsha ya Wahariri na Waandishi wa Habari iliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mhadisi Luoga amesema Mkutano huo utahusisha Wakuu wa Nchi 54 katika Bara la Afrika, MaRais wa WB, AfDB, Umoja wa Afrika, Mawaziri wa Fedha na Mawaziri wa Nishati.
Akielezea chimbuko la Mkutano huo, Mhandisi Luoga amesema takwimu zinaonesha kuwa, takribani Waafrika milioni 685 hawajafikiwa na huduma ya umeme hadi sasa kati ya Waafrika zaidi ya Bilioni 1 hivyo Benki ya Dunia kwa kushirikiana na Benki ya Maendeleo Afrika wamekuja na Mpango Mahsusi ujulikanao kama Mission 300 ambao umelenga kuharakisha upatikanaji wa umeme kwa Waafrika Milioni 300 ifikapo 2030.
Ameeleza kuwa, Mpango huo unahusisha nchi zote za Afrika ambapo nchi 14 zimechaguliwa kuanza utekelezaji wa Mpango wa Mission 300 na nchi nyingine zitafuata.
Amezitaja nchi hizo kuwa ni Tanzania, Mali, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Ivory Coast, Bukina Faso, Chad, Liberia, Madagascar, Malawi, Mauritania, Msumbiki, Niger, Nigeria na Zambia.
Ameeleza kuwa, Tanzania imeingizwa katika Mpango huo kwa kuwa ni nchi mwenyeji wa Mkutano kwani imeshapiga hatua kubwa katika usambazaji wa umeme kwa wananchi
Kuhusu uunganishiaji umeme wananchi, Mhandisi Luoga amesema kwa mwaka Tanzania inaunganishia umeme wateja takriban 500,000 na katika kipindi cha miaka mitano (2025-2030) inatarajia kuwaunganishia umeme wateja milioni 2.5, hadi sasa idadi ya Wananchi waliounganishwa umeme ni milioni 5.2 na kufikia mwaka 2030 wateja watakaounganishwa na umeme watakuwa ni milioni 7.7.
Ameeleza kuwa kupitia Mpango Mahsusi wa Kitaifa (National Energy Compact) wa M300 unaofadhiliwa na Benki ya Dunia (WB), Benki ya Maendeleo ya Africa (AfDB) na Wadau wengine wa Maendeleo, Tanzania itaweza kuunganishia umeme watanzania milioni 13.5 yaani karibu mara mbili ya uwezo wake katika kipindi hicho cha miaka mitano na hivyo kufanya ongezeko la wateja milioni 8.3.
Ametaja faida nyingine za Mpango mahsusi wa M300 kuwa ni pamoja na kuongeza kiasi cha upatikanaji wa nishati safi ya kupikia na kuongeza kiwango cha nishati ya umeme itokanayo na umeme jadidifu ikiwa pamoja na jua, upepo na jotoardhi.