Na Mwandishi wetu
NCHI ya Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa kongamano la 10 la Jotoardhi Afrika (ARGe-C10) ambapo takribani washiriki 1000 kutoka mataifa mbalimbali wanatarajiwa kushiriki .
Kongamano hilo litafanyika kuanzia Novemba 11 hadi 17, 2024 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Hayo yamebainishwa jijini Dar es salaam leo Machi 18 na Kamshina wa Umeme na Nishati Jadilifu, Mhandisi Innocent Luoga wakati wa Uzinduzi wa maandalizi ya kongamano hilo amesema kongamano hilo la jotoardhi litahusuisha nchi 50 zikiwemo wanachama wa ARGeo ambazo ni Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Ethiopia na Djibouti
“Watu takribani 1,000 wa kada mbalimbali zinazohusiana na sekta hii muhimu katika kuzalisha nishati safi na salama wanatarajiwa kushiriki.”amesema mhandisi Luoga
Amesema mwaka 2022 Rais Samia Suluhu Hassan alikubali ombi la Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) kufanyika kwa kongamano hilo, hivyo kuanzia sasa Tanzania inaendelea na maandalizi ili liweze kufanyika.
“Kongamano hili ni muhimu kwa Tanzania kutokana na kuwa na rasilimali nyingi za jotoardhi, hivyo matumaini ya washiriki ni kujifunza l na kubadilishana taaluma”amesema Mhandisi Luoga
Aidha amesema Serikali kupitia Kampuni ya Uendelezaji Jotoardhi Tanzania (TGDC) itashirikiana na UNEP kuhakikisha kongamano hilo muhimu linafanikiwa kwa kiwango kikubwa, ili dhamira ya serikali kuongeza nishati jadidifu inafikiwa.
Vilevile amesema katika kongamano hilo litakutanisha wataalam, wawekezaji, wafanyabiashara na viongozi mbalimbali ambao watapata nafasi ya kuchochea kasi ya uzalishaji nishati hii.
Aliendelea kueleza kuwa nchi Tanzania inaweza kuzalishaji megawati 5,000 za umeme wa jotoardhi huku kwa sasa wakitekeleza miradi mbalimbali ambayo inatarajiwa kuzalisha megawati 200 ifikapo 2027 jambo ambalo litasaidia nchi kukabiliana na changamoto ya umeme.
“Tuna maeneo matano ambayo tumeyaainisha kwa ajili ya uzalishaji wa nishati ya jotoardhi ambayo ni ngozi tutazalisha megawani 70, Kiejo Mbaka megawati 60, , Natron megawati 60, Songwe megawati tano na Ruoyi Kisaki megawati tano, hadi kufikia megawati 200,” amesema
Kwa upande wake Meneja wa TGDC, Mhandisi Mathew Mwangomba amesema kongamano hilo limekuja wakati muafaka kwa kuwa dunia ipo katika mapambano ya kupunguza hewa ukaa ambayo imekuwa na madhara makubwa katika mazingira.
Amesema upatikanaji wa jotoardhi nchini unaendana na hatua tatu muhimu ambazo ni sayansi jiolojia, jiofizikia na jiokemia ambayo ipo nchini kupitia Bonde la Ufa la Magharibi, Mashariki na Kusini (Tripple Juction).