Waziri wa Katiba na Sheria Dk Pindi Chana amesema Tanzania na Morocco zinafurahia uhusiano wa muda mrefu kati ya nchi hizo mbili uliosaidia kuleta manufaa katika sekta mbalimbali.

Akizungumza Dar es Salaam kwenye maadhimisho ya miaka 25 tangu kutawazwa Mfalme Mohammed wa VI wa Morocco Dk Chana amesema mahusiano hayo yaliyoanza tangu ukoloni na baada ya uhuru yamedumu na kuendelea kuimarika zaidi baada ya ziara ya kiserikali ya Mfalme huyo hapa nchini Oktoba 2016.

Amesema katika ziara hiyo mikataba 22 ilisainiwa katika maeneo mbalimbali ya ushirikiano, ikiwemo ulinzi na usalama, biashara na uwekezaji, kilimo, utalii, usafiri, afya, elimu, utamaduni na michezo.

“Napenda kuishukuru Serikali ya Ufalme wa Morocco kwa misaada mbalimbali inayotolewa kwa Tanzania katika sekta mbalimbali. Mbali na uhusiano wa nchi mbili, nchi zetu mbili pia zinafanya kazi kwa karibu sana katika ngazi za kikanda na kimataifa hasa ndani ya mfumo wa Ushirikiano wa Umoja wa Afrika(AU), Umoja wa Mataifa(UN) na nchi za Kusini-Kusini,”amesema.

Dk Chana amesema Tanzania inatilia maanani maendeleo ya mahusiano hayo ya muda mrefu ya nchi hizo mbili na itaendelea kushirikiana na Morocco kusukuma maendeleo mapya yenye manufaa kwa pande zote mbili.

Balozi wa Ufalme wa Morocco hapa nchini Zakaria El Goumiri.

Kwa upande wake, Balozi wa Ufalme wa Morocco hapa nchini Zakaria El Goumiri amesema ushirikiano wa nchi hizo mbili umestawi kote na mara kwa mara mazungumzo ya kisiasa yameongezeka. Pia, yameonyesha ubora uratibu na ushirikiano katika vikao mbalimbali vya kikanda na kimataifa.

Amesema kumekuwa na ongezeko kubwa la biashara kati ya nchi hizo ambapo takwimu zinaonesha ukuaji mkubwa kutoka Dola milioni 28 mwaka 2016 hadi dola milioni 285.5 mwaka wa 2022.

Goumiri amesema ushirikiano umeendelea katika maeneo mbalimbali ikiwemo utoaji wa mafunzo na elimu, Morocoo ikiongeza idadi ya udhamini kwa wanafunzi wa Kitanzania katika nyanja muhimu kama vile dawa, uhandisi, na utalii.

Amesema serikali zote mbili zimeazimia kuandaa Jukwaa la pili la Biashara la Morocco-Tanzania baadaye mwaka huu. litakalotumika kuchunguza fursa mpya za uwekezaji, kujenga ushirikiano imara na kuendeleza maendeleo ya nchi zote mbili.

“Ninakushukuru tena kwa kuungana nasi katika jambo hili muhimu kusherehekea na uhusiano kati ya Morocco na Tanzania uendelee kuwa na nguvu,,”amesema.