Makamu Rais wa Benki ya Dunia wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika, Victoria Kwaka, ameipongeza serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta “miujiza” kwenye uchumi.
Kwaka ameipongeza Tanzania kwa utulivu wa uchumi wake wakati nchi mbalimbali duniani zikiwa kwenye msukosuko wa uchumi unaotokana na vita ya Ukraine na sababu nyingine.
Amesema wakati nchi mbalimbali zikihangaika na janga la mfumuko wa bei wa tarakimu mbili, huku akiitaja Ghana kuwa na mfumuko wa bei wa asilimia 30, Tanzania imeweza kuwa na mfumuko wa bei wa tarakimu moja tu.
Taarifa kutoka Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonesha kuwa Mfumuko wa Bei wa Taifa kwa mwaka ulioishia mwezi Septemba 2022 ni asilimia 4.8.
“Tumeona karibu nchi zote duniani zikiwa na akiba ya fedha za kigeni dhaifu, lakini Tanzania imeweza kuwa na akiba ya fedha za kigeni inayotosha kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje za kipindi cha takribani miezi mitano,” Kwaka alisema katika mazungumzo jijini Washington DC na msafara wa viongozi wa Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Mwigulu Nchemba.
“Tunaona mataifa mengi yakihangaika na nakisi kubwa ya bajeti, wakati Tanzania nakisi yake ya bajeti ni sawa na asilimia 3.5 tu ya Pato la Taifa. Nimemuuliza Waziri wa Fedha wa Tanzania kuwa wamewezaje kufanya miujiza hii? Hili ni jambo la kupongezwa sana na niwape moyo muendelee na usimamizi huu makini wa uchumi.”
Kwaka pia aliipongeza Tanzania kwa kuwa na sera nzuri za fedha na uchumi zinazoleta utulivu kwenye uchumi.
“Mfumuko wa bei ni kama kodi mbaya ambayo inaumiza zaidi wananchi masikini. Naipongeza Tanzania kwa jitihada zake zote za kudhibiti mfumuko wa bei,” alisema.
“Ni matarajio yetu kuwa tutaitumia Tanzania kama mfano bora wa kuigwa na nchi nyingine duniani.”