Na Shamimu Nyaki, JamhuriMedia
Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amafanya mazungumzo na Balozi wa Marekani hapa nchini Michael Battle yaliyojikita katika kuendeleza Sekta za wizara hiyo.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika leo Oktoba 3, 2023 jijini Dar es Salaam, Mhe. Dkt. Ndumbaro amemueleza Balozi huyo nia ya Tanzania kuwasilisha mapendekezo ya matumizi ya lugha ya Kiswahili katika Umoja wa Mataifa na kuomba nchi hiyo iunge mkono suala hilo, kwa kuwa lugha hiyo tayari inatumika katika Jumuiya ya Afrika Mashariki, Kusini mwa Afrika na Umoja wa Afrika.
Kwa upande wake Balozi wa Marekani Mhe. Battle ameipongeza Tanzania kwa kufuzu kucheza Mashindano ya Kombe la Mataifa Barani Afrika yatakayofanyika mwakani nchini Ivory Coast, ambapo amesema nchi yake ipo tayari kutoa ufadhili kwa vijana wenye vipaji katika michezo na Sanaa kwa kuwa Taifa hilo limepiga hatua kwenye eneo hilo, na pia kutoa utalaamu kwa makocha wa michezo mbalimbali.
Awali Katibu Mkuu Bw. Gerson Msigwa amesema kuwa Tanzania inakusudia kuwa na vituo vya michezo katika majiji pamoja na vituo vya kuhifadhi utamaduni, hivyo ameikaribisha nchi hiyo kuunga mkono jitihada hizo.