Serikali imefanikiwa kutimiza masharti ya itifaki namba tano ya azimio la Dar es Salaam la mwaka 2004 inayoweka utaratibu mzuri wa matumizi ya rasilimali, ikiwemo uchimbaji, uchakataji, usafirishaji na uuzaji wa madini.
Kutokana na kutekeleza masharti hayo, Tanzania sasa inaruhusiwa kutoa Hati ya Uhalisia wa madini ya bati ambayo yanapatikana kwa wingi mkoani kagera.
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo, amesema kuwa sasa Tanzania inaungana na nchi nyingine kadhaa za eneo la Maziwa Makuu kutoa hati hiyo na kuwezesha madini yake kuaminika zaidi katika soko la kimataifa.
“Tanzania inakuwa nchi ya nne kutimiza vigezo ili kuweza kutoa hati za uhalisia kwa madini ya 3T (tin – bati, tantalum na walfranite) yazalishwayo nchini wakati wa kuyauza nje ya nchi baada ya DRC, Rwanda na Burundi. Aidha, nchi za Uganda, Jamhuri ya Afrika ya Kati na Zambia zimo kwenye hatua za mwisho za kukamilisha mchakato huu ili nazo ziruhusiwe,” anasema Nyongo.
Hati hizo zimezinduliwa katika mkutano wa kimataifa wa madini uliofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na sasa wachimbaji wa madini hayo nchini wana uhakika wa kupata soko zuri la madini, kwa sababu yatakuwa na hati hiyo ambayo itayatambulisha rasmi.
Kwa mujibu wa Nyongo, hivi sasa Tanzania itapaswa kutoa hati ya uhalisia kwa kila mzigo wa madini hayo ambao utauzwa nje ya nchi na wanunuzi watatakiwa kuhakikisha kuwa hawanunui madini hayo nchini bila ya kuwa na hati hiyo.